The House of Favourite Newspapers

DEREVA WA TRENI MBARONI BAADA YA KUKUTWA AMELEWA

JESHI la Polisi Mkoa wa Tabora limewakamata watu watatu kwa matukio tofauti akiwemo dereva aliyekuwa akiendesha treni ya abiria huku akiwa amelewa na wengine wawili waliokutwa wakisafirisha madawa ya kulevya aina ya bangi.

 

Taarifa ya polisi iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo  imemtaja dereva aliyekamatwa akiendesha treni ya abiria akiwa amelewa kuwa ni Elirehema Macha mkazi wa Dodoma.

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora Kamishna Msaidizi Emmanuel Nley,  alisema  dereva huyo alikamatwa wiki iliyopita baada ya kuendesha treni ya abiria namba B 12 iliyokuwa ikitoka Dar es Salaam kuelekea Kigoma akiwa amelewa na kutosimama katika kituo cha Malongwe.

 

Aliongeza kuwa kitendo cha dereva kutosimamisha treni kwenye kituo hicho kilileta taharuki kwa abiria waliokuwa wakiteremka na wale waliokuwa wakitaka kupanda ndipo taarifa ikatolewa polisi ambapo walimkamata.

 

Katika tukio jingine Kamanda Nley alisema polisi imewakamata watu wawli wakiwa na madawa ya kulevya aina ya bangi.  Watu hao ni Amos Maziku ambaye ni ajenti wa mabasi na Hassan Selemani dereva ambao walikutwa kwenye kituo cha mabasi cha Sagara cha mjini Nzega wakiwa na madawa hayo yenye kilo 51.45 wakiyasafirisha.

 

Alisema  watuhumiwa hao walikuwa wakisafirisha bangi hiyo kwenye basi la Shabco lenye namba za usajili T 501 BRZ lililokuwa likielekea jijini Mwanza wakiwa wameyaweka ndani ya ndoo kubwa ya maji na wameifunga ndani ya mifuko ya  sandarusi wakiwa wamechanganya na sufuria na sahani ili isijulikane.

 

Aidha alisema katika misako inayoendelea,  wamefanikiwa kukamata silaha mbili zilizotengeneza kienyeji.

Comments are closed.