The House of Favourite Newspapers

DARASA HAPA NI MWISHO AU TUSUBIRI TENA

MOJA ya wasanii ambao wamekuwa gumzo kwenye muziki wa Tanzania kwa muda mrefu ni Shariff Thabeet maarufu kama Darasa. Jamaa huyo amekuwa bora kuanzia kitambo, baadaye akapotea na miaka ya hivi karibuni akaibuka tena na ngoma yake iliyojulikana kwa jina Too Much, hii ilitoka Julai 15, 2016, pamoja na kwamba ilikuwa na mistari mikali lakini haikuhiti sana.

 

Ni ngoma ambayo wapenzi wa muziki wa kipindi hiki walikuwa wanaulizana, huyu ni nani? Wachache sana walimfahamu na kuanza kumfuatilia.

 

Ukitazama leo kwenye mtandao wa You Tube utaiona kuwa imetazamwa mara milioni 3.4, kuanzia mwaka 2016, pamoja na kwamba wasanii wengi hawajafika hapo baada ya kukaa kwenye game kwa miaka 10, lakini kwake ilikuwa simpo tu.

 

Baada ya hapo, Braza alitulia kwa muda wa miezi sita, akajipanga na kuamka tena na bonge moja la ngoma alilolipa jina la Muziki akiwa na fundi Ben Pol.

Huu ulikuwa kama wimbo wa Taifa na kutikisa kila eneo la nchi hii na nchi jirani huku ikipigwa kila mahali, kwenye magari, pikipiki, kumbi za starehe, radio stesheni na televisheni kila kona ilikuwa ni Muziki. Ukitazama leo utakubaliana nami, kuanzia Novemba 23, 2016 hadi kufikia leo wimbo huo umetazamwa mara milioni 13.9.

 

Ngoma ilienda vairo hadi Kenya na Uganda,na kufanikiwa kuchukua tuzo ya East Africa Awards, Ni wanamuziki wachache sana wa Tanzania ambao wameweza kufikia hapo ni kiwango cha juu sana tena kwa msanii ambaye alipotea muda mrefu.

 

Braza akatulia, Mei 5, 2017, akaja na ngoma nyingine hatari sana, Hasara Roho, ilisikilizwa lakini ikaisha utamu haraka na hadi leo imetazamwa na watu milioni 3.4.

 

Hasara Roho ilikuwa kazi nyingine mzuri kutoka kwa CMG Darasa lakini ilimezwa na ukubwa ngoma ya Muziki amabyo aliitoa miezi michache nyuma.

Baada ya hapo yalizungumzwa mengi, kila mmoja aliongea lake kuhusu msanii huyu, wengine wakasema kuwa hawezi kurudi tena kwenye muziki, l a k i n i yote yamebaki kwenye vitabu, baada ya zaidi ya mwaka na nusu Darasa huyu hapa tena na ngoma yake mpya ya Achia Njia.

 

Ngoma hii ilitoka Desemba 14, 2018, ni ngoma ambayo haikuwa na promo kubwa, zaidi ya wengi kuingia kwenye mtandao wake wa Instagram wakaona ameposti kipande cha video baada ya kutokuwa ameingia huko kwa zaidi ya mwaka mzima, ikafahamika kuwa kuna kitu kinakuja, kweli baadaye Achia Njia ikatoka.

 

Wengi walifikiri kuwa Darasa atarejea kama alivyoondoka, lakini ikawa tofauti kwenye mistari hakuna tofauti kubwa, somo ni lilelile kama ilivyokuwa kwenye Muziki, Too Much na Hasara Roho hakukuwa na promo nyingi, hakufanya kiki yoyote, lakini leo baada ya mwezi na uchee braza ametazamwa na watu zaidi ya milioni 1 bila mbwembwe.

 

Alipofika milioni moja, hakusema, hakutangaza wala hakujisifu kuonyesha kuwa kuna kitu amekifanya kikubwa kama ilivyokuwa pia kwenye Too Much na Muziki. Ajabu sana, pamoja na kwamba hakuna promo, hakuna kiki jamaa anatoboa tena ingawa wengi w a n a s e m a hakuja kama walivyokuwa wanategemea.

 

Ndiyo hata Too Much ilianza taratibu, ikaja Muziki ikateka nchi, nafikiri bado tunatakiwa kumsubiri Darasa atarejea tena, au tusubiri tuzoee ngoma hii.

 

Achana na hiyo, Januari 25, amekuja na ngoma nyingine akiwa amemshirikisha Marioo bado hajatoa video yake, lakini kasi yake hii inaonyesha kuwa kuna jambo anataka kufanya, labda tusubiri kumuona tena braza, kwa sababau anaonekana kuwa na moto ule ule.

 

Baadhi ya interview ambazo Darasa amekuwa akifanya amezungumza mambo mengi sana ambayo ni shule kwenye maisha ya kawaida na Muziki wa Tanzania, lakini anakiri kuwa hakufaidika kwenye nyimbo alizotoa hapo nyuma kama jinsi alivyokuwa maarufu.

 

“Kwenye muziki wetu kutengeneza jina ni rahisi sana, lakini kutengeneza fedha ni kazi sana, mimi nilitaka kuwa kwenye daraja ambalo nalitaka lakini kuna ambao wapo wanaotaka kukuonyesha kuwa hicho unachofanya siyo sahihi, njia ya kupita ni huku,” alisema Darasa.

 

Nafikiri hadi sasa tunatakiwa kumsubiri Darasa, labda atakuja tena, au ajitokeze na kusema kuwa hapo ndiyo mwisho, lakini najua wengi bado wanasubiri kasi kama ile ya Muziki.

MAKALA NA PHILIP NKINI

Comments are closed.