The House of Favourite Newspapers

Chadema Yalaani Kutekwa Mgombea Udiwani Muleba

Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dkt. Vincent Mashinji (katikati) akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.

 

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimelaani kitendo cha mwanachama wake, Athanas  Makoti, ambaye ni mgombea udiwani katika kata ya Buhangaza wilayani Muleba kutekwa na watu wasiojulikana na  kumtaka kujitoa katika kinyang’anyiro ya udiwani.

 

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa chama hicho,  Dtk. Vincent Mashinji,  amesema  jeshi la polisi linatakiwa kufanya uchunguzi wa haraka ili  kubaini waliomteka mgombea huyo wa udiwani.

 

Amesema kuwa Makoti alitekwa Februari 2 mwaka huu katika mazingira ya kutatanisha na  kupatikana Februari 5 akiwa ametelekezwa  eneo la  Hospitali ya Kagando  iliyoko Muleba ambako mpaka sasa ndipo amelazwa.

 

Amesema kuwa watekaji walimteremsha katika bodaboda aliyokuwa amepanda wakati akitokea kwenye  mchakato wa kampeni za udiwani ambapo watekaji hao walikuwa ndani ya gari aina ya Toyota RAV 4.

 

Ameongeza kuwa Makoti alitakiwa kukukubali kupokea pesa ambazo walikuwa nazo  ili  aweze kujitoa katika kinyang’anyiro hicho cha udiwani  lakini baada ya kukataa ndipo alianza kusulubiwa hadi hapo walipotimiza azima yao.

HABARI NA DENIS MTIMA | GLOBAL PUBLISHERS

 

 

Comments are closed.