The House of Favourite Newspapers

Insane (Mwendawazimu)-13

Huo ndiyo ulikuwa mpango wake, hakutaka kumuacha Fabian kwani aliona kuwa aliharibu kila kitu, hasa kumchukua msichana ambaye alikuwa akimpenda kwa moyo wa dhati.

Alichokifanya ni kuondoka chuoni na kuelekea Tandale kwa Mtogole, huko, akakutana na kundi la vijana wa kihuni waliojiita Mbwa Mwitu lakini wao walikuwa wakifanya kazi ya kuteka watoto wa kishua na kuwataka wazazi wao watoe kiasi kikubwa cha fedha ili wawaachie.

Walikuwa na makazi yao hapo, ilikuwa vigumu kuwafahamu kwani muda wote walionekana wasafi, wenye nguo za bei mbaya huku wengine wakiwa na magari lakini kazi kubwa waliyokuwa wakiifanya ilikuwa ni kuwateka watu mbalimbali na kuihitaji fedha.

Polisi waliwashindwa, kuwafahamu ilikuwa ngumu kwani unaweza kukutana na mtu amevaa shati safi, limepigwa pasi na tai huku usoni akiwa na miwano kumbe upande wa pili wa maisha yake alikuwa katika kundi hilo la watekaji.

Kazi zao zilifanyika kimyakimya, serikali ilipata kazi sana kuwagundua, hawakujua walikuuwa wakipatikana wapi kwani kulikuwa na wengine walisema walikuwa Mburahati, wengine Kigogo na sehemu nyingine lakini ukweli wenyewe ni kwamba vijana hao walikuwa Tandale, tena kwenye kambi moja karibu kabisa na mzee aliyejiita Kibogoyo.

Theo alikuwa na marafiki wengi kutoka uswahilini, alikuwa akikutana nao sehemu mbalimbali na ndiyo haohao ambayo walimuunganishia na wasichana wa uswahilini nha kutembea nao, alipotaka kulitafuta kundi hilo, akawasiliana nao na kuwaambia uhitaji wao, wakamwambia aelekee huko kwani kazi hiyo haikuwa ngumu hata kidogo.

Alipofika Kwa Mtogole, akakata kulia na kuchukua barabara iliyokuwa ikielekea Tandale Sokoni ambapo kabla hajafika huko, akakata kona ya Barabara ya Kiboko Baa ambapo mbele akasimamisha gari pembeni kabisa na daraja lililokuwa juu ya mto mdogo.

Kwa kuwa alikuwa na marafiki zake huko, akawapigia simu, ndani ya dakika kadhaa, wakatokea mahali hapo ambapo wakamchukua na kuanza kuelekea naye katika kambi ya vijana hao ambayo wala haikuwa mbali kutoka hapo walipokuwa.

Walipofika huko, yeye mwenyewe akashangaa, mbele yake kulikuwa na vijana wengi waliokuwa wamevalia nadhifu huku wengine wakiwa na suti, alishangaa, hakuamini kama hao ndiyo waliotakiwa kufanya kazi hiyo iliyokuwa mbele yake, ya kumuua Fabian.

Hakuwaamini kwa sababu hawakuonekana kuwa katili, aliwapuuzia kwa kuwaona watoto wa mama. Akakaribishwa na kupelekwa kwenye ofisi ndogo ya mkuu wa kundi hilo, alipofika huko, akakutana na jamaa akiwa amevalia suti nyeusi huku mkononi akiwa na iPad.

Akakaribishwa na kukaa kwenye kiti kikubwa. Akabaki akiiangalia ofisi hiyo, ilionekana kuwa nzuri mno ambayo ilitakiwa kuwa ofisi ya wizara moja kubwa. Akaelezea shida yake huku akiwa na picha ya Fabian.

“Ninataka huyu mtu auawe haraka sana,” alisema Theo huku akimwangalia mwanaume huyo.

“Kisa?”
“Kwani nyie mpo kwa ajili ya kuua au kujua kisa kwanza?” aliuliza Theo, akaonekana kukasirika kuulizwa swali hilo.

“Ni lazima tujue kisa, tukijua, tunajua ni kifo cha aina gani anatakiwa kupewa,” alisema mwanaume huyo.

“Kanipora demu wangu!”

