Chikwende Apata Wakati Mgumu Simba SC

HAKUNA fundi wa mpira anayeweza kufanya kila jambo kwa usahihi uwanjani, hii imejidhihirisha kwa kiungo mshambuliaji mpya wa Simba raia wa Zimbabwe, Perfect Chikwende.

 

Katika mazoezi ya Simba yaliyofanyika Jumatatu ya wiki hii kabla ya kikosi hicho kwenda mkoani Mara kucheza na Biashara United, kiungo huyo alijikuta akipata wakati mgumu mbele ya kocha wa viungo wa timu hiyo, Mtunisia, Adel Zrane.

 

Tukio hilo lilifanyika ndani ya dakika tatu, ambapo Kocha Zrane aliwataka wachezaji wote kusimamia mguu mmoja huku wakiwa wamekanyaga juu ya kitu, ambapo Chikwende alionekana kupata wakati mgumu kiasi cha kushindwa kabisa kusimamia mguu mmoja.

 

Pamoja na kutokea kwa hali hiyo, Chikwende hakukata tamaa, ambapo aling’ang’ana hadi kocha alipobadilisha aina ya mazoezi.

 

Chikwende ambaye amejiunga na Simba kwenye dirisha dogo msimu huu akitokea FC Platinum ya Zimbamwe, tayari ameichezea Simba michezo miwili ya Ligi Kuu Bara na kufanikiwa kutoa pasi moja ya bao waliposhinda 2-1 dhidi ya Dodoma Jiji.

MUSA MATEJA, Dar es Salaam


Toa comment