The House of Favourite Newspapers

Dianmond Kufanya Kufuru ya Funga Mwaka!

0

 

 

HII ni zaidi ya shoo ya kufunga mwaka! Ukiachana na shoo yake kukusanya mastaa wengi kuliko, siri ya mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kuwakusanya mastaa maadui zake katika jukwaa la Wasafi, imefichuka, IJUMAA WIKIENDA linakuletea uhondo kamili.

 

NI DISEMBA 31

Diamond au Mondi anatarajia kuwakutanisha mastaa wahasimu wake kwenye shoo ya kufunga mwaka 2019 na kuukaribisha mwaka 2010 itakayofanyika Desemba 31, mwaka huu kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma.

 

Mastaa ambao kwa miaka tofauti walikuwa kwenye tofauti na Mondi kama Raheem Rummy Nanji ‘Bob Junior’, Kifesi, Suleiman Mirundi ‘Mwarabu Figther’, Richard Martin ‘Rich Mavoko’ na Q-Boy, tayari wamealikwa na wanatarajia kuwepo siku hiyo.

 

Mondi ameendelea kuporomosha orodha ya mastaa mbalimbali watakaokuwa Kigoma siku hiyo ambapo vyanzo vinaeleza kuwa, wapo wengine kibao aliokuwa na tofauti nao akiwemo Nurdin Bilal Ali ‘Shetta’ na Emmanuel Elibaliki ‘Nay wa Mitego’.

 

SIRI NI NINI?

Kwa mujibu wa chanzo ndani ya Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Mondi ameamua kuwakusanya wasanii hao ili kuzidi kujitengenezea heshima ya kuendelea kuwa juu.

 

“Diamond anajua kabisa yupo juu mno, sasa anataka kuzidi kuwa juu! Hivyo, namna pekee ya kuendelea kuwapata watu ni kuonesha upendo hasa kwa watu aliotofautiana nao huko nyuma,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

 

“Wewe fikiria, wale wote ambao ni maadui zake wana mashabiki wao, hivyo kwa kitendo cha yeye kuonesha uungwana (kuwaalika), hata wale mashabiki wao nao watamuunga mkono yeye.”

 

FELLA ANENA

Mmoja wa mameneja wa WCB, Said Fela ‘Mkubwa Fella’ naye ameeleza kwa upande wake siri ya kuwarejesha wote kwenye shoo hiyo maalum kwamba ni kwa ajili ya Mondi kutimiza miaka kumi tangu aanze muziki.

 

Amesema jambo kubwa lililowasukuma kufanya hivyo ni upendo ambao wapo nao Wasafi tangu kuanzishwa kwake na familia yao kwa jumla.

“Sisi kauli yetu ni kwamba, hatufanyi kwa ajili ya kutengeneza utengano katika timu ndiyo maana mpaka leo unaona Fela yupo, Babu Tale yupo na Nasibu (Mondi) mwenyewe yupo.

 

“Tunafanya haya ili kuunganisha nguvu ili jamii ijue nini tunafanya kwa upendo mkubwa.

“Vilevile tunatengeneza maisha kwa kila kijana maana yake kwenye ujana kuna mambo mengi yanatokea kwa kuwa unaweza ukatengeneza chuki zisizokuwa na msingi, kumbe hujui kuwa unatengeneza hasara zisizo na msingi.

 

AMHURUMIA MAVOKO

“Mimi mpaka leo roho inaniuma kumuona Rich Mavoko hafanikiwi kama jina lake lilivyo kubwa. Alikuwa anaenda vizuri sana katika wasanii ninaowapenda na ninaongea kila siku kutoka kwenye moyo wangu kwa sababu alikuwa anafanya vizuri zaidi, lakini wakatokea watu wakamshawishi upuuzi na mambo mengi yaliyopitapita bila sababu mpaka, leo hafanyi vizuri kama mwanzo. Inaniuma sana!

 

“Lakini kwa kuwa nia yetu ni kuwa wamoja na ndilo lengo letu, kuonesha upendo kwa kila mtu, ndiyo maana kwenye miaka kumi lazima tumualike na yeye aje Kigoma tueneze upendo na mwisho wa siku sanaa yetu izidi kukua,” alisema Fela.

 

TUJIKUMBUSHE

Kwa nyakati tofauti, Mondi alijikuta akitofautiana na baadhi ya mastaa ambao alianza nao safari yake ya muziki na kusababisha malumbano kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Hivyo shoo hii, inakwenda kumkutanisha na baadhi ya mastaa ambao kwa namna moja au nyingine, hakuwahi kukutana nao kwa miaka kadhaa.

 

NI SHOO YA KIHISTORIA

Mbali na kuwakutanisha mastaa karibu wote wa Wasafi watakaolishambulia jukwaa moja, watakuwepo pia mastaa wengine katika nyanja za filamu na tasnia nyingine mbalimbali.

 

ORODHA MPAKA SASA

Baadhi ya mastaa ambao tayari Mondi amewataja kuwa watakuwepo siku hiyo hadi mwishoni mwa wiki iliyopita ni pamoja na Blandina Chagula ‘Johari’, Irene Uwoya, Khadija Kopa, Lulu Euggen ‘Amber Lulu’, Jacqueline Wolper na Rashinda Wanjara.

 

Wengine ni Nyandu Toz, Mwarabu Figther, Young Killer, Linex Mjeda, Aunt Ezekiel, Tessy Chocolate, Esma Khan, Kifesi na mkongwe wa Bongo Fleva, Dully Sykes.

STORI: NEEMA ADRIAN,WIKIENDA

Leave A Reply