DARASA AONYESHA JEURI YA PESA
WAKATI mtazamo wa baadhi ya watu wakiamini kuwa Muziki wa Hip Hop Bongo haulipi kivile, hali imekuwa tofauti kwa staa Sharif Thabeet ‘Darassa’ baada ya kubainika anaishi kwenye mjengo wa kifahari uliopo maeneo ya Bahari Beach jijini Dar.
Tangu atambe na Wimbo wa Muziki miaka miwili iliyopita kisha akaachia Wimbo wa Hasara Roho, Darassa hakuonekana tena kwenye ulingo wa muziki hali iliyozua sintofahamu kwa mashabiki wake.
ALIUNDIWA ZENGWE
Baada ya kujificha kwa zaidi ya mwaka, mwishoni mwa mwaka jana zilivuja taarifa kuwa msanii huyo amejiingiza kwenye matumizi ya madawa ya kulevya ambapo gazeti dugu na hili la Ijumaa lilichimba na kubaini haikuwa kweli.
TUPATE HABARI MPYA
Mwishoni mwa wiki iliyopita, mapaparazi wetu wa kitengo maalum cha Oparesheni Fichua Maovu (OFM) walipenyezewa ubuyu mpya wa mjini kuwa msanii huyo kwa sasa maisha yake yamenyooka na kwamba anaishi kwenye jumba la kifahari na magari mawili ya kutembelea akiwa na mke wake, mtoto mmoja wa kike pamoja na mama yake mzazi.
“Natumai hapo ni kikosi kazi cha OFM, watu wanasema tu kuwa ohhh Hip Hop hailipi kwamba wanaofanikiwa kumiliki majumba ya kifahari ni wa kuimba kama vile Kiba (Ally Salehe) na Diamond (Nasibu Abdul), hivi mmeona maisha ya Darassa anayoishi kwa sasa? Mmeona hayo magari yake? Fanyieni kazi yupo Bahari Beach huku njooni,” kilisema chanzo.
OFM KAZINI
Baada ya taarifa hizo kutua dawatini, OFM ilifuata ramani iliyoelekezwa hatua kwa hatua hadi katika mjengo huo ambapo baada ya kufika getini, walikutana na dada wa kazi katika nyumba hiyo ambaye hakujitambulisha jina.
“Karibuni ndani, karibuni sana!”
MANDINGA YAMEPAKI NJE
Mara baada ya kuingia eneo la ndani ya fensi, OFM ilishuhudia mjengo wa kifahari wa ghorofa moja sambamba na magari ya kifahari; BMW jeusi pamoja na Toyota Alphard.
MENEJA WAKE AFUNGUKA
Wakiwa bado katika mjengo huo ambao walikaribishwa hadi sebuleni, OFM walipata nafasi ya kuzungumza machache na meneja wa Darassa anayefahamika zaidi kwa jina moja la Kimbe.
OFM: Sisi ni waandishi tumekuja kufanya mahojiano na Darassa?
Meneja: Kwa sasa Darassa amelala, huwa ana kawaida ya kushinda studio kwake kwenye hicho chumba cha pili (anaone sha) na ikifika saa moja asubuhi hupumzika. Labda mpange siku nyingine mje kumtembelea. Licha ya kutopata fursa ya kuzungumza na Darassa mwenyewe, OFM iliweza kushuhudia ndani ya mjengo huo wenye ‘sebule kama uwanja wa taifa’ ukiwa umesheheni samani nzuri na za kuvutia.
Ijumaa Wikienda lilitaka kujua zaidi kuhusu mjengo huo wa kifahari kama Darassa amepanga au anamiliki pamoja na maswali mengine lakini meneja wake huyo, aliwataka waandishi wafike siku nyingine wazungumze kila kitu Darassa mwenyewe akiwepo.
ANAMILIKI AU KAPANGA?
Ili kujishibisha zaidi kujua kama kweli anamiliki au amepanga mjengo huo, OFM walitoka moja kwa moja hadi kwa Mjumbe wa Serikali za Mitaa, Athuman Nassor ambaye alisema: “Kwanza hizo taarifa za Darassa kuishi maeneo hayo mnayosema ndiyo kwanza nazisikia kutoka kwenu ila kuna mjumbe mwenzangu anayehusika na masuala ya ardhi ngoja nikawakutanishe naye ili aweze kuwasaidia.”
OFM walipomfikia mjumbe huyo anayehusika na kitengo cha ardhi, Khalfan Suleiman, naye alifunguka hivi: “Ninachokifahamu hiyo nyumba anamiliki mama mmoja anaishi Kunduchi (mama Maua) ila sina uhakika kama ameshaipangisha au ameshaiuza kwani sijafika eneo hilo kwa muda mrefu.”
TUJIKUMBUSHE
Kabla ya kutoka kimuziki, Darassa alikuwa akiishi na mama yake mzazi maeneo ya Kiwalani jijini Dar na baada ya kuanza kukubalika kupitia Wimbo wa Muziki ambao ulimpatia mafanikio makubwa, alihamia maeneo ya Makongo Juu na kuchukua nyumba nzima.
Imeandikwa na Stori: Shamuma Awadhi na Memorise Richard.
Comments are closed.