The House of Favourite Newspapers

CHADEMA Watangaza Kumuombea Tundu Lissu Jumapili Hii (Video)

0
MAKAMU Mwenyekiti wa Baraza la Vijana CHADEMA Taifa (BAVICHA), Patrick Ole Sosopi amefunguka na kusema wao kama chama wameamua kuwakutanisha wanachama wao mbalimbali wa imani tofauti kwa ajili ya kufanya maombezi ya kitaifa kumuombea Mbunge Lissu.
Akiongea na waandishi wa habari leo Makao Makuu ya CHADEMA, Sosopi amesema kuwa jambo hilo halihusiani na mambo ya kisiasa bali wameamua kukutana kwa lengo la kuombea taifa katika mambo mbalimbali ikiwa pamoja na kuliombea jeshi la polisi ili wafanye kazi zao kwa kufuata misingi ya haki na usalama zaidi.
“Madaktari wamefanya kazi kubwa sana kuendelea kuokoa maisha ya Tundu Lissu na sisi tumekaa na kufikiri kwamba ni bora tukutane ili kwa pamoja tuweze kufanya maombezi, tunajua chama chetu kina kila aina ya watu wenye imani mbalimbali ya dini, hivyo Baraza tumeandaa maombo maalum kwa ajili ya Mhe. Tundu Lissu na kuita ‘Tanzania National youth Prayer for Lissu’ tutafanya maombi hayo ya kitaifa na kutoa wito kwa watu wote, jambo hili si la kisiasa na wala halina sura ya kisiasa,” alisisitiza Sosopi.
Aidha Sosopi amesema kuwa wanategemea kufanya maombezi hayo siku ya Jumapili jijini Dar es Salaam maeneo ya Sinza Darajani viwanja vya TP na kudai kwamba mpaka sasa wamefanya maandalizi yote ikiwa pamoja na kuandika barua kwa taasisi zote za dini kuweza kufika kwa ajili ya maombezi hayo.
Mbali na hilo Sosopi amedai kuwa kwa kuwa wanaamini jambo hilo halina sura ya kisiasa hivyo wanategemea kuona jeshi la polisi nchini likifika kwa lengo la kutoa ulinzi kwa raia ambao watafika kwa ajili ya maombezi hayo na si vinginevyo.
“Naomba jambo hili lisitafsiriwe vibaya sisi, kama viongozi wa kisiasa tutakwenda pia kusikiliza maombi na si kwenda kuongea chochote, tutakwenda uwanjani kwa sababu sisi kama CHADEMA hatuna kanisa wala msikiti kufanya maombezi hayo ndiyo maana tunakwenda uwanjani hapo, tunaamini hapo ni sehemu sahihi kuweza kuwakutanisha watu wetu wote bila kujali itikadi zao,” alisema Sosopi.
VIDEO YA TAMKO HILO

Leave A Reply