The House of Favourite Newspapers

DIMBWI LA DAMU-11

Mlinzi alizidi kumvuta 
Nicholaus kumrudisha  
wodini lakini kwa Nicholaus kitendo hicho kilikuwa ni kuingia hatarini! Kukamatwa kwake kulimaanisha kifo na hakuwa tayari kufa kama tayari alishanusurika na kifo katika tetemekeo la ardhi!
“Wewe si ndiye uliyekuwa upigwe risasi siku ile ya tetemeko nashanga ni kwanini    hawakukugundua hebu twende!” Alisema askari akizidi kumvuta Nicholaus.

“Lakini meno yanaweza kunisaidia!” Aliwaza Nicholaus na kuangaza macho yake huku na kule, nyuma yake aliona kundi kubwa na mbwa likimfuata.

“Hapana ni lazima nijaribu kujiokoa hawezi kunikamata kibwege kiasi hiki!”Aliwaza Nicholaus na hapohapo bila hata kuchelewa aliikunja shingo yake kisawasawa   mdomo wake ukatua kwenye mkono wa askari.

Aliyashindilia meno yake yote ya mbele ndani ya mwili wa askari huyo! Aliyasikia  yakipenya sawasawa ndani ya nyama zake, askari alilia kwa maumivu makali lakini Nicholaus hakujali alizidi kuyazamisha! Damu nyingi ilitiririka kupitia pembeni mwa mdomo wake  hilo halikumfanya aache kuyazamisha meno yake, alidhamiria kujiokoa kutoka mikononi mwa kifo.

“Aaaaagh! Nakufa!” Alilia askari huyo huku akijaribu kuutoa mkono wake mdomoni kwa Nicholaus lakini haikuwezekana! Ghafla meno  yakatoka na kipande cha mnofu! Askari alianguka chini kwa maumivu makali.

Kwa Nicholaus huo ulikuwa upenyo wa kujaribu tena kuokoa maisha yake! Lakini aliwaogopa mbwa waliokuwa wakimsubiri na kumuungurumia pembeni yake! Alijua kitendo chake cha kukimbia kingemaansiha kuandamishwa na mbwa na kwa umri aliokuwa nao alijua     isingekuwa rahisi kuwashinda nguvu mbwa hao wakubwa kama ndama!

Akiwa katika mawazo hayo ghafla alimwona askari akijaribu kunyanyuka ardhini ili amfuate, alionekana  mwenye hasira kali! Kabla hajakaa vizuri Nicholaus alimfuata na kumpiga teke sehemu ya siri! Teke lake hilo lilifanikiwa kutua moja kwa moja kwenye korodani zake, akaangua kilio kingine na kurejea tena ardhini!

“Mama yangu mtoto wewe una balaa!” Alipiga kelele.

Nicholaus hakutaka kupoteza muda zaidi palepale alianza kutimua mbio kwenda upande wa pili, kundi kubwa la mbwa wakibweka lilimfuata.

“Sijui nifanye nini sasa?” Aliwaza huku akikimbia.

Ghafla wazo  jipya lilimwijia kichwani ingawa hakuwa na uhakika kama lingeweza kumsaidia, alikitemea mkononi kipande cha mnofu kilichokuwa mdomoni mwake na kukitupa nyuma yake walikokuwa mbwa,  kikatua usoni kwa mbwa aliyekuwa akiongoza mbio hizo! Mbwa wote walisita na kuanza kugombania kipande hicho cha nyama! Nicholaus akapotelea gizani.

“Vipi?

“Nilikikamata kitoto kimoja kilitoroka wodini!”

“Kitoto gani?”

‘Ni kile kilichotakiwa kupigwa risasi sababu ya kuigiza madawa ya kulevya hapa Iran kabla ya tetemeko!”

“Kilikuwa wapi?”

“Kumbe kilikuwa kimelazwa wodini!”

“Sasa kipo wapi?”

“Kimekimbia!”

Yalikuwa ni mahojiano kati ya mlinzi aliyeng’atwa na Nicholaus na walinzi mwenzake wa kampuni ya Metropol Security iliyoilinda  hospitali hiyo walipofika eneo  hilo mbio baada ya kusikia mwenzao akilia kwa sauti!

“Kimeelekea wapi?”

“Huko wanakobweka mbwa ndiko kimekimbilia!”

