The House of Favourite Newspapers

Dk. Bashiru: Wapuuzeni Hao Wapumbavu, Chama Chetu Imara – VIDEO

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Dkt. Bashiru Ally.

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Dkt. Bashiru Ally,  leo Julai 23,  2019,   ametoa wito kwa wanachama wa chama hicho kuwapuuza wale aliowaita wapumbavu, yaani watu wanaoendeleza mjadala usiokuwa na tija ndani ya chama hicho, na akawahakikishia kwamba chama hicho kiko imara.

Bashiru ameyasema hayo jijini Dodoma alipozungumza na wanachama wa chama hicho kuhusu waraka wa makatibu wastaafu wa chama hicho,  Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba, ambapo ameonya kwamba wanachama watakaoendeleza mjadala ndani ya chama hicho ili kujipatia umaarufu wa kisiasa, wakibainika watachukuliwa hatua.

 

“Kuna watu wanasema kwamba CCM imetumbuka na kutumbuliwa,  na kila aina ya kejeli. Kwa kweli Kiswahili chepesi ninachosema ni kwamba wapuuzeni hao wapumbavu, na ole wake mwana-CCM abainike anafanya malumbano ya rejareja; atachukuliwa hatua,” amesema.

 

Aidha, amesema, uongozi wa CCM hautaruhusu malumbano ndani ya chama hicho, huku akieleza kwamba mwenyekiti wake, Dkt. John Magufuli, yuko tayari kuwasamehe watu hao, ili kukijenga chama.

 

“Msijifanye majasiri wa kupambana na kufanya malumbano, hakuna ruksa hiyo kwenye chama chetu. Waacheni wabwabwaje kitotototo watachoka wenyewe,” alisema na kuongeza:

 

“Ole wake mwana-CCM yeyote atakayetaka kutumia fursa ya upumbavu wa wapumbavu wa mwaka kutafuta kiki ya kisisasa ili achaguliwe kwenye serikali za mitaa.  Hapana msifanye hivyo.

 

“Jifunzeni kutoka kwa kiongozi wetu ambaye wakati wote hana muda wa malumbano. Amevumilia, wanaomtusi,  wengine wana umri wa watoto wake lakini amewavumilia na yuko tayari kuwasamehe pia. Lakini kwa kufanya hivyo si kwamba ni mwoga.”

 

Amesisitiza kwamba chama hicho hakikatazi kukosolewa, lakini kina utaratibu wa kukosoa kistaarabu akisema Mwalimu Julius Nyerere “alishatuasa tujisahihishe, kujisahihisha ni kujiimarisha.  Tujikosoe, tukosoane kwa adabu na nidhamu, tuache utoto. Kisiwe chama cha siasa za kipuuzi, kwa sababu majira haya ni ya uchaguzi.”

Comments are closed.