The House of Favourite Newspapers

Mo Dewji Asimulia “Niliwaambia Watekaji Waniue” – Video

BILIONEA kijana Afrika na mmiliki wa mojawapo ya klabu maarufu ya soka Afrika mashariki Simba SC – Mohammed Dewji amezungumza kwa mara ya kwanza kuhusu sakata lake la kutekwa nyara mwaka jana na namna alivyotishiwa maisha yake nchini Tanzania.

 

Katika mahojiano maalum na ya kipekee na BBC Swahili, Mo ameeleza kuwa kwa kipindi kizima, alihisi kwamba kuna uwezekano mkubwa hatoweza kutoka salama na kuwa mwisho wake wa maisha unakaribia.

 

“Saa 24 za kwanza baada ya kutekwa zilikuwa kama mwezi. Imani ndio kitu kikubwa kilichonisaidia katika kipindi kizima.”

Katika kuikumbuka siku hiyo, Mo ameeleza: “Walinifunga macho, miguu na mikono kwa siku tisa. Tulikuwa hatuongei sana, walikuwa sio watu wa hapa.

 

“Walikuwa wakinitisha na kuniweka bastola kwenye kichwa na kuniambia wataniua.” ameeleza mfanyabiashara huyo.

Mwaka jana mwezi Oktoba, Dewji alitekwa na watu wasiojulikana mjini Dar es Salaam. “Kufunga mlango (wa gari) tu, kugeuka nimekuta watu wanne ambao wamevaa mask nyeupe – wamefunika uso, wakapiga bunduki juu mara mbili halafu wameniwekea bunduki.”

 

Anasema awali alidhani ni jaribio la kutaka kuibiwa gari, na hakuwa na budi kufuata maagizo alipoambiwa alale chini kwenye sakafu. “Kwenye sekunde sitini hivi, hao watu wamekuja wamenibeba na kuniweka ndani ya gari.”

 

Anasema kilichofuata katika safari hiyo anayosema iliyokuwa ngumu, watekaji wake walimvua nguo kwa kuhofia huenda ana kifaa cha kutambua anakokwenda yaani tracker na kumfunga mikono na miguu na kwenye dakika 20 wakamfikisha katika nyumba.

 

“Niligundua kuwa lugha wanayotumia sio lugha ya Tanzania, ilikuwa ni geni. Asubuhi walikuwa wananifungua mikono wananifunga mbele, lakini usiku ndio kulikuwa na mitihani walikuwa wananifunga nyuma. Na wakikufunga nyuma maanake huwezi kulala, lazima ulale kulia au kushoto.”

 

Mo anasema alikuwa akitoa ushirikiano kwa kila alichotakiwa kufanya. Kikubwa anasema alikuwa akimuomba Mungu atoke salama. Siku ya tisa anasema “walinisukuma pale Gymkhana na nikasikia gari limeondoka.”

 

Kwa muda wote alipewa tu kipande cha khanga aliyotumia kujifinika mpaka siku walipomuachilia ndiyo aliyotumia pia kujifunika.

 

Mo Dewji alitekwa Oktoba 11 2018 na watu wasiojulikana alfajiri wakati alipokuwa akielekea mazoezini alipofika katika hoteli moja ya kifahari katika eneo la Oysterbay jijini Dar es Salaam kama ilivyo ada yake kila siku alfajiri kwa ajili ya kufanya mazoezi ya viungo.

 

Siku tisa baadaye, Dewji alirejea nyumbani salama. Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Dar es salaam Lazaro Mombasasa aliyemtembelea Dewji kuthibitisha kurejea kwake nyumbani, alisema watu waliomkamata walikuwa na lafudhi ya mojawapo ya lugha za mataifa ya Kusini mwa Afrika.

 

Maswali ambayo hadi leo yamesalia kufuatia mkasa wa kutekwa kwake MO ni: Kwanini ametekwa? Nani aliyemteka? Kwanini hakuwa na mlinzi? Washukiwa kadhaa wamekamatwa, na baadhi yao kuachiwa baada ya kuridhishwa na upelelezi wa maafisa wa usalama.

 

Aliyekamatwa hivi karibuni ni dereva wa teksi Mousa Twaleb aliyefikishwa mahakamani nchini akihusishwa na utekaji wa mfanyabiashara huyo maarufu.

 

Mkuu wa polisi wa Dar es Salaam, kamanda Lazaro Mambosasa alieleza kwamba bwana huyo ambaye pia ni dalali wa nyumba ndiye ‘aliyewakaribisha mjini watekaji wa Mo na kuwapangisha nyumba ambayo alidai kuwa waliitumia kumficha Mo baada ya kumteka’.

 

Kuhusu uchunguzi ulipofikia, Mo amesema kwamba hafuatilii sana uchunguzi ambao unafanyika nchini kufuatia mkasa huo ulitokea mwaka jana mwezi kama huu Oktoba.

