Chemical; Elimu Inafanya Apotee Kwenye Gemu

UKIWA unataja listi ya marapa bora wa kike Bongo, utawashangaza wengi kama ukiliacha jina la Chemical, ambaye kwa kipindi cha hivi karibuni amekuwa mmoja wa wasichana wanaofanya poa kwenye gemu ya rapu.

 

Chemical ambaye jina lake halisi ni Claudia Lubao, alifahamika zaidi mwaka 2015, baada ya kuachia Wimbo wa Sielewi, akimshirikisha Saprano, ngoma ilifanya vizuri na kushika chati mbalimbali za muziki wa Bongo Fleva.

 

Baada ya Sielewi, ikawa ni mawe juu ya mawe, kama Am Sorry Mama, Mary Mary, Tila Lila, Kama Ipo Ipo Tu akiwa na Msaga Sumu, Asali akiwa na Beka Flavour, Mjipange akiwa na Mr Blue na magoma mengine makali ambayo yaliimbwa sana kitaa.

 

Lakini wakati watu wanataraji mengi kutoka katika muziki wake, ghafla nguvu yake ikaanza kupungua taratibu na hata ile spidi ya kutoa nyimbo ikawa inapotea. Ndipo Championi Jumatatu likakaa naye kwenye Kilinge na kumdodosa ili kujua nini kinamkwamisha kuachia ngoma mfululizo na hapa Chemical anaanza kumwagika:

 

“Ni kweli spidi yangu ya kuachia kazi imepungua tofauti na kipindi cha nyuma, kwa sasa nimekua nikiachia ngoma kwa ajili ya kuwaridhisha mashabiki wangu lakini siyo kufanya kama kazi.

 

“Lakini siyo kwamba sipendi kutoa nyimbo mfululizo, ila kuna mambo mengine nafanya nje ya muziki, ambayo yanafanya nishindwe kutenga muda mwingi wa kurekodi ngoma.

 

“Kwa sasa nimerudi tena chuo kuongeza elimu kidogo, kama unavyojua muziki unahitaji muda, hauwezi kufanya mguu mmoja nje mwingine ndani lazima utafeli,” anasema Chemical.

 

NINI KIMEKURUDISHA CHUO WAKATI TAYARI ULISHAMALIZA?

“Elimu haina mwisho ndugu yangu, baada ya mwaka jana kumaliza ‘Bachelor Degree in Fine and Performing Arts’ pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwa sasa naendelea tena, nachukua ‘Masters in Culture and Heritage’.

 

“Unajua kwenye maisha kila mtu na ndoto zake, kwa hiyo mimi nilikuwa na ndoto ya kufanya muziki, nimeshafanya na nimeona manufaa yake, kwa hiyo nimeona bora niongeze elimu tena kwa sababu sitaki nifanye muziki maisha yangu yote, itafika wakati nitasimama na kufanya shughuli zangu nyingine.

 

KWA HIYO KWA MWAKA HUU TUSITEGEMEE KUONA KAZI ZAKO KWA WINGI?

“Unajua nilishaachia ngoma nyingi sana miaka ya nyuma hata mwaka jana, lakini kwa 2020 malengo yalikuwa ni kuachia albamu, ninatamani sana nitoe albamu ambayo itaenda kwa mashabiki wangu, kama hilo litatimia basi mashabiki watanisikia sana. Unajua nikitoa albamu nitapata muda wa kupumzika na kufanya mambo ya shule zaidi.

 

MIAKA MITANO KWENYE GEMU KUNA NINI AMBACHO UMEFAIDIKA NACHO?

“Namshukuru Mungu kuna vitu vingi sana ambavyo nimepata, mwanzo watu walikuwa hawamjui Chemical, lakini sasa hivi najulikana, bado umri wangu mdogo lakini naendesha maisha yangu mwenyewe bila kutegemea wazazi, ikiwemo ishu za shule.

