The House of Favourite Newspapers

Chongo!-24

0

UIipoishia wiki iliyopita
Kauli hiyo ilimtisha Mwani, akili yake ikamrudisha nyuma na kukumbuka jinsi siku ile Bata alivyomkazia macho yule dada kiasi kwamba akili yake ilionekana kama imepotea kwa muda. Akakumbuka pia jinsi alivyokuwa akifurahia alipokuwa akimzungumzia yule dada. Akaanza kupata woga!Sasa endelea…

Akilini mwake, akatambua kulikuwa na jambo la ziada kati ya Bata na kama siyo yule mwanamke, basi hata mwanaume. Yaani kwa vyovyote kuna jambo lisilo la kawaida baina yao. Hata hivyo, alijikuta akipata woga na kuhisi hatari katika dhamira ya Bata.

“Bata, now I can understand (Bata, sasa naweza kukuelewa). Sikia, ili nikupe msaada unaotaka ni vizuri ukanieleza wazi hasa kitu gani kipo katika akili yako. Hii ni kwa sababu nakumbuka siku ile tulipokuwa kule kijiweni, ulionekana kumtazama sana yule dada Al Shababu na sasa ninapata picha kwamba kuna kitu,” Mwani alimwambia Bata.

Bata naye akavuta kumbukumbu, akakumbuka jinsi alivyopoteza uwezo wake wa kiakili kwa muda mfupi wakati yule dada alipokuwa akitoka ndani ya nyumba na kuingia kwenye teksi na akaendelea kukumbuka jinsi Mwani alivyomshtua baada ya kumuona amezamia katika kumtazama!
“Yes Mwani, nina tatizo kubwa ni ukweli mchungu kwangu, naogopa ukifahamu siri iliyopo utakosa raha maana ni hatari, naomba tu uridhike kuwa unamsaidia mtu mwenye kuhitaji msaada. Tafadhali,” Bata alimsihi Mwani.

“No, siwezi Bata. Hivi unanichukulia kirahisi namna hiyo? Yaani nikupe msaada wa kuingia nyumba ya watu bila kujua nia yako, ukiwaua? Unataka nipate dhambi? Labda nikuambie kitu, ninao uwezo wa kukuingiza mle ndani, hata bila wenyewe kujua ukitaka, lakini lazima uniambie ukweli,” Mwani alimwambia.

Mapigo ya moyo wa Bata yakasimama kwa sekunde kadhaa baada ya kusikia kuwa msichana huyo angeweza kumwingiza ndani ya nyumba ile bila wenyewe kujua. Hili ndilo hasa alilolitaka. Lakini kumwambia ukweli, lilikuwa ni tatizo kubwa kwake, hasa akikumbuka kuwa alishakubaliana na wenzake juu ya kutosema.

Akamwita Elina ili ampatie maji ya kunywa baridi, maana kiu ilimkamata ghafla. Mwani naye akaagiza maji. Ilimchukua Bata kama dakika tano nzima akiwa mwenye mawazo mengi ndipo alipoinua kichwa kumtazama machoni Mwani.
“Nitakueleza, lakini tafadhali ibakie kuwa siri yako milele yote,” Bata alimwambia Mwani na kuanza kumsimulia kila kitu alichokijua juu ya watu wale alioamini ndiyo walewale waliotaka kutoa uhai wake, miaka kadhaa iliyopita.
***
Sule alikuwa amekaa kwenye kona, katika sehemu ya baa ya hoteli ya Johannesburg, akiburudika kwa bia, macho yake yakicheza na kila mtu aliyeingia mlangoni. Macho yake yalikuwa yanataka kukutana na mtu mmoja tu, Twaha.

Huyu ni yule mshkaji ambaye siku chache nyuma, katika hoteli hiyohiyo, aliwaeleza marafiki akiwemo Jerry, juu ya mtu aliyefanyiwa ubaya, ambaye sasa anawatafuta wabaya wake ili kulipa kisasi.
Jerry alimpatia Sule namba ya simu ya Twaha, ili apate muda wa kumdadisi na ikiwezekana, amuongoze kumuona Bata, wapate kumfanyia tathmini. Hata hivyo, wawili hao hawakuwa wakifahamiana, ingawa Sule alipewa picha ya Twaha na Jerry.
Kwa asili ya kazi yake ya uaskari, sura ya Twaha angeitambua mara tu angeingia mlangoni, hata kama atakuwa amejitahidi kubadilika kwa kiwango gani. Sule akatoa simu yake na kubonyeza namba za Twaha kumfahamisha kuwa alishafika sehemu ya ahadi.
“Nipo njiani kaka,” Twaha alimjibu Sule, aliyerudisha simu mezani na kuendelea na kinywaji chake taratibu. Dakika kumi baadaye Twaha alifika hotelini hapo, lakini tofauti na Sule alivyotegemea, hakuweza kumtambua hadi alipoona simu yake ikiita na kugundua kuwa, kijana aliyekaa meza ya pili kutoka pale alipo, ndiye aliyekuwa akimsubiri.

Ni wewe Twaha?” Sule alimuuliza alipoona jina lake linatokea katika simu yake.
“Yes, Sule siyo?” Naye alijibu huku akiuliza na walipokubaliana, wakasogea katika meza aliyokaa Sule na kushikana mikono kusalimiana.
***
Kwenye mwavuli mmoja ndani ya Ukumbi wa Dar Live, siku ile ya Jumapili, Bata, Jully, Elina na Mwani walikuwa wamekaa kila mmoja akinywa kinywaji baridi, wakionekana kama vijana wengine waliokuja kujirusha, katika siku hii ambako kulikuwa na michezo na burudani mbalimbali.
Walikuwa wanasubiri oda yao ya nyama ya Mbuzi upande mzima waliyoagiza baada ya mabishano mengi kama wangeweza kumaliza au la.
“Sasa dada Mwani tukusikilize ili utueleze jinsi gani huu mchezo unavyoweza kufanyika na kutuwezesha kufikia malengo bila kuacha alama nyuma yetu,” Bata alianzisha mazungumzo huku wasichana hao watatu wakionekana kuwa tayari kwa lolote.
Je, nini kitaendelea? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua katika toleo lijalo.

Leave A Reply