Walinzi nao walisikiliza kwa makini sauti ya mbwa ilikotokea na watatu kati yao walianza kukimbia kuelekea upande huo lengo lao likiwa kumkamata Nicholaus! Walipofika walikuta mbwa wamezuiliwa na senyenge za hospitali na hakumwona Nicholaus mahali popote.

Nicholaus alishauruka uzio wa  senyenge na kutua upande wa pili ambako aliendelea kukimbia zaidi, kifua kilimbana sababu ya kukimbia sana lakini hakukata tamaa alizidi kuongeza kasi akipita katika majani marefu!

Ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuwa katika jiji la Tehran na hakuelewa mahali popote lakini hakuogopa alizidi kusonga mbele akiwa amekaa tamaa na alikuwa tayari kwa lolote! Mbele kidogo alijikwaa kwenye chuma na kuanguka, alipotupa macho mahali alipojikwaa aliiona reli ikipita alinyanyuka na kuanza kuifuata reli hiyo.

Alijua ni  ingemfikisha  stesheni ilikuwa ni reli ya kuelekea kwenye visima vya mafuta vya Aldharfi, vilivyokuwa maarufu kwa uzalishaji wa mafuta katika nchi ya Iraq, reli hiyo iliunganisha nchi ya Iran na Iraq.

Alitembea bila kujua muelekeo   lakini alijua kwa uhakika ni lazima   angefika katika stesheni ambako angekuta watu, mpaka wakati huo hakuwa na  hofu ya kukamatwa  tena hivyo alizidi kutembea kwa kasi kwenda mbele zaidi! Alitembea juu ya reli na kila gari moshi lilipokuja alijificha  pembeni kwenye nyasi na kulipisha! Alitembea hivyo hivyo usiku kucha bila kufikia kituo chochote.

Mpaka jua linachomoza na Nicholaus alikuwa bado akitembea katikati ya reli, tena akiwa katika pori asilolifahamu vizuri, hakujua lilikuwa na  wanyama gani wakali au la!  Lilikuwa ni pori lililotisha lakini hakuogopa alizidi kusonga mbele, hakukata tamaa alitaka kujiokoa.

Kwa masaa mawili alizidi kutembea porini akifuata reli lakini mbele zaidi alichoka na kukaa juu ya reli  kwa sababu ya uchovu alijikuta akipitiwa na usingizi  na kulala juu ya  reli.

********

Treni la abiria lililobeba vibarua wapya kutoka Tehran kwenda kwenye visima vya mafuta vya Mohamed huko Iraq lilikuwa likitimua vumbi porini  lilikuwa na  mwendo wa kasi  kupita kiasi, wafanyakazi walikuwa wakiwahishwa kazini!Walikuwa ni vibarua wapya wa  tajiri Mohamed aliyemiliki visima vingi vya mafuta nchini Iran, Iraq na Kuwait.

Mzee Mohamed mwenyewe alikuwemo ndani ya treni hilo baada ya kurejea kutoka Tehran ambako mke na mtoto wake walifariki kwa tetemeko la ardhi.

Hakuna mtu hata mmoja kati ya watu wote waliokuwemo ndani ya behewa la dereva wa treni   aliyejua kuwa kilometa moja mbele yao Nicholaus alilala juu ya reli akiwa usingizini na kuota ndoto juu ya dada yake Victoria! Dereva alizidi kuongeza mwendo!

“Ongeza kasi tafadhali tumechelewa sana!” Mzee Mohamed aliamuru.

“Sawa mzee! Lakini tutawahi tu leo~”

“Lakini mimi utaniacha kambini   akili yangu bado haijatulia kidogo baada ya kufiwa na mke na mtoto wangu! Ninahitaji kupumzika”

“Sawa mzee!” Alijibu dereva akiwa amemwangalia mzee Mohamed alipogeuza macho yake kuangalia mbele alisikika akipiga kelele!

“Mungu wangu tumeua!”

“Nini?”

“Kuna mtu katikati ya reli!”

“Funga breki!” Tajiri aliamrisha na dereva alijitahidi kufanya hivyo lakini  kwa sababu ya kasi ambayo  treni ilikuwa nayo haikuweza kusimama   ilijivuta kwa nguvu kuelekea mahali Nicholaus alipolala relini! Lengo la dereva lilikuwa kumuokoa lakini ilionekana siyo rahisi!

“Mama yangu wee tunakufaaa!” Vibarua ndani ya mabehewa walisikika wakipiga kelele!

