The House of Favourite Newspapers

Dkt. Hashil Abdallah Aongoza Kikao Kazi Cha Wataalamu Kamati Ya Biashara

0
NAIBU Katibu Mkuu Viwanda na Biashara katika Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Hashil T. Abdallah

NAIBU Katibu Mkuu Viwanda na Biashara katika Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Hashil T. Abdallah kwa niaba ya Katibu Mkuu Prof. Godius Kahyarara ameongoza mkutano wa ngazi ya wataalamu ulioshirikisha wadau mbalimbali kutoka Tanzania na Kenya kujadili Vikwazo visivyo vya kiushuru (NTB’s) vilivyopo baina ya nchi hizi mbili.

 

Kikao hicho kimefanyika leo tarehe 11 Machi, 2022 Visiwani Zanzibar ni muendelezo wa Vikao vya kuanzia ngazi ya wataalamu vilivyoshirikisha nchi ya Tanzania na Kenya kuanzia tarehe 9 Machi, 2022 hadi tarehe 12 Machi, 2022 ambapo Mawaziri wa sekta husika baina ya Tanzania na Kenya watakutana kwa ajili ya kuja na majibu ya pamoja kuhusu umalizwaji wa Vikwazo visivyo vya kiushuru.

Dkt. Abdallah amesema kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Prof. Godius Kahyarara amekuwa na Imani kubwa na kamati hii iliyohusisha wataalamu wa Tanzania na Kenya katika kuhakikisha wanafanya majadiliano kwa kina na kitaalamu zaidi ili kufikia makubaliano ya kuondoa vikwazo hivyo ili kurahisisha biashara baina ya Nchi hizi hizi mbili.

 

Dkt. Abdallah amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Kenya Uhuru Kenyatta wamekuwa wakijadiliana namna bora ya kumaliza changamoto hizi za kibiashara ili kukuza biashara na kuchochea uchumi wa Tanzania na Kenya pamoja na kukua kwa kasi na kutumia vizuri masoko ya SADC, AGOA na AfCFTA.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Mifugo kutoka Serikali ya Jamhuri ya Kenya Bw. Harry Kimutai amesema kuwa ni wakati sasa wa Tanzania na Kenya kuonesha mshikamano uliokuwepo kipindi kirefu. Bw. Kimutai ameongeza kuwa Tanzania na Kenya zimekuwa na mahusiano mazuri ya kibiashara kwa kipindi kirefu na changamoto hizi zimekuwa zikifanyiwa kazi na kupunguzwa mara kwa mara hivyo amesema ni wakati sasa wa kuionesha Afrika na Dunia kwa ujumla kuwa sisi ni ndugu.

Kikao hiki kimehudhuria na Viongozi mbalimbali kutoka Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt. Islam Seif, Katibu Mkuu anayeshughulikia biashara kutoka Wizara ya Viwanda, Biashara na Maendeleo ya Ujasiliamali kutoka Kenya Dkt. Bruno Linyiru,  Balozi Fatma Mohamed Rajah Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kutoka Tanzania na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasiri na Utalii Bw. Juma S. Mkomi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Kikao hiki cha majadiliano kitaendelea kesho ambapo kitawakutanisha pamoja mawaziri wa Wizara za kisekta kutoka Tanzania na Kenya na kuja na majumuisho na hitimisho la umalizwaji wa vikwazo visivyo vya kibiashara baina ya Tanzania na Kenya.

Leave A Reply