The House of Favourite Newspapers

Coca-Cola Kwanza Yadhamini Matembezi Ya Hisani

Kampuni ya vinywaji baridi ya Coca-Cola Kwanza inadhamini kwa mara ya nne mfululizo matembezi ya kilomita 5 yenye lengo la kukusanya zaidi ya Tsh 100m kuwasaidia kina mama wenye saratani ya matiti nchini Tanzania. Matembezi hayo yatafanyika Jumatatu 14/10/2019 katika viwanja vya The Green (zamani uwanja wa Farasi).

 

Fedha nyingine itatumika kuelimisha vijana mashuleni na kusaidia ujenzi wa hosteli ambayo itakuwa inatumiwa na akina mama wanaokuja jijini Dar es Salaam kufuatilia matibabu. Matembezi hayo vile vile yatajumuisha mbio za kilomita 9.

 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam 9/10/2019 meneja masoko na biashara wa Coca-Cola Kwanza Wahida Mbaraka amesema kampuni yake inaona fahari kutumia sehemu ya faida yake kudhamini matembezi hayo ya hisani kusaidia kuboresha maisha ya akina mama nchini.

Mashindano hayo ambayo yanaandaliwa na asasi ya saratani Tanzania (TBCF) yanatarajia kuwaleta pamoja washiriki zaidi ya elfu mbili mia tano na mgeni rasmi atakuwa John Ulanga, Mkurugenzi Mkazi wa chapa ya Afrika Mashariki.

 

’Siku hizi saratani ya matiti siyo tishio kwa wanawake peke yake bali hata kwa wanaume vile vile. Napenda kuchukua nafasi hii kuwaomba wanaume kujitokeza kupima ili kuona kama wana dalili za saratani ya matiti au la”, alisema Mbaraka.

 

Akizungumza katika mkutano huo, mratibu wa programu wa TBCF Kisa Mwakatobe amesema watatumia matembezi hayo ya hisani mbali na mazoezi ya mwili pia yatatoa elimu jamii kuhusu saratani ya matiti na haki zinazohusiana na matibabu na maisha kwa ujumla.

 

Amesisitiza umuhimu wa kupima afya mara kwa mara kwani ugonjwa huo ukigundulika katika hatua za awali unaweza kutibiwa kirahisi.

Comments are closed.