The House of Favourite Newspapers

Corona Yaongeza Simanzi Mazishi ya Mama Rwakatare

0

 

 

DAR: Licha ya kuwa ni desturi ya Waafrika na Watanzania kushiriki mazishi ya ndugu, jamaa, marafiki na wapendwa wao, hali hiyo imekuwa tofauti kwa Mchungaji wa Kanisa la Mikocheni B Assemblies of God ‘Mlima wa Moto’, Dk Getrude Rwakatare ‘Mama Rwakatare’, ambaye amezikwa juzi.

 

Mama Rwakatare ambaye pia alikuwa Mbunge wa Viti Maalum (CCM), amezikwa katika eneo la kanisa lake lililopo Mikocheni B jijini Dar na idadi ya watu 10 tu.

 

Hali hiyo imeibua na kuongeza simanzi mara mbili kwa ndugu wa familia yake, wabunge, viongozi wa serikali, waumini na Watanzania kwa jumla hasa ikizingatiwa Mama Rwakatare mbali ya kuwa mtumishi wa Mungu pia alijitoa kwa wananchi wa kada zote kwa kuwasaidia na kugusa maisha yao kwa namna mbalimbali.

 

Simanzi hiyo inatokana na ukweli kwamba mazishi yake yalitarajiwa kuhudhuriwa na maelfu ya waombolezaji kama ilivyokuwa kwa misiba mingine kama wa aliyekuwa Mwenyekiti wa IPP, Dk Reginald Mengi, lakini kutokana na janga la maambukizi ya Corona, Serikali ilitoa maagizo ya watu wasiozidi 10 kushiriki mazishi hayo.

 

Kifo chake ambacho familia yake ilieleza kilisababisha na matatizo ya moyo, kimeacha gumzo kwa Watanzania na kuweka historia ya kuwa kiongozi, tajiri na mtu mashuhuri wa kwanza nchini kuzikwa katika mazingira ya aina hiyo.

KISA CORONA

Aprili 21, mwaka huu Spika wa Bunge, Job Ndugai alitoa taarifa bungeni kuwa mazishi ya mbunge huyo wa Mvomero, Morogoro yatasimamiwa na Serikali.

Spika Ndugai alisema watu wachache watashiriki katika mazishi ya mbunge huyo kutoka mkoani Morogoro, kutokana na wakati wa sasa kukumbwa na Ugonjwa COVID-19.

 

Alisema suala la kumleta marehemu bungeni kalingana na mazingira ya sasa, haitawezekana.

“Haitawezekana kuaga bungeni na kumpeleka katika nyumba ya milele, mazingira ya sasa hayaruhusu kumleta hapa, maelezo mengine tutapata kesho (jana) baada ya kuzungumza na familia na Bunge,” alisema.

 

Alisema Bunge linajali maisha ya wabunge wake na litaendelea kuchukua hatua zinazowezekana kumsaidia katika kuhakikisha anapewa msaada kila anapohitaji.

 

Majibu hayo ya Ndugai yalisawazisha giza lililokuwa limetanda kuhusu mazishi ya mchungaji huyo hasa ikizingatiwa baadhi ya wabunge akiwamo Mbunge wa Kigoma- Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) ambaye aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuhoji shughuli za kuaga mwili wa marehemu kutofanyika bungeni kama ilivyo taratibu za mbunge akifariki dunia.

 

WAUMINI WAMLILIA

Licha ya kwamba asilimia kubwa ya waumini hawakuruhusiwa kushiriki mazishi hayo, baadhi yao walieleza simanzi waliyokuwa nayo dhidi ya kiongozi wao ambaye amewatoka.

“Hili ni jambo ambalo limetuuma sana, kutomuaga wala kushiriki mazishi yake kwa kweli limetuongezea uchungu ambao hauelezeki.

 

“Kwa sababu sio desturi yetu mtu akifariki dunia hata kama ndugu wapo nje ya nchi wanamsubiri aje kushiriki mazishi, lakini kwa kiongozi wetu imeshindikana ndiyo maana tunaelekeza sala zetu sasa kupambana na hili janga la Corona,” alisema muumini mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Aghata.

 

Simanzi hiyo ilielezewa na muumini mwingine ambaye alilieleza IJUMAA kuwa; “Kumzika mtu ni suala la msingi, lakini kwa mtu maarufu kama Mama Rwakatare ilitarajiwa wachungaji, watu serikalini kushiriki, lakini sasa imeshindikana. Hatuwezi kumlaumu mtu kwa sababu ndiyo hali halisi inabidi tu kuchukua tahadhari kujikinga na ugonjwa huu.”