“Hahaha! Demu anauma sana. Basi sawa, tuachie picha yake na utuambie anapatikana wapi na wapi, tuchoree ramani ya kila kitu kitakachoendelea,” alisema mkuu huyo na hivyo Theo akaanza kufanya kama alichoambiwa.

Alihakikisha anawaambia kila kitu kuhusu Fabian, aliwaelekeza mahali alipokuwa akipatikana, alipopendelea kwenda na kila siku za Jumamosi ilikuwa ni lazima aende Mlimani City kuangalia filamu.

Hakuishia hapo, aliwapa kila kitu walichokuwa wakikihitaji, waliporidhika, wakamwambia aache kiasi cha shilingi milioni kumi na tano, hicho hakikuwa tatizo, akachukua mfuko wa kaki aliokuwa nao na kuwapa kiasi cha shilingi milioni saba huku akiahidi kukamilisha kingine kazi itakapofanyika.

Akaondoka, moyo wake ukaridhika, alijiona kuwa mshindi. Hakumpenda Fabian kwa sababu tu alimchukulia msichana aliyekuwa akimpenda kwa moyo wa dhati. Ndani ya gari, moyo wake ulikuwa na furaha tele kiasi kwamba alitamani apate mbawa na kuruka kurudi nyumbani.

“Acha afe! Kwani wangapi wamewahi kuua kisa mapenzi? Mimi si wa kwanza na sitokuwa wa mwisho,” alisema Theo huku akibadilisha gia tu. Moyo wake ulikuwa na furaha tele.

****

Mapenzi yalikuwa motomoto, kila mmoja alimpenda mwenzake na kutamani kumuonyeshea kwamba alikuwa akimpenda hata zaidi ya mwenzake. Kila siku walikuwa pamoja, kwa kitendo cha Theo kuingilia penzi lao na hatimaye kurudi na kuwa kama zamani kuliwaongezea mapenzi maradufu.

Wakawa na utaratibu wa kwenda Mlimani City kuangalia sinema kila Jumamosi, hiyo ilikuwa ratiba yao ambayo waliipanga iwe hivyo hata kama watakuja kuoana na kuishi pamoja.

Siku zikakatika, katika yote yaliyokuwa yakiendelea, Theo alikuwa akifuatilia kwa karibu sana. Moyo wake uliumia, alilia lakini kuna kipindi alijifariji kwa kuona kwamba kuna siku angefurahi kwani wawili hao wasingeweza kuwa pamoja miaka yote.

“Ipo siku!”

Hata baada ya kwenda katika kundi lile la watekaji na mipango kufanikiwa, hatimaye Jumamosi moja ambayo kama kawaida kwa Fabian na Esther kuelekea katika Ukumbi wa Cinemax uliokuwa Mlimani City walikuwa wakielekea huko, wakati wanatoka mida ya saa nne usiku, wakashtuka wakifuatwa na vijana watatu waliovalia mavazi makubwa.

“Nyie ni wakina nani?” aliuliza Fabian lakini hata kabla hajajibiwa, akanyooshewa bastola kisiri na kutakiwa kunyamaza.

“Njoo huku!’

Akavutwa na kupelekwa katika gari jingine. Esther alikuwa aishuhudia kila kitu, hakujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea, alitamani kupiga kelele lakini kijana mwingine naye akiamnyooshea bastola na kumtaka aelekee katika gari lao.

“Na wewe ingia kwenye gari!” alisema kijana huyo.

Ingawa kulikuwa na watu wengine mahali hapo lakini hakukuwa na mtu aliyejua juu ya wale watu, waliwaona lakini kutokana na kila mtu kuwa kwenye mishemishe zao, wakahisi kwamba watu hao walikuwa pamoja kumbe ndiyo utekaji ulikuwa ukifanyika.

Wote wakaingia ndani ya gari na kuondoka mahali hapo. Ndani ya gari, Fabian hakuelewa ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea. Esther alikuwa akilia tu, mbele yake alikiona kifo, hakuwafahamu watu hao lakini kwa jinsi walivyoonekana, walionekana kuwa watu hatari sana.

“Jamani nimefanya nini?” aliuliza Fabian lakini hata kabla hajajibiwa, akapigwa kitako cha bastola usoni!”

