The House of Favourite Newspapers

Dogo amcharanga mapanga kaka’ke!

Unyama (3)Haruni Sadiki aliyecharangwa mapanga na mdogo wake.

Gabriel Ng’osha
Inasikitisha sana! Kijana Haruni Sadiki (24), mkazi wa Jangwani, Dar, amenusurika kuuawa kwa kucharangwa mapanga na mdogo wake aitwaye Abdurazaki Bakari ‘Riziki’ (22).

Akizungumza akiwa na maumivu makali kwenye Hospitali ya Muhimbili, Haruni aliliambia gazeti hili kuwa chanzo cha tukio hilo ni ugomvi uliotokea kati ya wanandugu hao.

Unyama (2)Sehemu ya jeraha kichwani mwa Haruni Sadiki aliyecharangwa mapanga.

“Kuna mdogo wetu anaitwa Hemed (5), alikuwa na tabia ya kukojoa kitandani. Nakumbuka siku ya tukio yule mtoto alikojoa kama kawaida ndipo ukaibuka ubishi kati ya Riziki na kaka yetu mwingine aitwaye Nasri.

“Nasri alitaka Hemed (aliyekojoa) atembezwe mtaani na godoro kichwani huku akipigiwa ngoma lakini Riziki hakutaka mtoto afanyiwe hivyo badala yake alitaka ampige ndipo ukaibuka utata kati yao.

Unyama (1)Mtuhumiwa, Abdurazaki Bakari ‘Riziki’

“Baada ya malumbano, walijikuta wakigombana ndipo nikawaamulia. Katika kuwaamulia nikampiga ngumi Riziki kwa bahati mbaya, jambo lililomchukiza na kuahidi kulipiza kisasi.

“Maisha yaliendelea kama kawaida Riziki akiwa na kinyogo hadi aliponiomba twende sehemu tulivu tuzungumze jambo, nikakubali, cha ajabu akawa ananipeleka kwenye jumba bovu.

“Tulipofika kwenye jumba hilo alianza kunipiga na kuniuliza kwa nini nilimpiga ngumi, nilijua ni utani, nikamsukuma akaanguka ndipo akachomoa panga kiunoni na kunicharanga.

“Alinikata kisogoni, nikaanguka, akanikata vidole viwili vya mguuni, alipoona napiga mayowe ya kuomba msaada akatoweka.

“Bahati nzuri wasamaria wema walinikimbiza Hospitali ya Amana kisha nikahamishiwa Muhimbili ambapo iliwalazimu kumalizia nusu ya kiganja kilichokuwa kinaning’inia,” alisema Haruni.

Mtuhumiwa amefunguliwa jalada la kesi Namba ILA/RB/3847/15- SHAMBULIO LA KUDHURU MWILI na anasakwa na polisi.

Comments are closed.