 

WASIFU WA MAREHEMU

Mchungaji Rwakatare ambaye pia alikuwa mmiliki wa Shule za Kimataifa za St Mary’s, aliaga dunia Aprili 20 katika Hospitali ya Rabinisia, Tegeta jijini Dar alipokuwa amelazwa baada ya kuugua ghafla.

 

Alizaliwa Desemba 31, 1950 na kupewa jina la Getrude Pangalile. Alipofikisha umri wa kuanza shule, alijiunga na Shule ya Msingi Ifakara. Alipohitimu elimu ya msingi, alijiunga na Shule ya Sekondari ya Korogwe alikosoma kidato cha kwanza hadi kidato cha sita.

 

Baadaye, alikwenda nje ya nchi kusoma na kujiunga na Chuo cha North London Polytechnic, alikosomea kozi ya uongozi kwa ngazi ya stashahada. Baadaye aliendelea na masomo, akajiunga na Chuo cha Eastern and Southern Africa Management Institute alikopata Shahada ya Mawasiliano ya Umma (Bachelor Degree in Mass Communication).

 

Safari yake ya kitaaluma haikuishia hapo, alisafiri mpaka Chicago, Illinois nchini Marekani alikokwenda kujiunga na Chuo Kikuu cha Kikristo cha Moody ambako huko ndiko msingi wake wa mambo ya kichungaji ulipojengeka na kumfanya kuwa Mama Rwakatare ambaye leo tunamjua.

 

Safari ya kielimu, iliendelea na kumfanya kuzidi kupanda ngazi moja ya kitaaluma hadi nyingine, hadi kufikia hatua ya udaktari wa falsafa (Philosophy Doctorate- PhD) na kulifanya jina lake sasa libadilike na kuwa Dokta Getrude Pangalile.

Pengine utajiuliza jina la Rwakatare limetoka wapi wakati alizaliwa akiwa anaitwa Getrude Pangalile? Jina hilo lilitoka kwa mumewe, Kennedy Rwakatare. Walipooana, ndipo jina lake likabadilika na kuwa Getrude Pangalile Rwakatare. Kwa bahati mbaya, mumewe huyo alifariki dunia mwezi Machi, 2013 huko Bukoba mkoani Kagera.

 

AJIRA SERIKALINI

Ajira ya kwanza ya Mama Rwakatare aliporejea nchini, ilikuwa ni katika Mamlaka ya Bandari ya Afrika Mashariki (East Africa Harbours Authority) ambako aliajiriwa kuanzia mwaka 1984 na kuendelea na kazi hiyo hadi alipoamua kujiajiri mwenyewe kwenye ajira binafsi na kuanzisha shule ya kwanza ya St Mary’s, miongoni mwa shule za mwanzo kabisa nchini kufundisha kwa kutumia mtaala wa Kingereza (English Medium), akiwa ndiyo mkurugenzi wake.

 

UTUMISHI WA MUNGU

Mama Rwakatare pia alikuwa mtumishi wa Mungu ambapo mwaka 1995 alianzisha Kanisa la Mikocheni B Assemblies of God au maarufu kama Mlima wa Moto ambayo ni miongoni mwa makanisa makubwa nchini kwa sasa.

KATIKA SIASA

Katika siasa, nyota ya Mama Rwakatare ilianza kung’ara mwaka 2007 alipoteuliwa na Rais wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Kikwete kuwa mbunge wa kuteuliwa kwa tiketi ya CCM na aliendelea kuwa mbunge mpaka mwaka 2015 Kikwete alipomaliza muda wake.

Aprili, 2017 aliteuliwa tena kuwa mbunge wa viti maalum baada ya Mbunge Sofia Simba kuvuliwa uanachama wa CCM na nafasi yake kubaki wazi.

Tangu hapo ameendelea kuwa mbunge wa viti maalum katika utawala wa Rais Dk. Magufuli.

 

HUDUMA KWA JAMII

Licha ya mafanikio makubwa aliyoyapata kwenye dini, siasa na miradi binafsi, Mama Rwakatare alikuwa si mchoyo wa fadhila! Kwa kipindi kirefu amekuwa mstari wa mbele kwa kuisaidia jamii, mwaka 2007 alianzisha kituo cha Watoto Yatima cha Bright Future ambacho mpaka leo kimekuwa kikiwasaidia watoto yatima na wale wanaoishi kwenye mazingira magumu.

 

Mama Rwakatare ameacha watoto wanne; Rose Rwakatare, Tibe Rwakatare, Mutta Rwakatare na Humphrey Rwakatare.

Stori: GABRIEL MUNSHI, Ijumaa

Leave A Reply