Cristiano Ronaldo Kwenye Tuhuma Za Ubakaji

 

POLISI mjini Las Vegas, Marekani, wametoa waranti ya kuchunguzwa kwa chembechembe za vinasaba au DNA ya Cristiano Ronaldo kama sehemu ya uchunguzi wa madai ya ubakaji dhidi ya nyota huyo wa soka wa kimataifa wa Ureno anayechezea klabu ya Juventus.

 

Wakili, Peter S. Christiansen, ameliambia shirika la utangazaji la Uingereza (BBC)  kuwa ombi hilo ”ni la kawaida”.

 

Jarida la Wall Street limeripoti kuwa waranti hiyo imewasilishwa hivi karibuni katika mfumo wa mahakama ya Italia.

 

Ronaldo amekanusha kwamba alimshambulia mwanadada Kathryn Mayorga katika mgahawa mmoja mjini Las Vegas hotelini mwaka 2009.

 

”Bwana Ronaldo amekuwa akishikilia usemi kuwa yale yaliyotokea Las Vegas mwaka 2009 ni mambo ya watu wawili waliokubaliana, kwa hiyo bila shaka chembechembe za DNA zitapatikana, kwa hiyo sioni haja ya polisi kutoa ombi hilo kama sehemu ya uchunguzi wao,” ilisema taarifa ya Christiansen.

 

Gazeti la Der Spiegel la Ujerumani ambalo lilikuwa la kwanza kuangazia taarifa hiyo mwezi Oktoba, lilisema kuwa Bi Mayorga aliandikisha ripoti katika kituo cha polisi cha Las Vegas muda mfupi baada ya kufanyika kwa tukio linalodaiwa.

Der Spiegel lilisema kuwa mwaka 2010, Mayogra aliafikiana na Ronaldo kutatua suala hilo nje ya mahakama ambapo alilipwa dola 375,000 ili asizungumze hadharani madai hayo.

 

Mawakili wake sasa wanasema makubaliano hayo hayakuwa rasmi.

 

Wakili wa Ronaldo amewahi kusema kuwa mteja wake hakukataa kutia saini makubaliano hayo, hivyo “sababu zilizomfanya kufikia uamuzi huo zimepotoshwa”.

 

Aliongeza: ”Hatua hiyo haimaanishi amekiri kuwa na makosa.”

 

Bi Mayorga alipata ujasiri wa kuzungumzia masaibu yake kutokana na kampeni ya “MeToo movement”  ambayo imekuwa ikiendeshwa mtandaoni.

 

Wakili wake amesema kuwa mteja wake atamfungulia mashtaka Ronaldo nchini Marekani.

 

Ronaldo alihamia Juventus kutoka Real Madrid mwezi Julai kwa malipo ya Euro milioni 99.2.

 

Ameshinda tuzo ya Ballon d’Or  ambayo hupewa mchezaji bora wa soka duniani – mwaka 2008, 2013, 2014, 2016 na 2017.

 

Nyota huyo wa kimataifa wa Ureno aliwahi kupinga madai dhidi yake kama “taarifa yenye kughushiwa” na baadaye mwezi Oktoba akatoa taarifa kupitia mtandao wake wa Twitter ambapo alipinga “vikali” suala hilo.

 

Wakili wake anadai kuwa hati za uchunguzi zilizotumiwa na gazeti la Der Spiegel ”ni za kubuniwa” lakini gazeti hilo linasema “halina sababu” ya kutilia shaka uhalisia wake.

 

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Loading...

Toa comment