The House of Favourite Newspapers

DIAMOND HATARINI KUFUNGIWA MAISHA!

DAR ES SALAAM: Baada ya kufungiwa kufanya shoo ndani na nje ya nchi kwa muda usiojulikana, mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ana hatari ya kufungiwa kujihusisha na muziki maisha yake yote endapo tu atathubutu kufanya vitendo vinavyoashiria kulitunishia msuli Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Ijumaa limeelezwa.  

 

Diamond, mkazi wa Madale- Tegeta jijini Dar alifungiwa kufanya shoo Jumanne iliyopita kutokana na madai ya kuendelea kuupafomu Wimbo wa Mwanza almaarufu Nyegezi katika Tamasha la Wasafi. Wimbo huo ulifungiwa na Basata Novemba 12, mwaka huu.

TAARIFA KUTOKA BASATA

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Basata, Diamond yupo hatarini kufungiwa maisha kujishughuilisha na shughuli za kimuziki endapo tu atajaribu kuleta malumbano ya hoja kama alivyowahi kufanya mara kadhaa huko nyuma. 

TUJIUNGE BASATA

Mmoja wa maofisa wa Basata ambaye alizungumza na Ijumaa alieleza kuwa, mara kadhaa Diamond amekuwa akionywa na Basata, lakini amekuwa akijaribu kutunisha msuli kwa kuona pengine anaweza kubebwa na umaarufu wake. “Unajua Diamond anafikiri kwamba pengine kwa sababu ni maarufu na jina lake ni kubwa hadi nje ya nchi, basi anaweza kufanya tu jambo lolote na sisi tukamuangalia, haipo hivyo, sanaa inaongozwa kwa sheria, taratibu na kanuni zake,” alisema ofisa huyo aliyeomba hifadhi ya jina.

MCHAMBUZI ANENA

Mbali na ofisa huyo, mmoja wa wachambuzi wa habari za burudani Bongo aliyeomba hifadhi ya jina alilieleza Ijumaa kuwa, Diamond anapaswa kuwa makini kwani anaonekana ana tabia ya kutunisha msuli wake pindi anapopewa maelekezo na mamlaka hususan viongozi wa Serikali. “Kama utakumbuka kipindi kile aliwahi kutunishiana msuli na mheshimiwa Juliana Shonza (Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo) baada ya kufungiwa nyimbo zake mbili (Wakawaka na Halelujah).

“Mjadala ulikuwa mkubwa sana mitandaoni na mitaani, waziri anatoa maelekezo, Diamond anamjibu kwa lugha kali sana kwenye mahojiano aliyoyafanya redioni, jambo ambalo lilisababisha watu wengi kuhoji anapata wapi jeuri ya kumjibu waziri ambaye ameteuliwa na Rais kwa maneno ya shombo kiasi kile?” Alihoji mchambuzi huyo.

FEDHA ZIMEMLEVYA?

Kama hiyo haitoshi, mchambuzi huyo alikwenda mbali zaidi kwa kusema, anamuona Diamond ni mtu ambaye umarufu na fedha alizonazo zinampa jeuri kwani hata kwenye sakata la hivi karibuni la kuchelewa ndege jijini Mwanza nalo pia alithubutu kuwatunishia msuli Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).

“Inabidi ajiangalie, mambo kama yale aliyoyafanya kung’ang’ania kwamba hakuchelewa bali wahudumu waliuza tiketi zake. ATCL wakalazimika kuitisha mkutano wa waandishi wa habari (press) kujitetea kupitia kwa msemaji wao, lakini wapi, Diamond bado alizidi kusisitiza kwamba hakuchelewa, aliwahi ndege, lakini wahudumu waliuza siti yake,” alisema mchambuzi huyo.

VIDEO YAKE YAIBUA MAMBO

Wakati mjadala wa Diamond kufungiwa ukiwa wa moto, kwenye mitandao ya kijamii kulilipuka moto zaidi baada ya kusambazwa upya kwa video ambayo alikuwa akimchana Waziri Shonza miezi kadhaa iliyopita.

Wachangiaji mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii waligawanyika. Kuna ambao walifikiri video hiyo ni mpya na kumuonya Diamond kwamba asimlaumu mtu pindi yatakapomkuta makubwa kwani Basata hawawezi kumvumilia, watamuongezea adhabu. Mbali na hao, wapo pia wachangiaji wengine ambao waliweza kuifahamu video hiyo siyo mpya, bali ni ya zamani na kuwashambulia wale ambao walikuwa wanamponda Diamond kwa maneno makali wakidhani ni video mpya.

BASATA WANASEMAJE?

Jitihada za kumpata Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza ili kusikia anazungumziaje kuhusu mwenendo wa Diamond sambamba na adhabu waliyompa hazikuweza kuzaa matunda kufuatia simu yake ya mkononi kuita muda mrefu bila kupokelewa.

DIAMOND, MAMEJA NAO HAWAPATIKANI

Ijumaa pia lilijaribu kumtafuta Diamond na mameneja wake wote juzi, lakini hawakuweza kupatikana. Hamis Taletale ‘Babu Tale’ namba zake mbili zilionekana kufungiwa huku ile ya Said Fella ikiita muda mrefu bila kupokelewa.

Comments are closed.