 

Ameeleza kwamba amekuwa tu akisoma kwenye vyombo vya habari na anachokifahamu kufikia sasa ni kwamba kuna mtu mmoja au wawili kutoka Msumbiji, mmoja wa Afrika kusini na mwingine Mtanzania ambaye amewekwa ndani. “Mimi ni mtu nasamehe watu, siweki vitu ndani ya moyo wangu”.

 

MO DEWJI NI NANI?

Mo alizaliwa tarehe 8 Mei mwaka 1975, ikiwa na maana kwamba kwa sasa ana miaka 43.

Alizaliwa eneo la Ipembe, Singida maeneo ya katikati mwa Tanzania.

Kwa mujibu wa jarida maarufu la masuala ya fedha la Forbes, ana utajiri wa dola bilioni 1.5.

Ni wa pili miongoni mwa watoto sita wa Gulamabbas Dewji na Zubeda Dewji.

 

Alisomea elimu ya msingi katika shule ya msingi ya Arusha na baadaye akasomea elimu ya sekondari katika Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST) jijini Dar es Salaam.

Alisomea masomo zaidi ya sekondari Marekani katika jimbo la Florida mwaka 1992.

Alisomea chuo kikuu cha Georgetown jijini Washington DC na kuhitimu mwaka 1998 akiwa na shahada ya kwanza katika biashara ya kimataifa na fedha, na masuala pia ya dini.

 

Baada ya kufuzu, alirejea Tanzania na kuanza kushiriki katika usimamizi wa kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL) iliyoanzishwa na babake miaka ya 1970.

Alihudumu kwa miaka miwili kabla ya kuwa afisa mkuu mtendaji wa kampuni hiyo, wadhifa ambao ameendelea kuushikilia hadi sasa.

 

Dewji pia ni mpenzi wa michezo na amewekeza katika klabu ya mpira ya Simba Sports Club inayocheza katika Ligi Kuu ya Tanzania ambapo ni mfadhili mkuu kwa sasa.

Mo ndiye tajiri namba moja Afrika Mashariki, na pia miongoni mwa matajiri wenye umri mdogo zaidi Afrika.

 

Tathimini ya ukuwaji wa uchumi na Biashara Tanzania

Katika kutathmini kuhusu ukuwaji wa uchumi Tanzania Mo ameeleza kuwa kutokana mtazamo na dira ya nchi, hali ni ya kutia moyo.

“Tanzania inakuwa kwa 6.5% dhidi ya wastani wa ukuwaji wa uchumi Afrika, ambao ni 3%. Mfumuko wa bei uko chini ya asilimia 3.5%, hii ni habari nzuri.”

Kwa mujibu wa benki ya Dunia, Tanzania imeendeleza ukuwaji wa uchumi katika muongo mmoja uliopita, kwa wastani wa kati ya 6% – 7% kwa mwaka.

Kadhalika, idara ya takwimu nchini Tanzania inaeleza kuwa pato jumla la nchi lilikuwa ni 7% mwaka jana, ongezeko kutoka 6.8% mnamo 2017.

 

Hata hivyo, mfanyabiashara hiyo ameeleza kwamba changamoto hazikosekani.

Mojawapo kubwa amelitaja ni ajira, na pia uwekezaji mdogo katika seta kama kilimo na viwanda.

Swali kubwa anauliza Mo ni: “Kwanini viwanda vimefungwa, kwanini havizalishi?

Jibu lake anasema, ili kufanikiwa matatu haya ndio yanahitajika:

 

Tatizo kubwa anasema linalopaswa kuulizwa ni ‘kwanini mali ghafi husafirishwa nje mfano, 90% ya pamba nchini inayowagusa asilimia kubwa ya wakulima na tunazalisha 10%’.

Mfumo anasema ni mzuri lakini tatizo anafafanua ni udanganyifu na ushindani wa haramu katika biashara.

 

Anapendekeza serikali iweke sera zitakazosaidia wafanyabisahara katika sekta hiyo kuwawezesha kuzidisha uzalishaji wa biashara na kusaidia kudhibiti mali za nchi.

Siri ya ufanisi wa Dewji?

Kujituma: Anaeleza ni lazima vijana wawe na nidhamu ya kuwa na muda wa kulala, kuamka na kufanya kazi. Binafsi anaeleza kuwa huamka kila siku saa kumi na moja alfajiri na hufanya kazi kwa saa 80 kwa wiki.

 

Kusoma zaidi: Anausia watanzania hususan vijana wajenge mapenzi ya kusoma. “Watanzania hatupendi sana kusoma, ni heri kusoma umbea kuliko (content) itayotuongezea elimu.”

 

Kujikita katika biashara ndogo: Hii ni kwa mudhumuni ya kutengeza akiba ambayo anaeleza inakuwa ni msingi kwa vijana wanapokwenda kutafuta mikopo kujiendeleza. Inakuwa na uzito zaidi katika kufanikiwa kupata mitaji ya kupanua biashara zaidi.

‘Ili kufanikiwa kupanda lifti, ni lazima upande ngazi’ anasema Mo.

Comments are closed.