The House of Favourite Newspapers

Dkt. Mathayo Ataka Same Magharibi Wamuunge Mkono JPM

Mbunge wa Jimbo la Same Magharibi  CCM Dkt. Mathayo David Mathayo, akizungumza na wananchi wa jimbo lake.

MBUNGE  wa Jimbo la Same Magharibi  (CCM) Dkt. Mathayo David Mathayo, amewaomba wananchi wa  jimbo hilo kumuunga mkono na kumuombea afya njema Rais John Magufuli ili aweze kuiongoza Tanzania katika maendeleo makubwa zaidi na kurudisha nidhamu katika sekta mbalimbali za huduma nchini.

 

Ametoa kauli hiyo katika siku ya kwanza ya ziara yake ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020 kama alivyoahidi wakati akiomba ridhaa ya kuwaongoza wananchi wa jimbo hilo.

 

Dkt. Matayo alikuwa akizungumza na wananchi wa kata za Msindo, Mshewa na Mhezi, ambapo amesema serikali ya awamu ya tano imeonyesha mafanikio lukuki katika nyanja mbalimbali.

 

Aidha, amekabidhi vifaa mbalimbali alivyoahidi katika kata hizo zikiwemo pia fedha taslimu huku akitoa rai kwa uongozi wa kila kata kuhakikisha vifaa hivyo vinatumika kikamilifu ndani ya kipindi cha miezi mitatu.

…Akiendelea kufafanua masuala mbalimbali katika ziara hiyo.

 

Vilevile, wananchi wa kata hizo wamemshukuru mbunge huyo kwa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi huku wakibainisha kuwa msaada huo utasaidia kutatua kero zao za muda mrefu.

 

Katika kata ya Msindo, mbunge huyo ametoa fedha, mifuko ya saruji na mabomba ya maji, ambapo katika kata ya Mshiwa amekabidhi mifuko ya saruji na fedha taslim Sh. milioni 13.9 kwa ajili ya shughuli za maendeleo.  Pia ametoa Sh. mil. 9 katika kata ya Mhezi ikiwemo mifuko ya saruji.

Comments are closed.