 

“Lakini kubwa zaidi ni kuwa kama kioo kwa wasichana wengi ambao kila siku wanatamani kuwa kama mimi, wengine ni wanafunzi, wengine ni wasichana wadogo wote wanataka kuwa kama mimi, kwa hiyo hicho ni kitu kikubwa sana kwangu, ukiona watu wanataka kuwa kama wewe maana yake unafanya kitu kizuri na jamii inakubali.

 

KWA HIYO UNA MPANGO WA KUANZISHA LEBO YA MZIKI?

“Ndoto hizo zipo na tayari nimeanzisha lebo inayoitwa Chemilight lakini bado haijaanza kufanya kazi rasmi, natamani siku moja niweze kuwasaidia wasichana wenye kipaji cha muziki, ili waepukane na tabu ambazo nilipitia mimi.

 

ULIWAHI KUFANYA MUVI NA WEMA, VIPI ILIKULIPA?

“Kusema ukweli ile Muvi, ilitayarishwa na uongozi wangu wa mwanzo, licha ya kuwa wazo la Muvi lilitokana na wimbo wangu wa Mary Mary.

 

“Kwa bahati mbaya kuna vitu vilitokea baina yangu na uongozi, kwa hiyo ikabidi fedha ambayo nilitakiwa kuulipa uongozi wangu kwa kuvunja mkataba itoke kwenye muvi, kwa sababu kwa wakati huo sikuwa na hiyo hela ya kuwalipa, kwa hiyo sikupata chochote kutoka kwenye ile kazi, labda faida niliyoipata ni kujifunza zaidi kuhusu mambo ya kuigiza.

 

KUKAA KWAKO KIMYA KUNAMPA MWANYA ROSA REE KUWA KAMA MALKIA WA RAPU, UNAIZUNGUMZIAJE HIYO?

“Mimi sijawahi kushindana na mtu kwenye muziki, kwa sababu mimi nina ‘taste’ ya kipekee, ndiyo maana hata kama sifanya kazi kubwa, lakini utakuta watu wananiongelea na kunifananisha na wasanii wengine.

 

“Unajua kwa miaka hii miwili sijafanya muziki ‘serious’, lakini bado natajwa kila mahali, kitu ninachokiamini mimi hakuna mtu ambaye anaweza kuvaa viatu vya Chemical, hayo majina acha wapeane, lakini mimi ni mtu wa tofauti kabisa kwenye muziki wangu.

 

MPANGO WA KUOLEWA, KUWA NA FAMILIA VIPI?

“Kuolewa ni mipango ya Mungu, lakini mimi sijafikiria kuwa mke wa mtu kwa sasa, kwa sababu mume ni mwanaume, lakini upo utofauti wa kuwa na mume na kuwa na mwanaume.

 

“Kwa hiyo kumpata huyo mume ndiyo kazi kubwa, lakini kuwa na mwanaume ni rahisi, mimi sitaki kuwa na mwanaume ambaye atakuwa ananiwekea mipaka ya kufanya mambo yaliyopo kwenye ndoto zangu.

 

“Kuhusu familia ikiwemo kuzaa watoto hiyo ipo kwa sababu mimi ni mwanamke, lakini sijapanga kwa sasa kwa sababu bado nina mambo mengi sana nafanya, sitaki pia mwanangu apitie maisha ambayo mimi nimepitia, nataka aje akute mama yake staa na anaishi maisha mazuri.

 

USTAA UNAKUPA CHANGAMOTO GANI CHUO?

“Changamoto hazikosekani kwa sababu, ukishakuwa staa kuna vitu vingine unakuwa unashindwa kuvifanya, lakini pia usumbufu wa hapa na pale kutoka kwa wanafunzi nao upo sana, kwa hiyo inabidi wakati mwingine ukubali tu, kwa sababu tayari upo kwenye jamii hiyo,” anamaliza Chemical.

 


Loading...

Toa comment