The House of Favourite Newspapers

Chirwa Aweka Rekodi Kaitaba

0

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Yanga, Mzambia, Obrey Chirwa, juzi Jumamosi alifanikiwa kuan­dika rekodi katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba tangu alipojiunga na Yanga msimu uliopita.

Rekodi hiyo si nyingine bali ni ya kuifunga Kagera Sugar kila alipokutana nayo kwenye uwanja huo ambao kwa sasa ni moja kati ya viwanja vizuri vinavyotumika katika michuano ya Ligi Kuu Bara.

Juzi Jumamosi aliiongoza Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika uwanja huo baada ya kuifungia bao la kwanza katika dakika ya 40 akimalizia pasi nzuri ya Ibrahimu Ajibu ambaye pia aliifungia timu hiyo bao la pili katika dakika ya 48 ya mchezo huo.

Hata hivyo, katika msimu uliopita akicheza mechi yake ya kwanza uwanjani hapo, Chirwa alifanikiwa kuifungia Yanga mabao mawili katika ushindi wa mabao 6-2.

Mabao mengine ya Yanga katika mechi hiyo yalifungwa na Donald Ngoma ambaye pia alifunga mawili, Simon Msuva na Deus Kaseke ambao kila mmoja alifunga bao moja.

Kutokana na hali hiyo Chirwa ameweza kuendeleza rekodi yake ya kufunga katika uwanja huo unaomilikiwa na Halmashauri ya Mji wa Bukoba.

 Sweetbert Lukonge, Dar es Salaam  

Leave A Reply