The House of Favourite Newspapers

Chama Apiga Hesabu za Nusu Fainali CAF

0

KIUNGO Mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama, amesema wachezaji wote wana shangwe la kutosha baada ya kufanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakiwa wanaongoza msimamo wa Kundi A.

 

Simba imefuzu hatua hiyo baada ya kumaliza na pointi 13 wakifuatiwa na Al Ahly waliokusanya pointi 11. Hatua ya robo fainali itachezeshwa Aprili 30, mwaka huu.

 

Akizungumza na Spoti Xtra, Chama alisema kuwa kwa sasa mawazo yote ni kuona wanatinga nusu fainali ya michuano hiyo mikubwa barani Afrika, hilo linawezekana kwao kutokana na ubora wa kikosi chao.

 

Chama alisema kuwa licha ya kufungwa katika mchezo wa mwisho bao 1-0 dhidi ya Al Ahly uliochezwa Misri, lakini bado wana kikosi imara kitakachowapa matokeo mazuri na kufuzu nusu fainali.

 

“Haikuwa kazi rahisi lakini tunashukuru kufika hatua ya robo fainali. Lakini kwa sasa lengo letu kubwa ni kufika nusu fainali. Ni wazi ushindani utaongezeka katika hatua tuliyofika lakini kama ikitokea hatujafuzu, basi bahati haitakuwa yetu.

 

“Tutaendelea kupambana kutafuta matokeo ndani ya uwanja ili tufanikishe malengo yetu lakini pia kuwapa furaha mashabiki wetu ambao wanatuunga mkono kwa bidii wakati wote,” alisema Chama.

 

Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes, amezungumzia hatua ya robo fainali akisema: “Hatua ambayo inakuja ni ngumu zaidi kwa sababu tunakutana na timu ngumu, lakini tuna uhakika wa kufanya vizuri kwa sababu eneo letu la ulinzi limekuwa likitubeba sana.

 

“Haliruhusu kufungwa mabao kirahisi na utaona tulikuwa sehemu ya timu ambazo tulifungwa mabao machache hadi tunamaliza hatua ya makundi. Naamini hata mechi zijazo litakuwa msaada kwetu.”Timu zilizotinga robo fainali ya michuano hiyo ni Simba, Al Ahly, Mamelodi Sundowns, CR Belouizdad, Wydad Casablanca, Kaizer Chiefs, Espérance na MC Alger.

STORI: WILBERT MOLANDI NA SAID ALLY, DAR

Leave A Reply