The House of Favourite Newspapers

Dk 847 Zatosha Kumvuta Mkongo Yanga

0

DAKIKA 847 za michezo ya kimataifa alizocheza winga Mkongo wa AS Vita, Tuisila Kisinda, zimeonekana kuwashawishi vilivyo Yanga ambayo imeonyesha nia ya kumsajili msimu ujao.

Yanga kwa sasa inataka kuhakikisha inafanya usajili wa wachezaji wazuri wa kimataifa kwa ajili ya kukiboresha kikosi chao haswa katika eneo la ushambuliaji ambapo kumekuwa na idadi ndogo ya mabao msimu huu.

 

Kisinda akiwa na AS Vita katika michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, amefanikiwa kucheza michezo 13, huku akifunga bao moja na kutoa pasi tatu za mabao.

 

Winga huyo katika mechi hizo, hakufanikiwa kucheza kwa dakika zote na kuishia dakika 847, kama angecheza zote, zingekuwa 1170.

 

Kisinda mwenye umri wa miaka 20, katika michezo ya ligi ya mabingwa pekee amecheza michezo 11 kwa dakika 749, huku katika Kombe la Shirikisho akicheza michezo miwili kwa dakika 98 ambazo jumla ni 847.

 

Akizungumza na Spoti Xtra juu ya mchezaji huyo, Ofisa Muhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz, alisema uongozi wa timu hiyo baada ya kupokea ripoti ya usajili iliyoachwa na Kocha Mkuu, Luc Eymael juu ya wachezaji anaowahitaji, tayari umeshaanza michakato ya usajili.

 

“Tayari uongozi wa Yanga ulishapokea ripoti kutoka kwa kocha mkuu wa timu ambayo kuna wachezaji ameomba wasajiliwe wakiwemo wale wa nje, mipango inaenda vizuri, hivyo Wanayanga wakae mkao wa kula na lolote linaweza kutokea muda wowote,” alisema Nugaz.

 

Katika hatua nyingine, Yanga ina mpango wa kuachana na wachezaji kadhaa akiwemo David Molinga, Patrick Sibomana na Yikpe Gnamien, kisha kuleta majembe mengine kutokana na kile kilichoelezwa ni kushindwa kutoa mchango wao kwa ufasaha.

 

USAJILI KAMILI UPO HIVI

Ripoti ya Kocha Luc Eymael, amependekeza kuongezwa wachezaji sita msimu ujao na kwamba nafasi zinazohitajika ni kipa awe mzawa au wa kimataifa, beki wa kulia na kushoto ambao wote wazawa.

 

Pia kiungo mkabaji ambaye atakuwa akicheza sambamba na Papy Tshishimbi pamoja na washambuliaji wawili, mmoja mzawa na mwingine wa kimataifa.

 

Katika hilo la usajili, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, alisema: “Kocha ameyaweka mambo yote anayohitaji kwenye usajili ujao, hivyo siwezi kukwambia ni wapi anatamani kuongeza ila zaidi tusubirie dirisha la usajili ambalo litaweka mambo hadharani.”

 

STORI NA MARCO MZUMBE NA MUSA MATEJA

Leave A Reply