The House of Favourite Newspapers

Dc Aagiza Afisa Uthamini Kukamatwa, Kisa Kuzima Simu

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mkoani Dar es Salaam, Hapi Ali (Kulia) akimsikiliza mmoja wa wakazi wa Wilaya ya Kinondoni Dar es Salaam.

Na MWANDISHI WETU|IJUMAA WIKIENDA| HABARI

DAR ES SALAAM: Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Dar (DC), Ally Hapi ameagiza Jeshi la Polisi kumuweka ndani siku mbili, Afisa Uthamini wa wilaya hiyo, Einhard Chidaga kwa kosa la kutotekeleza majukumu yake na kudharau wananchi, kitendo kinachodaiwa kusababisha uwepo wa migogoro ya ardhi katika wilaya yake. 

Hapi alitoa agizo hilo jana kwenye mkutano wake na wananchi uliofanyika katika Viwanja vya Mkanada, Wazo jijini Dar baada ya baadhi ya wananchi kulalamika kutolipwa fidia zao na manispaa licha ya uthamini wa viwanja vyao kufanyika.

Hapi Ali

Katika mkutano huo ilitakiwa Afisa Uthamini huyo awepo ili kutoa ufafanuzi lakini hakutokea huku simu yake ya mkononi ikiwa haipatikani. Hapi alisema kuwa, afisa huyo hatekelezi majukumu yake inavyotakiwa kwa kuwa tangu ameanza ziara ya kutembelea wananchi ili kujua kero na changamoto zao, Chidaga hajawahi kuhudhuria kwenye ziara zake.

“Polisi mtafuteni alale ndani saa 48. Anajua kabisa kuna mkutano wa wananchi na kwamba anahitajika kusikiliza na kutoa majibu ya malalamiko ya wananchi lakini amezima simu,” alisema Hapi.

Comments are closed.