The House of Favourite Newspapers

Deci waanza upya

1

fedhazetu-001Stori: Elvan Stambuli, UWAZI

DAR ES SALAAM: Wanachama wa Development 

Entrepreneurship for  Community Initiative (Deci ), wameanza upya kulalamika na sasa wamemuomba Rais John Magufuli kuingilia kati urudishwaji wa fedha zao ambazo zinashikiliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kipindi kirefu sasa wakidai kwamba kuna viongozi ndani ya serikali wanaitumia sheria kukwamisha urejeshaji wa fedha hizo kwao.

Wakizungumza na gazeti hili juzi jijini Dar wanachama hao walisema fedha zao zipo BoT huku wao wakiteseka kutokana na ukweli kwamba wengine ‘walipanda’ baada ya kukopa sehemu mbalimbali ndiyo maana wanamuomba Rais Magufuli kuliangalia upya tatizo hilo.

“Sikuona sababu ya serikali kukata rufaa baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuamuru fedha za wanachama warejeshewe wanachama kwa sababu hakuna hata senti moja ya serikali mle,” alisema mmoja wa wanachama wa Deci aliyejitambulisha kwa jina la Khadija Mohammed.

Naye Charles Massawe alisema wameamua kumuomba Rais Magufuli fedha hizo kutokana na ukweli kwamba ni mtu aliye na huruma kwa wananchi wake anaowaongoza.

“Kwa kweli Deci ilifanya kazi kwa kipindi kirefu na sisi wote tukaiamini, kwa hiyo viongozi wa serikali walioiachia mpaka ikawa maarufu ndiyo majipu , watumbuliwe na wananchi warejeshewe fedha zao kwani wanateseka sana,” alisema Massawe.

Hata hivyo,  Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mabenki wa Benki Kuu ya Tanzania, Kennedy Nyoni alikaririwa hivi karibuni akisema kuwa benki hiyo haina dhamira yoyote ya kuendelea kushikilia fedha za Deci kama baadhi ya watu wanavyofikiria bali wanasubiri kukamilika kwa taratibu za kimahakama.

“Tunayo taarifa kuwa serikali imekata rufaa, hivyo haitakuwa busara sisi kutoa fedha hizo kwa wahusika bila kujua uamuzi wa Mahakama ya Rufaa Tanzania,” alisema.

Alifafanua kuwa kwa kuwa hukumu iliyotolewa Mahakama Kuu ya Tanzania imekatiwa rufaa, utekelezaji wa urudishwaji wa fedha kwa wanachama wa Deci hautafanyika hadi rufaa hiyo itakapotolewa uamuzi japo kuwa wana taarifa kuwa hadi sasa haijapangiwa jaji wa kuisikiliza.

Suala la Deci liliibuka mwaka 2009 baada ya serikali kuingilia kati shughuli za taasisi hiyo kwa kusimamisha shughuli zake kisha kuwakamata viongozi wake na kuwafikisha mahakamani.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ikawahukumu kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya sh milioni 21 vigogo wanne wa Deci.

Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Alocye Katemana, pamoja na adhabu hiyo pia aliiagiza serikali ifanye mchanganuo wa mali za Deci ambazo inazishikilia, kwa kuwa zipo mali zilishikiliwa zisizo za kampuni hiyo bali za watu wengine.

Alisema kuwa fedha za wateja wa Deci walizopanda zirejeshwe kwa wateja wenyewe ambao wataonesha uthibitisho wa kweli kuwa walipanda fedha zao huko.

Katika hukumu hiyo iliyotolewa na Hakimu Mkazi, Stewart Sanga na kusomwa na Hakimu Katemana, washtakiwa walikuwa watano, ambao ni Jackson Mtares, Dominick Kigendi, Timotheo ole Loitginye, Samwel Mtares na Arbogast Kipilimba.

Hakimu Katemana alisema washtakiwa hao ambao ni wachungaji wa makanisa ya Pentekoste walitiwa hatiani kuanzia wa kwanza hadi wa nne, isipokuwa mshtakiwa wa tano aliachiliwa huru baada ya mahakama kumuona hakuwa na hatia katika makosa hayo mawili.

1 Comment
  1. Upendo Lema says

    Magufuli mtenda haki atawasikia wanyonge

Leave A Reply