The House of Favourite Newspapers

KWA TABIA HIZI ZA…., DIAMOND KAMA MSHUA WAKE

Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’

WASWAHILI wanasema siku zote maji hufuata mkondo! Katika maisha ya kila siku, wanadamu tumekuwa tukiutumia msemo huo kwa kufananisha maisha ya mtoto pamoja na yale wazazi wake waliyoyaishi.  

 

Japo sio lazima yafanane lakini msemo huo siku zote huwa umekuwa ukishabihiana na uhalisia wa maisha ya watoto na wazazi hao. Ndio maana kuna wengine husema mtoto umleavyo, ndivyo akuavyo.

 

Licha ya kutofanana kila kitu lakini kwa mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na baba yake Abdul Juma, yapo mambo kadhaa yanayoonekana kufanana na kutengeneza ule msemo wa Kingereza wa Like Father Like Son ambao kwa tafsiri isiyo rasmi inamaanisha kwamba; baba anafanana na mwanaye:

UBRAZAMENI

Kama ni mfuatiliaji mzuri wa familia ya Diamond na baba yake basi hiki kitu hakitakuwa kigeni kwako, ukimuangalia Diamond sasa hivi na jinsi anavyojiweka halafu ukaja kumuangalia na baba yake utagundua kuwa Diamond ‘karithi’ kabisa ubrazameni toka kwa mzee wake.

 

Kuanzia mapigo ya nguo anazotupia, mapozi ya kwenye picha, kuvaa cheni, yaani baba yake mtupu ingawa sasa hivi baba yake umri unamtupa mkono lakini bado ana ubrazameni. Angalia nguo ambazo mzee huyo anazivaa, angalia mapozi anayoweka kwenye picha utasema bado kijana kumbe umri unaelekea kumtupa mkono.    

KUBADILI WAREMBO

Diamond anafahamika kwa kubadili warembo licha ya kuonekana kupenda kumuonesha kwa jamii mwanamke mmoja wa uhakika. Miongoni mwa warembo aliowahi kutembea nao Diamond na kuonesha kwamba ni wa uhakika huku akiwa ameanzisha uhusiano mwingine kwa siri ni pamoja na Wema Sepetu, Penniel Mungilwa ‘Penny’, Hamisa Mobeto, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ na Jokate Mwegelo.

 

Kwa upande wa mshua wake, pia amekuwa si mnyonge sana, enzi za ujana wake anatajwa kuwa na warembo tofautitofauti japo alikuwa akimuanika mmoja ‘serious’ akiwemo mama yake Diamond (Sanura Kassim ‘Sandra) na mwanamke mwingine ambaye anaishi naye hadi sasa.

KUZAA NA WANAWAKE TOFAUTI

Mbali na kuwa na wanawake wa kila aina, Diamond ameonekana pia kuzaa na wanawake tofautitofauti ambapo nyota yake ilianza kuonekana kwa Zari, mwanamke mjasiriamali ambaye kazaa naye watoto wawili, lakini pia akazaa na mwanamitindo Mobeto.

Kwa upande wake baba Diamond naye ana watoto wanne ambao kila mmoja ana mama yake, Diamond ana mama yake ambaye ni Sandrah, Queen Darleen ana mama yake, ana mtoto mwingine wa kike ambaye anaitwa Amina, huyo kazaa na mwanamke mwingine ambaye kwa sasa anaishi nchini Zambia na ana mtoto wa kiume naye ana mama yake.

KUISHI MBALI NA FAMILIA

Hili pia linafanana kwa mzee Abdul na Diamond. Diamond kwa sasa haishi na watoto wake; Tiffah na Nillan wapo Afrika Kusini na mama yao, lakini hata Dylan aliyepo hapa Dar naye haishi naye nyumba moja kwani yeye anaishi Madale lakini mtoto wake anakaa Mbezi Beach na mama yake.

Hilo lipo pia kwa baba yake mzazi, kwani katika watoto wake wote wanne aliozaa hakuna hata mmoja anayeishi naye.

KUPENDA MUZIKI

Tunaposema like father, like son kweli ipo kwa familia hii kwa sababu mzee Abdul ukienda mara nyingi kwake basi utamkuta kafungulia muziki mkubwa anasikiliza Bongo Fleva, vivyo hivyo kwa Diamond anayeupenda na kuufanya muziki huo kama kazi yake.

Memorise Richard.

Comments are closed.