The House of Favourite Newspapers

Chongo!-10

0

Ulipoishia wiki iliyopita

“Yes, yupo kijana mmoja alikuwa amejeruhiwa sana, nafikiri na watu waliotaka kumuua, alikuwa hapa kwa siku tisa, leo ana wiki tangu tumtoe kumpeleka Mwaisela,” Dokta Jenny alimwambia Innocent akimuonesha picha ya kijana huyo.

Sasa endelea…

Nifowadie hiyo picha kwenye simu yangu, halafu ngoja niende nikamuone, ndugu yangu atafurahi sana,” Innocent alimwambia dokta Jenny ambaye aliipiga picha hiyo kutokea katika kompyuta na kumfowadia kwenye simu ya mwanafunzi mwenzake wa zamani.

Alipotoka nje ya MOI, Innocent alimpigia simu Jerry na kumweleza kuhusu ishu hiyo na akamfowadia pia picha ya kijana aliyopewa na Jenny, alipoipata tu, Jerry alimuita mpenzi wake Ame na kumuonesha.

“Dah, aisee tulikosea, jamaa hajafa,” Jerry alimwambia Ame, aliyepatwa na mshtuko usio kifani.

“Mungu wangu, sasa nitafanyaje jamani, maana tangu niwaambie ndugu zangu kuhusu kupotea kwake wala sijawaambia lolote na wala sijaonesha juhudi zozote za kuwatafuta. Na akipona huyu, jela inakuita,” Ame alimwambia mpenzi wake akimtazama usoni. Wote walionekana kuogopa sana suala hilo.

“Hapa lazima tuhakikishe hili jambo linamalizika haraka. Tumtumie Innocent kukamilisha hili zoezi, apewe sumu afe leo hii,” Jerry alimwambia Ame, aliyetingisha kichwa kukubaliana naye.

Wakakubaliana kumuita Innocent ili wamueleze nia yao, na ikibidi makubaliano mapya. Kijana huyo wa Muhimbili aliitika wito na kukubali kwenda hadi Bunju, alikokutana na wapenzi hao na kuzungumzia ishu hiyo. Haikuwa kazi rahisi kukubali, kwani kutoa uhai wa mtu ni hatia aliyoapa kutoitenda.

Hatimaye baada ya ahadi ya donge nono, Innocent alikubali kuifanya kazi hiyo yeye mwenyewe. Alitanguliziwa malipo ya awali ya fedha, kisha kazi ikaachwa kwake.

***

Noel baada ya kukubaliana na daktari wa wodi aliyolazwa Bata, aliomba msaada wa kupatiwa machela kwa ajili ya kumtoa nje. Wahudumu wasaidizi waliitwa na daktari, ambao walimbeba na kumshusha chini, ambako alilazwa kwenye siti za nyuma ya gari na Noel akaliondoa gari taratibu.

“Unanipeleka wapi kaka, mbona bado sijapona,” Bata alimuuliza Noel wakati gari likiondoka.

“Ninakuhamisha hospitali mdogo wangu, ukipata nafuu zaidi nitakuambia kwa nini nimekuondoa hapa mapema,” Noel alimweleza Bata kwa sauti iliyojaa urafiki, iliyomfanya kijana huyo kujisikia vyema, akakubali kwa kutingisha kichwa. Gari likaenda likikabiliana na foleni, hadi lilipofika katika zahanati moja, iliyo ndani ndani sehemu za Madale nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Kabla ya kumteremsha mgonjwa wake kwenye gari, akaenda kuzungumza na daktari ili kumweka sawa. Hawakuchukua muda mrefu, wakakubaliana kwamba kijana huyo alazwe hapo na asiruhusiwe mtu yeyote kumuona zaidi yake yeye na mzee Masta, aliyedai angekuja naye kesho yake.

***

Innocent alienda Muhimbili hadi chuoni, akachukua mavazi ya uanafunzi, akaenda zake hadi jengo lenye wodi ya Mwaisela. Daktari wa zamu alipomuona alimkaribisha, kwani wanafunzi wa hapo waliruhusiwa kuhudumia wagonjwa wakiwa na madaktari.

Alikaa kwa muda kama dakika tano hivi kwenye chumba cha madaktari, kisha akaomba kuwaangalia wagonjwa, akaruhusiwa. Alikwenda hadi kitanda cha mwisho lakini hakumuona mgonjwa aliyemtaka. Akarudia tena, safari hii akiwafunua wale waliojifunika na kulala, lakini hakumuona Bata.

Akatoa simu yake na kuiangalia picha ya mgonjwa wake, bila kujali, akamuonesha daktari na kumuulizia juu ya kijana huyo mgonjwa.

“Aisee, ndugu zake walikuja na kumchukua jana, wanasema huku ni mbali, wameona bora wamsogeze hospitali ya karibu,” daktari huyo alimwambia Innocent.

“Aisee, kumbe ndugu zake wamemchukua. Maana kuna mtu alinipa picha hiyo akaniambia ni ndugu yake niwe namtembelea hapa wodini,” Innocent aliongopa, uongo ambao daktari aliukubali bila kujua nia yake mbaya.

Aliendelea kuzugazuga mle wodini na muda mchache baadaye akaondoka akiwa amechanganyikiwa. Kumkosa Bata wodini kulimaanisha kupoteza pia mamilioni ya shilingi aliyoahidiwa. Aliposhuka chini, akampigia simu Jerry na kumwambia kilichotokea.

Jerry akashtuka sana kwa maelezo yale. Alifahamu hakuna ndugu yeyote wa Bata anayejua kuhusu alipo, kutoweka kwake kulimaanisha hatari kubwa mbele yao. Akamjulisha na mpenzi wake juu ya suala hilo, kitu kilichowafanya wote wawe wanyonge ghafla, wakakaa chini na kujiuliza juu ya hatua iliyofaa kuchukuliwa.

Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua katika toleo lijalo.

Leave A Reply