The House of Favourite Newspapers

Chuo Kikuu Cha Kimataifa Kampala Kimeanza Upya Kwa Nguvu Mpya

“KUTELEZA sio kuanguka,” ni msemo tunaoutumia pale tunapokatishwa kabisa tamaa ya kusonga mbele, msemo huu unatupa faraja ya kusimama tena.

Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala nchini Tanzania (KIUT) ni miongoni mwa vyuo vikuu vilivyoufanyia kazi msemo huo baada ya kufungiwa udahili na TCU.

 

Kifungo cha chuo hicho kimekoma mwaka huu baada ya kukamilisha taratibu zote zinazohitajika na TCU.

Ni vyuo vichache vyenye uthubutu wa kuweza kusimama tena na kutumia adhabu ya kifungo kama funzo na kusonga mbele zaidi, hali hii inakifanya Chuo cha KIUT kuwa cha kipekee hapa nchini.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala nchini Tanzania (KIUT), Prof. Jamidu Katima.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu KIUT, Prof. Jamidu Katima anatupitisha kwa ufupi katika safari yao iliyokuwa na miba, milima na mabonde na jua kali mpaka hapa leo walipofikia sambamba na mipango ya chuo hicho kwa kusema yafuatayo:

“Nianze kwa kusema sababu za kufungiwa udahili

chuo chetu. Kilifungiwa udahili kwa kuwa na wafanyakazi ambao hawakuwa na vibali vya kufanyia kazi, kosa ambalo uongozi wa chuo ulifanya ukidhani kuwa mtu anaweza kuja nchini na kufanya mchakato wa kupata vibali husika.

 

“Sababu nyingine ni kwa baadhi ya wafanyakazi kukosa sifa. Kukosa sifa kuna maana tofauti, kutokana na mwongozo wa TCU, unasema ili mtu aweze kufundisha chuo kikuu, kwa ngazi ya shahada ya kwanza lazima awe ana ufaulu wa (GPA) 3.5, na kwa shahada ya uzamili awe na ufaulu wa (GPA) 4.0.

 

Wafanyakazi wengi waliokuwepo walikuwa wamekidhi vigezo kwa ngazi ya shahada ya uzamili yaani walikuwa wana GPA ya 4.0 na wengine walikuwa na shahada ya uzamivu lakini hawakuwa na sifa kwa ngazi ya shahada ya kwanza, kwa maana walikuwa chini ya GPA 3.5.

 

“Hivyo kwa kufuata mwongozo wa TCU hawakukidhi vigezo. Kwa kuwa KIUT kilikuwa Chuo Kikuu Kishiriki cha Chuo Kikuu Kampala nchini Uganda, walikuwepo wanafunzi wa shahada za uzamili na uzamivu. Hawa walikuwa na visa ya uanafunzi.

“Kwa taratibu za vyuo vyote ulimwenguni, wanafunzi hawa wanapaswa kusaidia kwenye kufundisha kwa mfano, kusimamia tutorials, elimu kwa vitendo nk. Hii inatoa mwanya wa kuwajengea uwezo wanafunzi hawa. Hivyo kosa jingine KIUT ilituhumiwa kutumia wanafunzi hawa kufundisha.

 

“Ili uweze kuendesha kozi inayotambulikana TCU ni lazima uwe na si chini ya walimu watano (5) wenye taaluma ya kozi unayofundisha (core staff), pungufu ya hapo utafungiwa.

“Kutokana na sababu hizo hapo juu tukajikuta katika kozi zetu kadhaa zina upungufu wa walimu kuanzia mmoja, wawili au watatu, hivyo kukosa sifa.

ATHARI ZA KUFUNGIWA UDAHILI

“Athari kubwa ni kusimama kwa shughuli za uendeshaji wa chuo. Mfano; tumekuwa tukijenga jengo la hospitali ya mafunzo kwa wanafunzi wa afya, lenye uwezo wa vitanda zaidi ya mia nane (800), imebidi lisimamishwe.

“Athari kwa muwekezaji, alipaswa kuendelea kulipa mshahara wa wafanyakazi kutoka kwenye vyanzo vyake vingine, vilevile mwekezaji alipaswa kuwalipa wafanyakazi kwa makubaliano ili KIUT

 

iweze kukatiza mikataba ya wafanyakazi walioachishwa kazi.

“Athari hasi kwa wafanyakazi wote ambao waliguswa na kasoro zilizoainishwa hapo juu waliachishwa kazi.

 

HATUA ZILIZOCHUKULIWA NA CHUO

“Moja ya jitihada zilizofanyika ni kuzisimamisha kozi zote zenye idadi ndogo ya wanafunzi na kuongeza nguvu kwenye program zenye wanafunzi wengi na walimu wachache.

“Tuliondoa baadhi ya wafanyakazi ambao hawakuwa na sifa na kuajiriwa katika maeneo muhimu na yale yenye upungufu.

“Pia tulibadili muundo wa chuo ambapo tulipunguza vitivo na idara zake. Tuliweza kupunguza vitivo kutoka saba (7) mpaka vitatu (3) na idara kutoka 21 mpaka 10.

“Mwitikio baada ya kufunguliwa

kwa kuangalia idadi ya wanafunzi wanaofanya maombi ili kujiunga na chuo mwaka wa masomo 2019/20 kwa kweli inatia moyo sana ukizingatia ni program takriban saba zilizofunguliwa ambazo zina maombi ya wanafunzi wapatao 800.

 

TASWIRA MPYA INAYOJENGWA NA KIUT

“Kikubwa ni kutaka kukikuza chuo katika nyanja ya utoaji elimu hii ni sambamba na kutafiti soko la programu zetu na zile ambazo tungependa kuwanazo mfano; program za uhandisi.

“Pili, kukamilika kwa jengo la hospitali kutawapunguzia adha wananchi wanaoutuzunguka ili wapate huduma za afya karibu yao badala ya kusafiri umbali mrefu kwenda hospitali za Amana,Temeke au Muhimbili.

“Tatu, chuo tayari kina mikataba ya awali ya kushirikiana na hospitali za mataifa ya nje ili kuwa na ushirikiano wa kutoa huduma kwa wagonjwa hapa nchini katika tiba zinazohitaji madaktari bingwa na waliobobea.

 

FAHARI YA CHUO KIUT

“Tunachojivunia sisi ni kuwa na mchanganyiko wa walimu wazawa na walimu kutoka nchi mbalimbali.

“Hali hii inawafanya wanafunzi kuweza kujifunza uzoefu kutoka mataifa tofauti wanakotoka walimu wa kigeni kutoka nchi kama Cuba, Kenya, India, Ireland, Nigeria na Uganda.

“Pia tunajivunia kuwa na viongozi na wasomi wa aina mbalimbali waliopo Serikalini waliotoka chuoni kwetu.

“KIUT iko kwenye mpango wa kuwatumia hawa viongozi kama mabalozi wetu.

 

Ujumbe:

“Tunakiri kuwa tulifanya makosa na tumeyarekebisha na tuko tayari kuanza upya, hatutaki kurudia tena makosa yaleyale, tunaomba wazazi na wanafunzi watuamini,” anaeleza Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala nchini Tanzania (KIUT), Prof. Jamidu Katima.

MAWASILIANO

Gongo la Mboto, Dar es Salaam, Tanzania
Week Days: 08:00am – 05:00pm

P. O. Box 9790, Dar es Salaam, Tanzania

Admissions: [email protected], 0689 504 923

Website: www.kiut.ac.tz

Comments are closed.