Chelsea Yazifanyia Kitu Mbaya Timu za Manchester, Bosi Mpya Aonesha Jeuri ya Pesa
BOSI mpya wa klabu ya Chelsea ya nchini Uingereza Todd Boehly ameonesha jeuri ya pesa kwa vilabu vya Manchester baada ya kuingilia dili mbili za wachezaji Marc Cucurella anayewaniwa na klabu ya Manchester City pamoja na Frenkie De Jong wa FC Barcelona.
Taarifa zinadai kuwa Chelsea wapo katika hatua za mwisho za kukamilisha dili la kuinasa saini ya Beki wa kushoto wa Klabu ya Brighton and Hove Albion raia wa Hispania Marc Cucurella kwa ada ya paundi milioni 50 baada ya kuipiku ofa ya Manchester City ya paundi milioni 35 iliyokataliwa hivi karibuni.
Aidha Chelsea imeanza mazungumzo na Klabu ya Barcelona kuangalia uwezekano wa kukamilisha dili la kiungo wao mkabaji raia wa Uholanzi Frenkie De Jong kwa ada inayokadiriwa kufikia kiasi cha Paundi milioni 80.
Tayari Manchester United ilikuwa imekwishakubaliana na FC Barcelona kukamilisha dili la uhamisho wa kiungo huyo ingawa changamoto ikabaki kwa mchezaji mwenyewe ambaye ameonesha nia ya kutotaka kujiunga na miamba hiyo ya soka nchini Uingereza.
Hadi sasa Klabu ya Chelsea imekamilisha usajili wa nyota wawili Raheem Sterling kutoka Manchester City pamoja na Mlinzi Kalidou Koulibaly kutoka klabu ya Napoli ya nchini Italia.