The House of Favourite Newspapers

CCM Yalaani Mauaji Yanayotokea Pwani

0
Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Humphrey Polepole.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimelaani vikali mauaji ya baadhi ya viongozi, raia na askari polisi, wanaouawa kwa kupigwa risasi katika wilaya za Rufiji, Kibiti na Mkuranga mkoa wa Pwani, na kutoa pole kwa familia zilizoguswa na mauaji hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Humphrey  Polepole, amesema chama hicho kwa niaba ya wananchi kinawataka viongozi wenye dhamana na usalama wa wananchi kujitafakari, huku akisisitiza kuwa ikiwa mauaji hayo yataendelea, chama hicho kitaielekeza serikali kuwachukulia hatua.

Aidha, Polepole amesema anasikitishwa na ukimya wa vyama vya upinzani kuhusu mauaji hayo, ambapo ameeleza kipindi hiki vyama vyote bila kujali itikadi za kisiasa vingetakiwa kuungana kutetea uhai wa wananchi wa maeneo hayo ambao ndiyo wapiga kura wao.

“Sasa imetosha, yeyote mwenye dhamana ajitafakari kwani hatupendi kusema hali hii ikiendelea watu wawajibike, ingawa kuwajibika kwa sababu ya watu kupoteza maisha ni ustaarabu wa kiungozi. Viongozi wote na wenye dhamana mchukue hatua, sitaki tufike pahala niseme, CCM tutaielekeza serikali kuchukua hatua kwa walio na dhamana kwa kutowajibika katika majukumu yao,” amesema Polepole.

Ametoa rai kwa serikali kuendelea kufuatilia vitendo hivyo vya kikatili ili visiendelee kutendeka hapa nchini.

Polepole amewataka wananchi wa maeneo hayo ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji kutoa ushirikiano kwa vyombo vinavyohusika na ufuatiliaji wa matukio yanayoendelea kwa sababu wao ndiyo wahanga wakubwa na kwamba wanatakiwa kuwa msingi wa kulitatua tatizo hilo.

“Nimezungumza na baadhi viongozi wa dini, tunapenda kuona wanasimama kuwatetea Watanzania ambao pia ni waumini wa dini zetu; tunatakiwa tusimame pamoja kuzungumzia uhai wa raia, tukikaa kimya tutakuwa hatuwatendei haki wananchi wanaoendelea kuumia. Tunatambua wanapitia wakati mgumu,” amesema.

NA DENIS MTIMA/GPL

 

Leave A Reply