The House of Favourite Newspapers

Chegge acha kuwa muoga, usiyejiamini!

0

SAIDI Chigunda maarufu zaidi kama Chegge, pamoja na Amani Temba ‘Mh Temba’ ndiyo alama ya TMK Wanaume Family, lile kundi la vijana wa Temeke lililo chini ya usimamizi wa ‘Mkubwa’ Said Fella.

Ni kijana mpambanaji kwelikweli, kwani hatua aliyofikia ni kubwa ambayo imempitisha katika vikwazo vingi, hasa ushindani miongoni mwa vijana wanaotamani majina makubwa yenye hadhi katika Bongo Fleva.

Kusimama katikati ya ‘msitu’ wa wasanii, waliokuwa wamefunikwa na kivuli cha Juma Nature, halikuwa jambo dogo, kiasi cha kumpa jeuri Fella kutotikisika baada ya Nature kuamua kujiengua tunduni miaka michache iliyopita.

Fella alipata kiburi kwa kujua kuwa pamoja na wasanii wengi walio kundini mwake, lakini alivitegemea zaidi vichwa viwili, Chegge na Mheshimiwa Temba ambao kwa muda mrefu sasa, wametengeneza partnership ya hatari, inayowafanya wawe kama kundi, ndiyo maana hata katika shoo wanazoalikwa, hutajwa kama Chegge na Temba, maana mmoja hasimami peke yake!

Nikiri kuwa mimi ni miongoni mwa mashabiki wa kazi zao, kwa sababu siku zote nimekuwa muumini sana wa mtu anayepata mafanikio kwa kujituma. Ni kutomtendea haki, kama hatawekwa katika kundi moja la wasanii ambao mchango wao kwa Bongo Fleva ni wa kutukuka!

Hata hivyo, hivi karibuni alitoa kauli ambayo ilinifanya niwe na mawazo yanayosigana, kama aliitoa kwa bahati mbaya au yalitoka moyoni mwake. Na kwa kuwa hajajitokeza kurekebisha, niamini kuwa ndiyo aliyokusudia kuyafikisha kwa hadhara.

Chegge ambaye hivi sasa anatamba na kibao chake cha Sweety Sweety, alikiambia kituo kimoja cha televisheni kuwa yeye na patna wake, Mheshimiwa Temba, watapotea endapo kazi zao hazitasimamiwa na bosi wao, Said Fella.

Katika kuthibitisha hilo, alisema hata gharama ya fedha iliyotumika katika kutengeneza video ya kibao hicho, yeye hafahamu lolote, kwani mchezo wote ulimalizwa na Mkubwa Fella.

Ingawa lengo lake lilikuwa ni kuthamini kinachofanywa na Fella kwao, lakini kwa upande mwingine, kauli hiyo imemuangusha, kwa vile inaonekana kama mtu asiyejiamini, mwoga na asiyefuatilia mambo yake.

Ni aibu kwa msanii mkubwa kama Chegge kutoa kauli ya kinyonge namna hiyo, kwani siku zote tunawategemea wasanii wakubwa wawe mifano. Kauli hii ilipaswa kutolewa na underground anayetafuta kutoka, maana hajui ABC za game, tofauti na yeye ambaye hana asichokijua katika muziki!

Na hii ndiyo inayochochea hawa wanaoitwa mameneja kujiona miungu watu kwa wasanii. Mtu anatoa mamlaka kwa msimamizi wake kumsimamia kila kitu, kiasi kwamba ukweli mwingi nyuma ya pazia anakuwa haujui. Kama hajui hata video yake iligharimu shilingi ngapi, ana uhakika gani kama Fella ‘hampigi’?

Wasanii, hasa wakubwa mifano ya Chegge, lazima wakue kiakili ili kuwapunguza wababaishaji wengi wanaojiingiza kwenye sanaa kwa mgongo wa umeneja. Kuna sehemu ambazo msanii anatakiwa kusimama yeye kama yeye na meneja anatakiwa kumsikiliza.

Unashangaa kuona wasanii wengi wa Bongo mikataba mingi ya kazi zao hawaijui, wanapelekwapelekwa tu kama alivyothibitisha Chegge kuwa yeye huambiwa tu nenda huku rudi kule.

Matokeo yake ndiyo tunakuja kushuhudia vijana wetu wengi wakidondoka kimuziki kwa sababu ya ubovu wa mipango yao, wanaishia kutaja majina ya watu kuwa ndiyo waliowaangusha, badala wajilaumu wenyewe kwa kutojitambua.

Dunia imeshabadilika, wasanii wanatakiwa kutambua wajibu, mipaka na majukumu ya kila anayewazunguka katika kazi zao, maana wasichokijua ni kuwa mwisho wa siku, wao ndiyo huwalipa watu wote walio katika crew, hata kama kwa macho ya kawaida, wanaonekana kama wanasaidiwa!

Leave A Reply