“Nyamaza wewe ngedere,” alisema mwanaume huyo, uso wa Fabian ukaanza kutapakaa damu.

Waliondoka nao, walipofika maeneo ya Mwenge, wakafungua mlango na kumtaka Esther atoke kwani hawakuwa wakimuhitaji. Msichana huyo hakuleta ubishi, akatoka garini, gari likaondolewa mahali hapo, akaanza kupiga kelele lakini ndiyo kwanza watu walikuwa wakimshangaa. Gari lilipoelekea, hakupojua. Akaona kuwa huo ndiyo mwisho wa kuwa na mpenzi wake, Fabian. Akabaki akilia tu.

****

Esther alibaki akilia, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya, alichanganyikiwa mno, alibaki pale barabarani akiomba msaada lakini hakukuwa na mtu aliyemsikiliza.

Akaondoka huku akilia, kitu cha kwanza kabisa kufanya kilikuwa ni kwenda katika Kituo cha Polisi cha Mwenge kilichokuwa karibu na kituo cha zamani cha daladala na kuwaambia polisi hao kitu kilichotokea.

Kila mmoja alishangaa, hakukuwa na aliyeamini kama bado mpaka siku hizo watu walikuwa wakitekwa. Wakamuuliza maswali kujua kama alimuhisi mtu yeyote aliyekuwa amehusika lakini hakujua chochote kile.

Alionekana kuchanganyikiwa, hivyo wakamwambia kwanza apunguze presha ili waweze kujua ni kitu gani walitakiwa kufanya. Alichokifanya Esther ni kuwasiliana na wazazi wa Fabian na kuwaambia kile kilichotokea, baada ya dakika arobaini, Bwana Boniface akawa amefika mahali hapo.

“Kuna nini? Umesema alitekwa? Ilikuwaje?” aliuliza Bwana Boniface huku akiwa amechanganyikiwa.

“Kuna watu walitufuata, wakatuchukua na kumteka,” alijibu Esther.

“Watu gani?”

“Sijui baba…”

Mzee Boniface alichanganyikiwa, mbali na kuwa na watoto wadogo wawili lakini kwa Fabian ndiye alikuwa mtoto pekee aliyezaa na mwanamke aliyekuwa akimpenda kwa moyo wa dhati.

Polisi wakaanza kuwasiliana na polisi wengine kwa kuwaambia kwamba walitakiwa kulipekua kila gari ambalo walilitilia shaka, kazi hiyo ikatakiwa kufanyika haraka sana hata kabla mambo mengine hayajaendelea.

“Msijali! Tutafanya kila linalowezekana mpaka kuhakikisha huyo kijana anapatikana. Polisi hatujawahi kushindwa kitu,” alisema mkuu wa kituo hicho cha polisi.

“Asante sana.”
Wakaondoka na kuelekea nyumbani. Kila mmoja alionekana kuwa na hofu kubwa. Esther alikuwa akilia tu, alikumbuka kilichotokea, picha ile ilipokuwa ikimjia moyoni, machozi yalitiririka mashavuni mwake huku moyo wake ukichoma na kumuumiza vibaya.

“Unahisi nani amehusika?’ aliuliza Bwana Boniface.

“Nahisi ni Theo.”
“Ndiye nani huyo?”

“Kijana kutoka chuoni.”
“Walikuwa na ugomvi?”

Hapo ndipo msichana huyo alipoanza kuhadithia kila kitu kilichokuwa kimetokea, uhasmaa mkubwa uliokuwa kwa watu hao wawili. Esther hakutaka kuficha kitu, alisimulia kila kitu na baada ya kumaliza, kila mmoja akawa na uhakika kwamba huyo Theo alikuwa amehusika.

Walichokifanya ni kutaka kuzungumza naye, walitaka kujua ukweli zaidi, hivyo alichokifanya Bwana Boniface ni kuondoka nyumbani huku akiwa na Esther mpaka Masaki kwa bilionea Edson, walitaka kuzungumza na kijana huyo.

Walipofika huko, wakakaribishwa mpaka ndani kwani kwa jinsi walivyojitambulisha, hakukuwa na aliyehisi kwamba walikuwa watu wabaya. Wakakaa kwenye makochi na kutulia, baada ya dakika mbili, mwanamke mmoja kutokea, alikuwa Bi Rachel.

