The House of Favourite Newspapers

CRDB Yapiga Jeki Chuo Cha Polisi Moshi

Zoezi la kukabidhi hundi ya Mil.10 likifanyika.

 

Kufuatia changamoto kubwa ya uchakavu wa vyoo vya wanafunzi wa kike katika chuo cha polisi Moshi ambayo imekuwa ikihatarisha afya ya wanafunzi hao wawepo chuoni hapo benki ya CRDB imetoa kiasi cha shilingi milioni kumi kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa vyoo vya chuo ili kuwapunguzia adha hiyo wanafunzi wa kike.

 

 

Msada huo unakuja wakati mwafaka kutokana na chuo hicho kuwa na majengo ya muda mrefu ambapo akikabidhi msaada huo Mkurugenzi wa ununuzi na Ugavi wa Benki ya CRDB, Pendason Philemon amesema msaada huo ni moja ya sera  maalum iliyojiwekea benki hiyo ya kusaidia jamii yenye kuagiza na kuelekeza kutenga asilimia moja ya faida yake kila mwaka.

“Dhamira hii ya kusaidia jamii kunaifanya benki ya CRDB kuendelea kuwa mdau wa maendeleo kwa kuchangia kwa kiasi kikubwa jamii inayotuzunguka pamoja na kusaidia serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika jitihada zake za kupeleka huduma za kijamii zenye kukidhi mahitaji ya wananchi hususani katika kuliunga mkono jeshi la polisi katika jitihada zake za kulinda wananchi na mali zao.”alisema Philemon.

 

Alisema benki ya CRDB inafahamu fika kuwa vyoo ni afya na usafi katika maisha ya binadamu yoyote yule duniani hivyo basi waliposikia chuo cha polisi kina uhitaji wa ujenzi na maboresho ya vyoo vya wanawake hawakusita kama benki kuunga mkono ombi hilo ili kuwezesha ujenzi huo.

 

Awali Gemini Mushy Kaimu Mkuu wa Chuo cha Polisi Moshi amesema msada huo uliotolewa na Benki ya CRDB ni muhimu kwa kuwajengea Askari polisi mindombinu bora ambapo licha ya kutumia bajeti ya serikali bado wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya uchakavu wa miundombinu chuoni hapo kufuatia majengo hayo kuwa ya muda mrefu.

 

Ni ombi letu pia katika mipango yenu kuzidi kuangalia mtakavyoweza kutia shime ili kuboresha mazingira ya kuwafundishia askari wetu ili watokao hapa wawe na ari kubwa zaidi ya kuwalinda raia na mali zao kwa ufanisi zaidi ili pato binafsi la mtanzania liweze kukua zaidi na utashi wa kuwekeza kupitia CRDB uweze kukua sawia”Alisema SACP Mushy.

 

Kwa upande wake Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Kaskazini bi Chiku Issa alisema CRDB iliguswa na hali mbaya ya vyoo vya wanachuo wa kike hivyo kuamua kuasaidia kutatua changamoto hiyo.

 

“Mimi kama mama kwa kweli nilipofika hapa baada ya kupokea maombi  niliguswa na kwa kutambua kauli mbiu ya choo ni nyumba  niliona ipo haja ya kuwasaidia askari wetu ambao ndio walinzi wa mali zetu na raia”.

 

Naye mlezi wa wanafunzi wa kike na Mkufunzi katika shule ya polisi Tanzania Mrakibu Mwandamizi waJeshi la Polisi, Pili Misungwi ameshukuru benki hiyo kwa msaada huo ambao amesema wanaishukuru benki hiyo kwa wepesi na uharaka wa nanma walivyolishughulikia suala hilo ambalo lilikuwa ni changamoto kubwa kwa wanafunzi askari wa kike.

 

“Tulihusisha wadau mbali mbali lakini mmoja wa wadau waliojitokeza kwa haraka na kuamua kutusaidia ni  CRDB kwa kweli kwa niaba ya mkuu wa Jeshi la Polisi nchini na Mkuu wa Chuo tunaishukuru sana CRDB kwa kutambua umuhumu wa kusaidia askari wanafuniz wa kike kwa sababu maumbile ya kike na kiume ni tofauti kwa kuwa watoto wa kike ni rahisi sana kupatwa na magonjwa endapo mindombinu haitakuwa misafi”alisema SSP Misungwi.

Comments are closed.