DC JOKATE: SINA AKAUNTI YA VIKOBA, MSITAPELIWE!
MKUU wa Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani, Jokate Mwegelo, amewataka Watanzania waelewe kwamba hana akaunti yoyote ya vikoba kwenye mitandao ya kijamii ya Instagram au Facebook inayotoa mikopo kwa wananchi.
Akizungumza jana katika Ofisi za Global Group zilizopo Sinza-Mori, Dar, Jokate amesema kumekuwa na watu ambao wametengeneza akaunti feki wakijifanya ni yake na kuwatapeli wananchi kwa kuwachangisha kwa maelezo kwamba anatoa mikopo.
“Mimi sina akaunti yoyote ya vikoba na sijihusishi na jambo hilo, kwa vyovyote waliofungua akaunti hiyo kwa jina langu ni matapeli, wana nia ya kuwaibia wananchi,” amesema Jokate.
Akifafanua zaidi, mkuu huyo wa wilaya kijana amesema amekuwa akipokea wageni mbalimbali wengine kutoka mikoani ofisini kwake wakidai kwamba wametuma fedha kwenye akaunti hiyo feki ya vikoba.
“Jana tumepokea mtu kutoka Tabora anadai amefuatilia akaunti hiyo feki kwa sababu alituma fedha, niwafahamishe wananchi kwamba sina vikoba mimi na wala sijafungua kwenye akaunti yoyote, iwe kwenye Instagramu au mitandao mingine yeyote,” amesema Jokate na kuwasisitizia wananchi kuwa makini na matapeli hao.
Hivi karibuni kumekuwa na mtindo wa matapeli kutumia mitandao ya kijamii kuwaibia wananchi na wengine kutumia simu kufanya uhalifu huo, jambo ambalo jeshi la polisi limekuwa likituma ujumbe kwenye simu za kiganjani kutahadharisha watu kujihadhari na wizi wa aina hiyo.
Jokate akiwa katika picha na baadhi ya wafanyakazi wa Global Group mwishoni mwa ziara yake.
PICHA NA MUSA MATEJA | GPL
Comments are closed.