The House of Favourite Newspapers

Dawa ya Kunasa Wezi Yazua Balaa!

WIKI kadhaa baada ya kuibuka kwa taharuki iliyosababishwa na kijana Salum Hamisi ‘Frank Joseph’ aliyedaiwa kunasiana na mzigo wa wizi kichwani huko Mlandizi, Kibaha mkoani Pwani, mwanamke mmoja naye ameibua balaa kufuatia kutangaza kutoa dawa ya kunasia wezi.

 

Mwanamke huyo, Esther Chacha (55),  hivi karibuni alitiwa mbaroni mchana kweupe na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Tarime na Rorya mkoani hapa kwa tuhuma ya utapeli kupitia dawa ya kunasia wezi.

 

Esther asiyefahamika makazi yake, yalimfika baada ya kudaiwa kumtapeli Neema John Masaga fedha taslimu shilingi milioni 1.6 kwa kujifanya sangoma kisha kumfanyia dawa hiyo ya kunasia wezi, lakini haikufanya chochote.

 

Esther alidaiwa kumhakikishia Neema kuwa, dawa hiyo ingemuwezesha kuwanasa wezi wa ng’ombe wake 11 na kuwarejesha nyumbani kwake, Mugumu wilayani Serengeti.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Tarime na Rorya, SACP Henry Mwaibambe aliliambia Uwazi kwamba, mwanamke huyo alikamatwa jirani na Stendi Kuu ya Mabasi Tarime baada ya kuwekewa mtego. Alisema kuwa, baada ya kumkamata atasafirishwa kupelekwa Kituo cha Polisi cha Mugumu kwani huko ndiko alikofanyia tukio hilo la utapeli akiwa na wenzake.

SACP Henry Mwaibambe.

Kamanda Mwaibambe alisema Polisi watahakikisha wanabaini mtandao wa matapeli hao na kuukomesha popote walipo kwani kumezuka wimbi la matapeli wa aina hiyo wakijifanya ni wataalamu wa mambo hayo ya uganga na mitandao. 5Alisema kuwa, kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Mugumu, mwanamke huyo alimtapeli Neema Februari 16, mwaka huu alipokabidhiwa shilingi milioni 1,600,000 kabla ya kutumiwa fedha nyingine shilingi 60,000.

 

Taarifa hizo za Polisi Mugumu zilieleza kuwa, mwanamke huyo, akiwa na wenzake, alikabidhiwa kiasi hicho kisha akapulizia pumzi kwenye chupa mbili za soda ambapo kulitokea moto katika chupa hizo.

Ilielezwa kuwa, aliziweka chupa hizo kwenye zizi la ng’ombe kisha aliondoka zake. Ilisemekana kwamba, baada ya kutengeneza dawa hiyo, mtuhumiwa huyo alimwambia Neema kuwa, ng’ombe wake 11 waliokuwa wameibwa wangejitokeza wakiwa na wezi sita ambao wangefika nyumbani hapo wakiwa wamelewa kisha kukiri kufanya wizi huo.

 

Pia alimuahidi Neema kuwa, zoezi hilo lingechukua muda mfupi wa siku 12 tu tangu kuwekwa dawa hiyo.Hata hivyo, siku zilikatika, lakini Neema hakuona chochote ndipo alipokimbilia Kituo cha Polisi Mugumu.

Ilielezwa kuwa, Esther alifunguliwa jalada la kesi lenye namba MUG/ IR/1623/2018 –KUJIPATIA FEDHA KWA NJIA YA UDANGANYIFU ndipo mtuhumiwa akaanza kusakwa.

Ilisemekana kuwa, kila Esther alipopigiwa simu na Neema ili kujua hatima ya zoezi hilo hakupatikana hadi alipokamatwa na Polisi ambapo anasubiri kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

 

Kwa mujibu wa Neema, alikuwa na uchungu kwa sababu aliuza ng’ombe wake 12 ili kupata fedha ambazo alimpatia mwanamke huyo aliyejifanya sangoma.

Kumekuwa na wimbi la matapeli wanaojifanya waganga wa kienyeji ambao wametapakaa kila kona nchini siku hizi hivyo Polisi wamekuwa wakiwataka wananchi kuwa makini na utapeli wao au kuwaripoti mara tu wanapowashtukia.

STORI: IGENGA MTATIRO, MARA

Comments are closed.