The House of Favourite Newspapers

CHIRWA AACHWA DAR NA YANGA

 

Straika tegemeo wa Yanga, Obrey Chirwa

YANGA inatarajia kuondoka Dar es Salaam leo Jumapili asubuhi kuelekea Shelisheli tayari kwa mechi ya marudiano dhidi ya St Louis kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika itakayopigwa Jumatano jioni. Lakini katika hali iliyoshtua wengi ni ishu ya straika tegemeo wa Yanga, Obrey Chirwa kuachwa kwenye safari hiyo muhimu ya kuwania tiketi ya kufuzu raundi ya kwanza ya michuano hiyo yenye fedha nyingi zaidi Afrika kwa ngazi ya klabu.

Taarifa ya Yanga imeeleza kuwa Chirwa pamoja na Thaban Kamusoko watabaki kutokana na majeruhi.

 

Yanga wamesisitiza kwamba Chirwa ana maumivu ya misuli kwenye nyama za paja aliyopata katika mechi dhidi ya Majimaji jijini Dar es Salaam.

 

Habari zinasema kwamba Chirwa tayari alikuwa na tiketi yake ya safari ya leo pamoja na Kamusoko, jambo ambalo liliibua mjadala zaidi huku kwenye mitandao ya kijamii ikidaiwa kwamba aligoma kuwapa viongozi pasi yake ya kusafiria mpaka wampe masilahi yake.

 

Lakini habari za ndani zinasema kwamba pamoja na hilo, mchezaji huyo amewaambia baadhi ya viongozi kuwa
amefuatwa na vigogo wa Simba ambao wanamshawishi asaini mkataba wa awali wa kuichezea Msimbazi msimu ujao.

“Unajua Chirwa ni mtu smati sana, ni miongoni mwa wachezaji ambao huwa hawatafuni maneno. Ametufuata akatuambia kabisa kwamba watu wa Simba wamemshawishi na fedha ili akubali kusaini mkataba wao lakini akakataa.

 

“Wanajua kwamba mkataba wake unamalizika mwisho mwa msimu kwahiyo wamemfuata na yeye ametuambia kabisa bila kificho, sisi tumemwambia atulie kwanza,” alidokeza kiongozi mmoja mwenye ushawishi ndani ya Yanga.

 

Chirwa alipoulizwa jana kuhusiana na ishu hiyo alikata simu na kuizima kabisa. Habari zinasema kwamba Yanga wameanza kuingiwa hofu ya kumpoteza mchezaji huyo ingawa baadhi ya viongozi wamepuuzia. Baadhi ya viongozi wa Yanga wanadhani kwamba kinachofanywa na Simba ni kuwachezea akili kuwatoa kwenye njia ya ubingwa ingawa wengine wamekuwa wakijiuliza mara kadhaa.

 

Said Tully ambaye ni kiongozi wa kamati ya utendaji na mmoja wa vigogo wa usajili wa Simba, alipoulizwa jana alisisitiza kwamba kwa sasa wanakazania ubingwa ishu za usajili zitakuja baadaye

Comments are closed.