The House of Favourite Newspapers

DC Kilolo Akalia Kuti Kavu, Majaliwa Aagiza Achunguzwe – Video

WAZIRI Mkuu  Kassim Majaliwa amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Happi,  afuatilie utendaji kazi kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Asia Abdallah,  ambaye pamoja na mambo mengine amekataa madereva kumi.

 

Hatua hiyo inatokana na watumishi 14 wa ofisi hiyo wakiwemo madereva 10 kuhamishwa baada ya mkuu huyo kudai hawafanyi kazi ipasavyo.

 

Hata hivyo, Majaliwa mesema ni muhimu kwa viongozi wakatambua dhamana zao katika utekelezaji wa shughuli zao pamoja na kuwatambua, kuwajali na kuwathamini watumishi wa kada zote wakiwemo madereva, hivyo ni vizuri wawaandae kwa kuwapa maelekezo kwa wakati kwa kuwa nao ni binadamu na wana familia.

 

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana Ijumaa, Septemba 27, 2019, wakati akizungumza na watumishi, halmashauri  na madiwani akiwa  katika siku ya nne ya ziara yake ya kikazi mkoani Iringa.

 

Majaliwa amesema pamoja na shughuli za maendeleo wanazofanya katika wilaya hiyo lakini hawana mshikamano, hivyo amemtaka mkuu huyo ahakikishe anashirikiana vizuri na wenzake kwa sababu watumishi wengi wamehamishwa tangu aingie katika ofisi hiyo na hata wanaoletwa wanalalamika na wanaomba wahamishwe.

 

Amesema watumishi wengi katika ofisi hiyo anawaona hawana uwezo wakiwemo wasaidizi wake kama madereva, watunza kumbukumbu na makatibu muhtasi.

 

“Hata aliyekuwa katibu tawala wa wilaya hiyo alihamishwa kwa sababu za kutoelewana na DC na hata huyu Katibu Tawala wa Wilaya aliyepo sasa hana raha anataka kuhama kwa sababu hizo hizo,” alisema Majaliwa.

 

“Lazima tuwatambue wasaidizi wetu na majukumu yao. Ofisi ya Mkuu wa Wilaya haiwezekani ikawa hivi, lazima kuna shida kuwaondoa watumishi wote, Mkuu wa Mkoa fuatilia hii ni mpya,” amesema na kuongeza:
“Hapa tujue mbovu ni nani?   Mkuu wa Mkoa tunataka tujue DC wako anataka dereva wa aina gani, tangu amefika hapa madereva 10 wote hawafai,” amesema.

 

Majaliwa amesema, “Ili mfanye kazi vizuri mnatakiwa mshikamane mfanye kazi kama timu moja kwani pamoja na shughuli mnazofanya hamna ushirikiano.”

 

“DC sasa utabaki peke yako utakuwa unaandika mwenyewe, unaendesha gari mwenyewe maana wote hawafai. Mkuu Mkoa nakukabidhi majina ya watumishi hao ushughulikie suala hili. Na Katibu Tawala wa Mkoa usilete watumishi wengine hapa mpaka suala hili litakapopatiwa ufumbuzi,” amesema.

 

Katika hatua nyingine, Majaliwa ameziagiza halmashauri zote nchini zihakikishe zinatenga kiasi cha fedha katika makusanyo yao ya ndani kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa miradi ya kimkakati kwenye maeneo yao kama ujenzi wa vituo vya afya, barabara za halmashauri na masoko badala ya kutegemea fedha kutoka Serikali Kuu pekee.

 

Amesema wilaya ya Kilolo ambayo haina kituo cha mabasi inatakiwa itenge fedha kutoka kwenye makusanyo yao na kuanzisha mradi wa kituo hicho ambao utekelezaji wake utaboresha huduma kwa wananchi pia, mradi huo utasaidia katika kuongeza mapato ya halmashauri. Halmashauri ya wilaya ya Kilolo inakusanya sh. bilioni nne kwa mwaka.

 

Waziri Mkuu amesema watumishi wanapaswa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwani wananchi wanahitaji waone matokeo ya uwepo wao kutokana na dhamana waliyopewa na Serikali katika wilaya hiyo.

“Madiwani nanyi simamieni halmashauri yenu vizuri kwa sababu nyie ndiyo wenye dhamana ya kuhakikisha wananchi wanahudumiwa vizuri,” amesema Majaliwa.

 

Awali, Mbunge wa Kilolo (CCM), Venance Mwamoto ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Magufuli kwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika wilaya yao ikiwemo ya umeme, ambapo kati ya vijiji 94 vilivyoko vijiji 54 vimeunganishiwa huduma hiyo na vilivyosalia vitakuwa vimeunganishiwa umeme ifikapo Desemba 2019.

 

Akizungumzia kuhusu miradi ya maji mbunge huyo amesema kati ya vijiji 94 vya wilaya hiyo vijiji 15 tu ndio bado havina maji ya uhakika lakini wanaendelea na mchakato wa ufuatiliaji ili kuhakikisha navyo vipate maji safi na salama.

 

Mapema , Waziri Mkuu amekagua mradi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya na kupokea taarifa ya ujenzi wa hospitali hiyo ambapo alisema ameridhishwa na ujenzi huo uliogharimu sh. bilioni nne na alitumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi wa wilaya hiyo akiwemo Mkurugenzi pamoja na mkandarasi anajenga.

Comments are closed.