The House of Favourite Newspapers

DK Kijo Bisimba aifungukia adhabu ya kifo

0

bisimba Mkurugenzi Mtendai wa Kituo cha Haki za Binadamu Tanzania (LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba

Elvan Stambuli, Amani

Dar es Salaam: Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Haki za Binadamu Tanzania (LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba amefungukia adhabu ya kifo kwa kunyongwa nchini na kushauri kuwa sasa ifutwe.

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake, Kijitonyama jijini Dar, hivi karibuni Dk Kijo Bisimba alisema adhabu hiyo inafaa kufutwa kwa sababu inakiuka haki za binadamu.

“Kwanza hapa nchini haitekelezwi na inawafanya waliohukumiwa kunyongwa kuishi kwa wasiwasi wakati wote gerezani,” alisema mkurugenzi huyo.

DK Kijo BisimbaAlifafanua kwamba, kuna baadhi ya watu huwa hawamuelewi anaposema hivyo, lakini alisema wanachotetewa wao ni thamani ya utu na uhai kutolewa bila kujali nani anayetoa uhai huo.

“Uhai wa binadamu ni lazima ulindwe, ni vema badala ya mtu kuhukumiwa kunyongwa, apewe kifungo cha maisha jela ili iwe fundisho kwa watu watakaokuwa wanamuona akitumikia kifungo hicho, kumuua mkosaji ni sawa na kutenda kosa lilelile,” alisisitiza daktari huyo.

Alisema kuna baadhi ya nchi mkosaji wa mauaji anahukumiwa kifungo cha maisha lakini kinakuwa na miaka inayotajwa.

“Baadhi ya nchi sheria zao zinatamka miaka ya kukaa jela kama ni miaka 20, 30 na kadhalika,” alisema.

Nchini Tanzania mtu anayepatikana na hatia ya kuua kwa makusudi huhukumiwa kunyongwa hadi kufa na tayari wafungwa wengi wameshapewa adhabu hiyo na mahakama lakini utekelezaji wake kwa walio wengi haujafanyika kutokana na marais wanaokuwa madarakani kutosaini hati ya utekelezaji, jambo ambalo kiongozi huyo analipinga kwani linamfanya mfungwa kuishi kwa jakamoyo.

Leave A Reply