“Samahani! Tunaweza kuonana na Theo?” aliuliza Bwana Boniface mara baada ya salamu.

“Nyie ni wakina nanii?”
“Huyu ni mwanafunzi mwenzake chuoni.”
“Na wewe?”

Bwana Boniface akaanza kujitambulisha, hakutaka kumficha mwanamke huyo, alichokifanya ni kumwambia ukweli kilichokuwa kimetokea kwamba kuna uwezekano kijana Theo alikuwa amehusika katika utekaji.

Bi Rachel aliwaangalia wote wawili, hakuyaamini maneno yao, Theo hakuwa na roho ya kikatili namna hiyo hivyo ilikuwa ni vigumu kuwaamini moja kwa moja.

Alipoona hilo halitoshi, akawachukua na kuwapeleka katika chumba cha kupumzika, huko, wakakutana na Bwana Edson ambaye alikuwa hoi kitandani. Ugonjwa wa Kisukari ulikuwa ukimsumbua kitandani hapo, alionekana kukata tamaa, japokuwa alikuwa bilionea mkubwa lakini alishindwa kuuondoa ugonjwa huo mwilini mwake.

Alitia huruma kitandani pale alipokuwa. Paja lake la mguu wa kulia lilikuwa limetafunwa, daktari aliyekuwa akimtibu alikuwa ndani ya chumba hicho, muda wote alionekana kuwa bize kumtibu mzee huyo.

Alipowaona wageni hao, akatoa tabasamu pana, akawakaribisha, wakakaa pembeni na kuanza kuzungumza naye. Bwana Boniface alikuwa na uchungu wa mtoto wake, hakutaka kujali hali aliyokuwa nayo mzee huyo, angejisikiaje, alimwambia ukweli juu ya kile kilichokuwa kimetokea.

“Sidhani kama Theo anaweza kufanya hivyo!” alisema baba yake huku akionekana kutabasamu.

“Amefanya kwa sababu alikuwa akimtaka huyu msichana…”
“Hawezi. Nimelea Theo, ni mtoto wangu wa kumzaa hivyo ninamjua vema, hajawahi kufanya tukio baya,” alisema Bwana Edson.

Wakati wao wakiwa nyumbani hapo, Theo alikuwa katika Hoteli ya Casanova akisikilizia kile kilichokuwa kikiendelea huko. Alimchukia Fabian na alitaka kuona kijana huyo akiuawa haraka sana.

Alikuwa akizungumza na watekaji ambao walimwambia kwamba kila kitu kilikuwa tayari, walimteka kijana huyo na kwenda naye msituni kwa ajili ya kumuua hivyo alitakiwa kusubiri.

Dakika ziliendelea kwenda, baada ya saa moja, wakampigia simu na kumwambia kwamba tayari walikuwa wamekwishamuua Fabian na kuuacha mwili hukohuko msituni.

“Safi sana…njooni hapana Casanova niwamalizie fedha zenu,” alisema Theo huku akionekana kuwa na furaha tele.

Hiyo ndiyo kazi ngumu aliyokuwa ameibakiza, baada ya kupewa taarifa kwamba kila kitu kilifanyika na Fabian alikuwa ameuawa, akanyanyua miguu juu ya kutoa tabasamu pana.

Alimshukuru Mungu, alihisi kwamba sasa angeishi kwa amani kwani hakukuwa na kitu alichokuwa akikitamani kipindi hicho kama kuona kijana huyo akiuawa ilimradi tu asimuone tena akiwa na msichana aliyekuwa akimpenda.

Baada ya saa moja, watekaji hao wakafika hotelini hapo na kukutana naye, wakamaliziwa malipo yaliyobakia.

“Kwa hiyo mmemuua?”
“Kama kawaida. Kesho utasikia kuna mwili umeokotwa porini,” alijibu kijana mmoja huku akionekana kuwa na furaha tele.

“Asanteni sana,” aliwaambia na kuagana huku akiwa na uhakika kwamba tayari mbaya wake alikuwa ameuawa, hivyo akaanza safari ya kurudi nyumbani kwao.

 

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Jumatatu hapahapa.

 

Comments are closed.