The House of Favourite Newspapers

KIPANDA USO UGONJWA HATARI KULIKO UNAVYODHANI

KIPANDA uso cha macho ni maradhi yanayosababisha maumivu ya kichwa yakiambatana na matatizo ya macho ambayo huuma.  Maumivu haya huweza kutokea bila dalili zilizozoeleka za kipanda uso na mara nyingi husababisha kuona kwa shida ambapo macho huona kama wingu zito au kutoona kabisa kwa kipindi kinachozidi saa moja.

Zipo sababu za ugonjwa huu. Wagonjwa tofauti wanaweza kuhisi moja ya kati ya nyingi zilizopo. Unaweza kutokana na kufinywa au kupungua kwa upenyo wa mishipa ya damu inayopeleka damu sehemu ya mbele ya ukuta wa jicho au au mabadiliko kwenye mshipa wa fahamu wa jicho (optic nerve).

Yaweza pia kutokana na maradhi yanayohusisha mfumo wa damu kama vile seli mundu au mwanga mkali unaomulika ghafla machoni. Pengine ikawa harufu kali ya marashi au sauti kubwa. Msongo wa mawazo, wasiwasi na unywaji wa pombe kupita kiasi ni sababu nyingine. Hata unywaji wa kiasi kikubwa cha kahawa nayo husababisha tatizo hilo bila kusahau mabadiliko ya hali ya hewa.

Ugonjwa huu unaweza kumpata yeyote lakini wenye historia ya kuugua wapo kwenye hatari zaidi. Tafiti za kisayansi zinaonyesha maradhi haya hurithiwa. Hii ina maana familia ambazo zina historia ya watu waliowahi kupata maradhi haya huwa kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa huu.

Kipanda uso cha macho kina uhusiano na homoni ya kike iitwayo Oestrogen hivyo kumaanisha huonekana zaidi kwa wanawake kuliko wanaume. Siyo tu huonekana zaidi kwa wanawake bali kwenye vipindi fulani kutokana na kuongezeka au kupungua kwa homoni hizo, mfano kipindi cha hedhi.

Kipanda uso cha macho huwa na dalili zinazofanana na kipanda uso cha kawaida kama vile kichwa kuuma, kupata kizunguzungu, kusikia kichefu chefu na mara nyingine kutapika. Ingawa dalili nilizotaja hapo juu huwa zinaonekana kabla au wakati wa maumivu makali ya kipanda uso si mara zote hutokea kwenye kipanda uso cha macho.

Kuumwa kichwa unapotazama mwanga mkali au kusikia sauti ya juu ni dalili nyingine ya ugonjwa huu. Lakini dalili kubwa ya kipanda uso cha macho ni kuona taswira ya vitu kama nyota au mwanga mkali wa mistari mistari.

Wengine huona giza muda mfupi kabla tatizo kutokea. Dalili ya kuona mwanga mkali wenye nyota nyingi ni dalili inayoripotiwa na wagonjwa wengi zaidi. Hali hii hudumu kwa kipindi kifupi kisichozidi dakika sitini au saa moja. Dalili za maradhi haya mara nyingi hufanana na za maradhi mengine hivyo mgonjwa anatakiwa amuone daktari ili apimwe na vipimo vitathibitisha.

Historia ya maradhi na vipimo vikionyesha kuwa kweli tatizo la mgonjwa ni kipanda uso cha macho basi atapewa dawa za kutuliza maumivu ya kichwa na kuzuia kuongezeka kwa shinikizo la damu kwenye macho. Yapo madhara ya kipanda uso cha macho ambacho mara nyingi husababisha maumivu makali yanayomfanya mgonjwa kushindwa kufanya shughuli zake za kawaida ingawa huwa haudumu kwa muda mrefu.

KIPANDA USO CHA MACHO NI DALILI ZA KIHARUSI

Mara nyingi kipanda uso cha macho huwa ni ishara ya maradhi mengine makubwa na yenye matokeo mabaya zaidi. Ugonjwa huu unaweza kuambatana na majeraha au uvimbe kwenye ubongo.

Pengine waweza kuwa dalili ya kiharusi au kutanuka kwa mishipa ya damu kwenye ubongo (aneurysm) kama siyo maradhi ya mishipa ya damu inayosambaza damu kwenye ubongo. Yaweza kuwa ishara ya maumivu ya mishipa ya fahamu au kichwa kikubwa (hydrocephalus) hasa kwa watoto. Wakati mwingine humaanisha upungufu katika maumbile ya fuvu la kichwa.

TIBA, USHAURI USHAURI

Uonapo dalili tulizozitaja hapo juu unashauriwa kumuona daktari ambaye atakupima na akigundua tatizo atakutibu na atakupa dawa na utapona kwa sababu ugonjwa huu unatibika. Ni vema kufanya mazoezi ya viungo ili kuepuka kupatwa na kiharusi lakini pia epuka kula vyakula vilivyopikwa na mafuta ya wanyama badala yake tumia mafuta ya mimea kama vile alizeti, mafuta ya karanga, ufuta, nazi nk.

Comments are closed.