The House of Favourite Newspapers

CEED TANZANIA YATOA MAFUNZO YA KUKUZA, KUSIMAMIA BIASHARA

Bwana Archad Kato kutoka kampuni ya uzalishaji mvinyo ya Alko Vitanges akizungumzia fursa,uzoefu pamoja na changamoto mbalimbali katika ukuzaji wa biashara zao.
Bi Elizabeth Swai akizungumzia juu ya uzoefu wake wakatiwa semina ya CEED Tanzania Dodoma

 

 

Kituo cha Ujasiriamali na Maendeleo ya Utendaji (CEED), kimewakutanisha wajasiriamali mbalimbali jijini Dodoma katika semina iliyolenga kutoa elimu ya usimamizi na ukuzaji biashara zao ndani ya jiji la hilo.

 

Akizungumza na waandishi wa habari, mwakilishi kutoka CEED Tanzania, Fred Laiser, alisema semina hiyo ni kwa ajili ya kuwapa ujuzi wa namna ya kuboresha biashara zao, ushindani wa kusaka fursa mbalimbali kutoka na kuongeza kwa idadi kubwa ya watu baada ya serikali kuhamishia shughuli zake jijini Dodoma.

 

‘’Sisi CEED Tanzania lengo letu kuu ni kuwasaidia wajasiriamali hapa nchini kukuza biashara zao. Leo tupo hapa Dodoma kwa lengo la kuwapa elimu na kutoa fursa mbalimbali za kibiashara ambazo wajariamali wanaweza kuzichangamkia. Pia kuwakutanisha na wenzao wajifunze namna ya kukuza biashara zao, kutatua changamoto zao.’’ alisema Laiser.

 

Mbali na hilo, Fred Laiser ametumia nafasi hiyo kuwataka wajasirimali mbalimbali nchini kujitokeza kwa wingi katika semina mbalimbali za ujasiriamali hasa zinazoendeshwa na CEED Tanzania kwa ajili ya kupata ujuzi wa biashara zao na pia kufahamiana na wajasiriamali kutoka kila kona ya Tanzania.

 

Kwa upande wao, wanufaikaji wa mafunzo hayo Bi.Elizabeth Swai mwanzilishi wa kampuni ya ufugaji kuku ya AKM Glitters Limited na Archad Kato kutoka Kampuni ya uzalishaji mvinyo ya Alko Vitanges walizungumzia fursa, uzoefu pamoja na changamoto mbalimbali katika ukuzaji wa biashara zao.

 

‘’Nawapongeza sana CEED Tanzania kwa kutupa nafasi hii ya kujifunza na kukutana na wajasiriamali wenzetu ili kujifunza mambo mbalimbali kutoka kwao. Moja ya changamoto inayotukabili sisi wajasiriamali hapa nchini ni kushindwa kuendeleza biashara zetu mara baada ya kuanzisha. Wengi tunapenda kujiajiri lakini wachache ndiyo wanaofikia malengo yao. Ili kutatua changamoto hizi inatupasa kujifunza vitu vipya kila siku na kujaribu mara kwa mara mpaka pale biashara itakapoweza kujiendesha yenyewe ‘’. alisema Archad Kato.

 

Kwa upande wake, Elizabeth Swai ametumia nafasi hiyo kuwataka wajasiriamali kutumia vizuri teknolojia katika kujifunza masuala mbalimbali kwasababu teknolojia imerahisisha kila kitu kwasasa ikiwa ni rahisi kupata taarifa  mbalimbali zitakazowasaidia kujielimisha  kukuza biashara zao.

 

Semina hiyo ilihudhuliwa na wajasiriamali takribani 52 kutoka kona mbalimbali za Dodoma na nje ya Dodoma ambapo kwa pamoja waliweza kujadili masuala mbalimbali katika kukuza biashara zao, namna ya kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika shughuli zao za kila siku za ujasiriamali.

Comments are closed.