Nicholaus alizisikia kelele hizo na  alipofumbua macho tayari treni lilishafika karibu yake kabisa tairi zake za chuma zilikuwa kama hatua moja kutoka alipolala! Hakuwa na njia ya kujiokoa alijua  hicho kilikuwa kifo! Akaanza kusali sala ya baba yetu uliye mbinguni ili asife katika dhambi.

***************

Ulikuwa ni uhakika  kuwa Victoria alikuwa mjamzito, hilo halikuwa na mjadala hata kidogo! Alilia kila siku na kushindwa kuelewa  angemweleza nini  Leah akirudi kutoka Bombay alikokwenda kupumzika! Ilikuwa ni aibu kubwa mno kwake na alijua wazi huo ndio ulikuwa mwisho wa uhusiano wake na mkombozi wake Leah! Aliamini hata angemwambia alibakwa asingekubali.

Alihisi mateso  yalikuwa yamerejea tena, shida zake zlikuwa zimeanza upya! Alishindwa kuelewa angekwenda wapi kama Leah angemfukuza  nyumbani kwao.

Alijua angerudishwa Tanzania, lakini huko  angeishi na nani? Aliamini hakuwa na ndugu wa kumtegemea! Victoria alichanganyikiwa na alishindwa kuelewa ni kitu gani kilikuwa mbele yake.

Alichokuwa na uhakika nacho kilikuwa ni mateso! Alijua    wakati wake wa kuteseka tena ulikuwa umefika baada ya kupumzika kwa kipindi! Alitamani kaka yake Nicholaus angekuwepo lakini asingeweza kumpata tena!

Lawama nyingi alizitupa kwa Shabir kwani kitendo alichomfanyia kilikuwa cha kinyama  na hakikustahili kufanywa na mtu mzima kama yeye, wakati Victoria akilia Shabir alifurahia kitendo hicho   hakumhofia Leah hata kidogo, muda wote alimfariji Victoria na kumwambia hakuhitaji kuwa na wasiwasi wowote, maneno hayo hayakuutuliza moyo wa Victoria na  machozi yake hayakukatika!

“Sina uhakika kama kweli Leah atanielewa!” Aliwaza Victoria kichwani mwake.

******************

Baadaye fikra za kutoa mimba  zilimwijia kichwani na kumwambia Shabir  aliyeupinga mpango huo kwa nguvu zake zote akidai yeye alitaka watoto na Leah alizaa mtoto mmoja peke yake ambaye hakutosheleza ukilinganisha na utajiri aliokuwa nao.

“Lakini kumbuka Leah ni ndugu yangu baba!”

“Usiniite baba tena!”

“Nipo tayari kuitoa hii mimba!”

“Hilo haliwezekani wewe kaa hapa, mama Manjit akirudi atachagua kukaa au kuondoka, najua hawezi kuondoka arudi Tanzania? Amechanganyikiwa?Nyie wote mtakuwa wake zangu na mimi nitakutunza vizuri sana Victoria usiwe na shaka!”

“Sitaki! Wewe ni baba yangu tu!”

“Baba yako? Wakati tayari una mimba yangu?” Alisema Shabir kwa dharau.

Maisha yaliendelea na mimba ilizidi kukua na kukomaa, hatimaye ikafikisha miezi mitatu! Kila siku asubuhi Victoria alitapika na kuugua! Alipoteza uzito mkubwa sana  wa mwili wake kwa sababu ya kutokula na mawazo mengi aliyokuwa nayo kichwani mwake, hofu ilimtawala maishani.

Waliendelea kuishi wawili tu  nyumbani, bibi Sundra baada ya likizo yake kwisha alirudi lakini alifukuzwa kazi bila sababu yoyote! Victoria  alitamani bibi Sundra awepo lakini haikuwa hivyo.

Bibi Sundra alikwenda mara mbili kuomba arudi kazini lakini mzee Shabir alimkatalia lakini mimba ya Victoria ilipoanza kuonekana  wazi aligundua ni kwanini hakutakiwa  kuishi pale, alikoma kabisa kwenda nyumbani kwa Shabir! Alimhurumia sana Victoria lakini hakuwa na la kufanya kumsaidia.

“Nitaitoa mimba hii! Kweli nitaitoa!” Hayo ndiyo yalikuwa mawazo yaliyotawala kichwa cha Victoria ingawa hakujua jambo hilo angeweza kulifanya vipi.

