The House of Favourite Newspapers

Chongo!-11

0

Ilipoishia wiki iliyopita

Jerry akashtuka sana kwa maelezo yale. Alifahamu hakuna ndugu yeyote wa Bata anayejua kuhusu alipo, kutoweka kwake kulimaanisha hatari kubwa mbele yao. Akamjulisha na mpenzi wake juu ya suala hilo, kitu kilichowafanya wote wawe wanyonge ghafla, wakakaa chini na kujiuliza juu ya hatua inayofaa kuchukuliwa.

Endelea…

Tunafanyaje sasa Ame, kwa vyovyote Bata ameshazungumza kuhusu mimi na ameondolewa pale kulinda usalama wake, hii ni hatari ya wazi kwetu,” Jerry alimwambia mpenzi wake, aliyekuwa akitingisha kichwa kukubaliana naye.

“Sasa tunafanyaje, hili ni kosa lako maana hukuifanya kazi yako vizuri,” Ame alimwambia Jerry, aliyemjibu kwa kumkazia jicho lenye kuonya.

“Huu siyo wakati wa kulaumiana, kosa limeshafanyika na hapa suala ni kutafuta suluhisho tu,” Jerry alimwambia Ame na akajiinamia kutafakari nini cha kufanya.

Baadaye, Jerry akapata wazo, akamshauri mpenzi wake wakimbie nchi angalau kwa muda. Juu ya wapi wataelekea, mwanaume akapendekeza waende Afrika Kusini, kwani yeye kule aliwahi kuishi hivyo ingekuwa rahisi kidogo kwa upande wake.

Ame akakataa, akamwambia ni bora kama kuondoka aende Jerry, ila yeye hakuwa tayari kuondoka bila kuwa na uhakika ni wapi alipo ndugu yake. Kwamba anaweza kubakia na kukabiliana na hali yoyote itakayotokea wakati huo, lakini siyo kukimbia nje ya nchi.

Wakakubaliana Jerry akimbilie Afrika Kusini ili Ame abakie kusikilizia kinachoendelea. Wiki moja baadaye, baada ya kukamilisha kila kitu muhimu, kijana huyo alipanda ndege kuelekea bondeni, akiwa na hofu kubwa moyoni mwake.

**

Hali ya Bata iliendelea kutengemaa kila siku, huku akiwazoea Noel na mzee Masta kama ndugu zake wapya. Kila alipopata nafasi ya kukaa nao, aliwauliza maswali mengi ya jinsi walivyokutana, maana akilini mwake hakuwa na kumbukumbu ya nini kilimpata, na wapi hasa majeraha hayo aliyapata.

Mzee Masta na Noel hawakuwa na haraka, walitaka kujiridhisha kuwa mgonjwa wao alikuwa amepona kabisa, ndipo waweze kukaa naye na kuzungumza naye kwa kina, waweze kumtambua na kuona namna wanavyoweza kumsaidia. Baada ya wiki mbili, hali ya kijana huyo ilikuwa nzuri na aliruhusiwa kuondoka hospitalini akiwa amepona karibu majeraha yote.

Hata hivyo, majeraha aliyoyapata yalimwachia kilema cha maisha kwani jicho lake moja lilikuwa limeharibika kabisa na hivyo likaondolewa. Noel aliishi naye nyumbani kwake kama ndugu yake na majirani zake walimtambua kama ndugu yake aliyepata ajali.

Wiki sita baada ya kutoka hospitalini, Noel na mzee Masta walikuwa wamekaa na kijana huyo nje ya nyumba, wakizungumza maneno mawili matatu. Baadaye, kama alivyokuwa akifanya mara kwa mara, akaomba kuelezwa ni nini hasa kilitokea hadi yeye kuwa katika hali kama ile.

“Kwani wewe hukumbuki chochote katika maisha yako hadi sasa?” Noel alimwuliza Bata aliyetingisha kichwa kuonesha kutokumbuka chochote.

“Wewe ulikuwa unaishi wapi kabla ya kujikuta na hali kama hiyo, yaani ulikuwa unaishi Dar es Salaam, Arusha, Tanga au wapi?” Noel alimuuliza tena, huku mzee Masta akimtazama na kutabasamu.

Bata alikiweka kichwa chake katika miguu yake, akajaribu kuvuta kumbukumbu, akainua kichwa na kuonesha kama anayekumbuka kitu.

“Yes, nilikuwa nasoma mimi, kwani hapa ni wapi, mimi nilikuwa nasoma shule moja hivi Dar es Salaam, tena nilikuwa nakaa kwetu, mmmmh, wapi vileeeee,” Bata alionesha tabasabu na kuwafanya wale watu wawili aliokuwa nao, nao kuvaa tabasamu nyusoni mwao. Ilikuwa ni mara ya kwanza kwao kuanza kuona mwanga wa kijana huyo.

“Kwa hiyo wewe kwenu ni hapahapa Dar, ulikuwa unakaa na wazazi wako au kwa ndugu?” aliulizwa tena swali lingine, safari hii na mzee Masta.

Bata akajikuna kichwani, huku akichekacheka, ilikuwa ni jambo la kutia moyo kwamba alikuwa ameanza kurejewa na kumbukumbu zake taratibu. Akawatazama tena halafu akasema anakumbuka alikokuwa anakaa.

“Safi sana, hebu tuambie ulikuwa unakaa wapi? Noel alimwuliza Bata, ambaye hadi wakati huo walikuwa hawajui jina lake.

“Kwani hapa tulipo ni wapi?” Bata aliwauliza akionekana kuwa na hamu sana ya kujua!

“Hapa ni Tegeta Magereji,”

“Tegeta?”

JIUNGE NA GLOBAL BRAKING NEWS

GLOBALBREAKINGNEWS100.jpg

Leave A Reply