The House of Favourite Newspapers

Daktari Bingwa Atumwa Kuchunguza Mwili wa Mtoto Aliyeuawa Kagera

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameeleza kusikitishwa kwake na kitendo cha mwalimu mmoja katika Shule ya Msingi Kibeta, wilayani Bukoba, mkoani Kagera anayedaiwa kumuadhibu mwanafunzi wa darasa la tano, Sperius Eradius (13) hadi kusababisha umauti wake akituhumiwa kuiba pochi ya mwalimu.

 

Ummy amesema wizara yake imetuma mtaalamu bingwa wa uchunguzi (Pathologist) kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando kwa ajili ya kwenda kufanya upya uchunguzi wa mwili wa marehemu mtoto huyo ambaye walezi wake wamegoma kuchukua mwili baada ya ripoti ya daktari wa mwanzo kueleza kuwa mtoto huyo alikuwa na majeraha mengine kabla ya kupigwa na mwalimu.

 

Kupitia Twitter, Ummy ameandika;

 

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha mtoto Sperius Eradius aliyekuwa darasa la 5 S/Msingi Kibeta, Bukoba ambapo kimehusishwa na adhabu ya kupigwa na Walimu wake. Ninatoa pole kwa wazazi/walezi, ndugu na marafiki wa marehemu.Mungu awape moyo wa ustahimilivu

“Kufuatia wazazi wa mtoto kutokuwa na imani na uchunguzi uliofanywa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kagera, Wizara yangu imetuma mtaalamu bingwa wa uchunguzi (Pathologist) toka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando kwa ajili ya kwenda kufanya upya uchunguzi wa mwili wa marehemu.

“Tayari mtaalamu huyo ameshawasili Kagera leo asubuhi kwa ajili ya kuanza uchunguzi mpya. Ninatoa wito kwa familia, ndugu na wananchi kuwa watulivu ktk kipindi hiki ambapo uchunguzi wa kibingwa unaendelea. Tutahakikisha kuwa uchunguzi unafanyika kwa ufanisi ili haki itendeke.

“Aidha nitumie fursa hii kuwataka Wazazi/Walezi na Walimu kutambua wajibu mkubwa tulionao wa kuwafundisha na kuwalea watoto wetu kwa kuzingatia sheria na taratibu tulizojiwekea. Vitendo vya ukatili dhidi ya watoto havikubaliki katika jamii yetu na ni kinyume cha sheria za nchi.

“Kama jamii tunao wajibu wa kuhakikisha mtoto anaishi, kukua na kuendelezwa ktk mazingira salama na rafiki kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya 2009. NINALAANI VIKALI Vitendo vya Ukatili vinavyofanywa dhidi ya watoto ktk jamii. Tutawafuatilia na kuwachukulia hatua wanaohusika.

Comments are closed.