“Ningekuwa na macho ingekuwa rahisi zaidi lakini upofu umenitesa!” Aliendelea na mawazo hayo hadi mimba ikafikisha  miezi minne bila hata kupata njia yoyote ya kukamilisha jambo hilo! Kwa taarifa aliyopewa na Shabir zilikuwa zimebaki  wiki mbili tu Leah arejee kutoka Bombay na Victoria hakutaka Leah aikute mimba hiyo.

“Lakini si ninaweza kufanya  mwenyewe?” Aliwaza Victoria siku moja katikati ya usiku na kuanza kukumbuka somo la Biolojia juu ya uzazi alilofundishwa na mwalimu  wake shuleni!  Victoria alipenda  biolojia kuliko masomo mengine yoyote shuleni.

“When a woman is pregnant,   a sac called  Amniotic sac is formed and inside the sac the feotus lies! A fluid called Amniotic fluid is found inside that sac, that fluid enables the feotus to  swim! If an accident happens and the sac is punctured all the fluid will drain out and the baby will die!(ndani ya mfuko wa uzazi wa mwanamke awapo mjamzito kuna kifuko kiitwacho Amniotic sac ambamo mtoto huogelea kwenye maji yaitwayo Amniotic fluid kama ikitokea ajali na kifuko hicho kikatoboka maji yote hutiririka na  mtoto  hufa!) Victoria aliyakumbuka maneno ya mwalimu wake wa biolojia darasani na yalimpa matumaini  ya kuitoa mimba peke yake ndani ya chumba!

“Kumbe nikitoboa tu kifuko hicho na maji  yakmwangika   mtoto atakufa na mimba itaharibika!”Aliendelea na mawazo  yake Victoria.

Alijua  alikuwa akipanga mauaji tena ya mtoto wake lakini hakusikia uchungu wowote ndani ya nafsi kwani ilikuwa ni bora kupoteza kitu chochote duniani lakini si uhusiano wake na Leah! Aliamini bila yeye asingeishi duniani.

“Nitatumia mrija wa kunywea soda na nitausukuma hadi ndani mpaka nikitoboe kifuko na maji yamwagike!”Alizidi kupanga Victoria, alikuwa amedhamiria kuitoa mimba yake.

*************

Kulipokucha asubuhi alimuomba Shabir aliyelala naye kitanda  kimoja ampe soda ya baridi na bila kusita Shabir alikwenda kwenye jokofu akachukua soda na kumletea Victoria kitandani.

“Ahsante sana baba, nipe na mrija tafadhali!”Shabir alichukua mrija na kumkabidhi Victoria, alishangazwa na tabia ya Victoria asubuhi hiyo, alitoa ushirikiano wa kutosha kuliko siku nyingine zote.

“Leo kazini huendi baba?” Aliuliza Victoria sababu alitaka aondoke ili akamilishe lengo lake la kuitoa mimba kwa mrija wa kunywea soda!

“Nitaondoka sasa hivi acha nijiandae!”Alisema Shabir na kuingia bafuni, alipotoka alivaa na kuaga, Victoria akabaki peke yake ndani!

“Huu ndio wakati  muafaka ni lazima niitoe hii mimba, siwezi kukubali Leah anikute nayo!”Baada ya kuwaza hayo tu Victoria aliweka soda yake chini akanyanyuka na kuvua nguo zote alizovaa ikiwemo nguo ya ndani kisha akachuchumaa sakafuni.

“Ee Mungu nisamehe nimelazimika kufanya kitendo hiki bila kupenda!” Alisema Victoria kwa sauti ya chini huku akilia, hakukipendea alichokuwa akikifanya hakutaka kuua!

Aliuchukua mrija na kuanza kuusukuma kuungiza ndani ya mwili wake, yalikuwa ni maumivu makali kuliko mengine yoyote aliyowahi kuyapata maishani, ingawa aliumia sana bado alizidi kuuchoma mrija ndani zaidi mpaka maji mengi yakamwangika  kama bomba na kuilowanisha sakafu, kwa sababu alikuwa kipofu hakujua maji yale yalikuwa ni damu au maji ya kawaida.

Ghafla alisikia kizunguzungu na kuangukia chini, hakuelewa kitu chochote baada ya  hapo hakuwa na fahamu hata kidogo.

 

 Je, nini kitaendelea?
Tukutane kesho hapahapa.

 

Comments are closed.