The House of Favourite Newspapers

Walioua polisi kituoni waibuka tena

0

MAREHEMU ENZI ZA UHAI WAKE (13)-001Ramadhani Mkagile enzi za uhai wake.

Issa Mnally na Richard Bukos, UWAZI

PWANI: Hali inatisha katika Kijiji cha Kimanzichana, Wilaya ya Mkuranga, Pwani kufuatia mauaji yanayofanywa na wanaodaiwa kuwa wafuasi wa kundi la kigaidi baada ya kumuua kwa kumpiga risasi mwenyekiti wa kijiji hicho, Ramadhani Mkagile, Uwazi limefuatilia.

Mwenyekiti huyo, aliuawa Julai 17, mwaka huu alipokuwa akisimamia mafundi waliokuwa wakijenga nyumba yake nyingine huku ikidaiwa kwamba, waliomuua ndiyo walewale waliowahi kuvamia Kituo cha Polisi cha Kimanzichana na kumuua polisi.

Kabla yake, mapema mwaka huu, watu hao wanadaiwa kumchinja karani wa Mahakama ya Mwanzo ya Mkuranga aliyetajwa kwa jina moja la Pazi na kumkata kwa majambia katibu wa kijiji hicho, Rajab Simkole.

Akizungumza na Uwazi kijijini hapo, shuhuda wa tukio hilo (jina lipo), alisema siku hiyo akiwa eneo hilo, alimuona mwenyekiti huyo akiwa na mafundi wake huku akiongea na mzee aliyepakana naye uwanja aliyemfahamu kwa jina la Magenge.

“Ghafla niliwaona vijana wawili wakiwa kwenye pikipiki aina ya Boxer. Walimpita kidogo marehemu kama mita kumi na tano kisha wakasimama, wakavaa kininja na kumrudia.

“Nilisikia wakimwambia; ‘nadhani sisi unatujua lakini leo ndiyo mwisho wa uhai wako’. Mmoja alichomoa bastola na kumfyatulia mwenyekiti huyo risasi mbili upande wa kushoto wa kichwa chake, zikamfumua na kutokea upande wa pili na kuanguka palepale.

“Mzee Magenge aliwauliza jamani mbona mnamuua amewafanyia nini? Kabla hajajibiwa, naye alipigwa risasi moja iliyompata kwenye goti la kushoto.

“Baada ya kufanya unyama huo, walitoweka lakini walionekana ni wenyeji kwa jinsi walivyokuwa wakichanja vichochoro. Tulichofanya ni kwenda kutoa taarifa polisi ambao walifika na kuuchukua mwili kwa ajili ya kwenda kuufanyia uchunguzi na Mzee Magenge alikimbizwa Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga lakini baadaye alipelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili baada ya hali yake kuzidi kuwa mbaya,” alisema shuhuda huyo.

Baadaye Uwazi lilizungumza na ndugu mmoja wa marehemu ambaye alikataa kutaja jina lake kwa kuhofia usalama wake ambapo alisema marehemu alianza kupata   vitisho kwa muda mrefu kutoka kwa kundi moja linalodaiwa kuwa na majina 18 ya watu ambao wanataka kuwatoa roho baada ya kuwachongea kwa jeshi la polisi kwa tuhuma za uhalifu.

Ndugu huyo alinong’ona kuwa, kundi hilo mwaka jana lilimpora silaha na kumuua askari mmoja kwenye Kituo cha Polisi Kimanzichana kilichopo mita chache kutoka nyumba ya mwenyekiti huyo.

Inadaiwa kuwa, kufuatia mauaji hayo, walikamatwa watu 18 waliosemekana kuhusika na matukio hayo ambao walihojiwa na kuachiwa huru na ndipo muda mfupi baada ya kuachiwa, likatokea tukio la kuuawa mwenyekiti huyo.

Staili ya wauaji hao inadaiwa ni kuua bila kuchukua mali yoyote kutoka kwa waliyemuua, hali inayoonesha ni mauaji ya visasi.

Naye mjane wa marehemu huyo, Sada Issa alisema: “Mume wangu kwa muda mrefu alikuwa akiniambia maisha yake yako hatarini kufuatia jina lake kutajwa kwenye orodha ya majina 18 ya watu wanaotakiwa kuuawa na kundi linalojiita Al Qaeda. Ukweli hata mimi niliogopa lakini nilikuwa nikimtia moyo mpaka mauti yalipomkuta.”

Mwenyekiti huyo ameacha mke na watoto wanne; Sofia, Mwajuma, Amran na Bakari. Mwili wake ulizikwa Jumanne iliyofuata kwenye Makaburi ya Kijiji cha Mikele Njia Nne, Mkuranga.

Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, ACP Bonaventura Mshongi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Akizungumzia kundi linalotajwa kuendesha mauaji eneo hilo ambalo limetajwa kujiita Al Qaeda, kamanda huyo alisema hilo bado hawajalithibitisha na linaweza kuthibitishwa baada ya watuhumiwa kukamatwa na kubanwa.

“Lakini watuhumiwa wote tunawasaka na watapatikana tu na kufikishwa kwenye mkono wa sheria,” alisema Kamanda Mshongi.

Leave A Reply