The House of Favourite Newspapers

CRDB Yakabidhi Zawadi Washindi wa Simbanking

0
Pichani ni Adam Salehe Rashid mshindi wa bajaji akionyesha funguo baada ya kukabidhiwa zawadi hiyo na  Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya CRDB, Stephen Adili (wa pili kulia). Adam ameshinda bajaji hiyo katika droo ya kwanza ya kampeni ya Benki ni Simbanking inayoendeshwa na Benki ya CRDB. Katika droo hiyo, Kibwana Hussein Killongo na Rahma Abdul Kyalumbika wameshinda pikipiki kila mmoja.  Zawadi hizo zilikabidhiwa katika eneo la Chanika jijini Dar es
Salaam. (Na Mpigapicha Wetu)
WATEJA watatu wa Benki ya CRDB leo wamekabidhiwa zawadi zao baada ya kuibuka washindi kutokana na kufanya miamala mingi ya huduma za benki kupitia simu zao za mkononi maarufu kama Simbanking.
Akikabidhi zawadi hizo jijini hapa, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa Benki ya CRDB, Stephen Adili amesema huu ni mwanzo tu kwa wateja wa benki hii kujinyakulia zawadi katika promosheni ya mwaka mzima ya Benki ni Simbanking yenye kaulimbiu ya Swahiba – lako, langu.
Adili amesema teknolojia imerahisisha mambo mengi hivi sasa kwa kuwawezesha wateja kupata huduma kupitia majukwaa tofauti zikiwamo simu za mkononi ambazo kwa Benki ya CRDB wanayo Programu ya Simbaking inayowaruhusu kupata zaidi ya asilimia 95 ya huduma zake mahali popote walipo.
“Simbanking imedumu sokoni kwa zaidi ya miaka 15 sasa, ni njia rahisi ya kupata huduma za Benki ya CRDB na kwa sasa tunayo kampeni ya kuwahamasisha wateja wetu na wananchi kwa ujumla kuitumia na wale wanaoitumia zaidi tunawapa zawadi za aina tofauti. Leo tupo hapa Chanika kukabidhi bajaji moja na pikipiki kwa washindi wetu waliopatikana katika droo ya kwanza ya kila mwezi,” amesema Adili.
Waliokabidhiwa zawadi hizo ni Adam Salehe Rashid aliyejishindia bajaji pamoja na Kibwana Hussein Killongo na Rahma Abdul Kyalumbika walioshinda pikipiki kila mmoja. Kukabidhiwa kwa zawadi hizo kunawakumbusha wateja wengine wa Benki ya CRDB kuendelea kutumia Simbanking hali itakayowaweka kwenye nafasi ya kushinda pikipiki au bajaji nyingine zitakazokuwa zinatolewa kila mwezi au Toyota Dualis itakayoshindaniwa kila baada ya miezi mitatu.
“Washindi hawa watatu wa kwanza wamefungua pazia kwa mwaka huu. Naomba mfahamu kwamba kuna magari manne aina ya Toyota Dualis yanayoendelea kushindaniwa hivyo nawasihi wateja wetu na Watanzania ambao hawatumii huduma zetu basi wafungue akaunti kwani kwa kufanya hivyo tu watakuwa wanaingia kwenye droo ya kushinda moja kati ya zawadi nyingi tulizonazo,” amesema Adili.
Ili kushinda moja ya zawadi zinazotolewa na Benki ya CRDB, mteja anatakiwa kufanya miamala mingi kupitia Simbanking kama vile kulipia bili za umeme na maji,  kukata tiketi ya usafiri wa ndege, kulipa ada na michango ya shule, kulipia bidhaa zinazouzwa mtandaoni au kununua muda wa maongezi na huduma nyingine nyingi zinazopatikana ndani ya Programu ya Simbanking.
“Sifa zilizowapa ushindi wateja hawa watatu zinawezekana kwa mteja mwingine yeyote wa Benki ya CRDB hivyo niwahimize wateja wetu wote kutoka mahali popote walipo kuendelea kutumia huduma za Simbanking ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kushinda zawadi kemkem tulizonazo,” amesema mkuu huyo.
Akipokea pikipiki yake, Rahma amesema ataifanya bodaboda ili imwingizie kipato. “Naamini haitonifaidisha peke yangu. Dereva
atakayekuwa anaiendesha naye atapata kitu cha kuisaidia familia yake. Nimefurahi kushinda na naipenda zaidi Benki ya CRDB kwani inarudisha sehemu ya faida yake kwetu,” amesema.
Leave A Reply