The House of Favourite Newspapers

DC: Msitumie WhatsApp kutuma nyaraka za kiserikali ni hatari

0

mg_whatsapp_code_compNa Mwandishi Wetu

KATAVI: Baada ya wananchi kulalamikia kero ya baadhi ya watumishi wa serikali kuwa hutuma nyaraka za kiserikali kwa njia ya WhatsApp, Mkuu wa Wilaya ya Mlele, mkoani Katavi, Rachel Kasanda amepiga marufuku watumishi wa umma wilayani kwake kutuma nyaraka hizo kwa njia hiyo kwani ni hatari.

Wananchi wilayani humo walilalamika kuwa kuna baadhi ya watumishi wa serikali wamekuwa wakituma nyaraka hizo kwa njia hiyo ndipo mkuu huyo wa wilaya akasema kusafirisha nyaraka za serikali kwa njia ya mtandao ni njia isiyotambulika na ni kosa kisheria.

Mkuu huyo wa wilaya aliamua kuzungumza na watumishi hao hivi karibuni wakati anajitambulisha baada ya kuteuliwa na Rais Dk. John Pombe Magufuli kuongoza wilaya hiyo ambapo alisema ameelezwa kero hiyo kwamba kuna baadhi ya watumishi wanatumia mitandao ya kijamii kama WhatsApp ambayo serikali haijaelekeza kutumia kutuma nyaraka zake.

“Kuna wakati utakuta nyaraka zinahitajika wizarani haraka, mtumishi naambiwa, anaamua kuipiga picha kwa simu nyaraka husika na kumtumia mtumishi mwenzake wizarani kwa njia ya WhatsApp,” alisema.

DC Kasanda alisema kufanya hivyo ni kosa na watumishi wa umma wanapaswa kutambua kuwa baadhi ya yanyaraka za serikali ni za siri wakati njia hizo hazina siri kwani kuna uwezekano hata mataifa mengine kudukua siri za serikali.

“Nyaraka zote za serikali lazima zitumwe kwa kutumia barua pepe zilizoidhinishwa na serikali na si vinginevyo,” aliamuru mkuu huyo mpya wa wilaya.

Aliongeza kuwa ni wajibu wa kila mtumishi wa umma wilayani humo kubadilika na kujituma katika kuwatumikia wananchi kwani serikali ya awamu ya tano ya Dk. Magufuli imeamua kushuka chini na kuwajali wananchi ambao ndiyo waajiri wao namba moja.

Leave A Reply