The House of Favourite Newspapers

DONGE LA BILIONI MOJA LA MO LAIBUA KIZAAZAA

Image result for BABA MO AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI

TUKIO la mfanyabiashara Mohammed Dewji (pichani) aliyetekwa hivi karibuni na watu wasiojulikana limekuwa likichukua sura mpya kila siku ambapo baada ya familia yake kutangaza kuwa, yeyote atakayefanikisha kupatikana kwake atapewa donge la shilingi bilioni moja, kizaazaa kimeibuka mtaani.  

Kizaazaa hicho kimetokana na uamuzi wa familia ya Mo kupitia kwa mmoja wa wanafamilia, Azim Dewji juzi kuongea na waandishi wa habari na kusema:

“Kwanza kabisa tunamshukuru Mwenyezi Mungu na pili tunashukuru serikali kwa jitihada inazozifanya kuhakikisha ndugu yetu anapatikana. Tunashukuru vyombo vya habari, taasisi za dini kwa maombi na kutufariji, tunaomba muendelee kutuombea.

 

“Katika kuhakikisha ndugu yetu Mo Dewji anapatikana, familia itatoa shilingi bilioni moja kwa atakayefanikisha kupatikana kwa mtoto wetu. Taarifa itakayotolewa itabakia kuwa siri ya mtoa taarifa na familia.”

 

MAPOKEZI YA TAARIFA HIYO

Baada ya familia hiyo kutangaza donge nono hilo, watu mbalimbali wamekuwa wakipiga simu kwenye chumba chetu cha habari kutaka ufafanuzi huku wengi wakionesha kuzitamani pesa hizo. “Hivi ndugu yangu na umasikini wangu huu mara namuona Mo sehemu, si ndiyo nitakuwa nimeuaga? Sasa hebu nielekezeni vizuri jinsi ya kutoa hizi taarifa na nitakavyolipwa mkwanja wangu,” alisema kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Saidi Kisako wa Geita.

 

Naye John Felix wa Kinondoni jijini Dar alisema kuwa, baada ya kupata taarifa hizo alichanganyikiwa na kutamani kuacha kazi zake zote, aingie kazini kumsaka kama wanavyofanya polisi. “Jamani bilioni moja siyo pesa ndogo, hapa nilipo natamani kufanya kazi ya polisi, yaani niingie nyumba hadi nyumba, mtaa kwa mtaa, nichunguze, nipeleleze ili nifanikishe kupatikana kwake maana daah… nimepagawa na hilo donge,” alisema John. Mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Eunice Laurence kwenye Mtandao wa Facebook aliandika:

 

“Mimi nimechanganyikiwa kabisa, natamani wale wazungu wanaodaiwa kumteka wanipigie simu waniambie alipo kisha nitawatoa kimtindo.” Kufuatia ‘kimuhemuhe’ hicho, mwandishi wetu alifanya uchunguzi na kubaini kuwa donge hilo limezua kizaazaa kwani kila mtu anahaha kutafuta taarifa zitakazofanikisha kupatikana kwa Mo.Image result for BABA MO AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI

“Huwezi kuamini tangu donge nono hilo limetangazwa, hapa mtaani ni kizaazaa, kila mtu anataka kuvaa kilemba cha upelelezi, hii bilioni moja itawatoa watu macho aisee,” alisema Joachin Khan wa Magomeni jijini Dar ambaye alidai akiipata pesa hiyo, anaacha kazi anayofanya na kuanza biashara.

 

TUJIKUMBUSHE KIDOGO

Mfanyabiashara Mo ambaye pia ni mwekezaji wa Klabu ya Mpira wa Miguu ya Simba ya jijini Dar alitekwa Alhamis iliyopita saa 11 alfajiri alipokuwa akiingia ‘gym’ katika Hoteli ya Colloseum iliyopo Oysterbay jijini Dar kwa ajili ya kufanya mazoezi binafsi kama kawaida yake.

 

Jeshi la polisi kupitia kwa Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Lazaro Mambosasa alieleza kuwa jitihada za kuhakikisha Mo anapatikana zinaendelea na wananchi washiriki katika kutoa taarifa za kumpata bilionea huyo ambaye mpaka gazeti hili linakwenda mtamboni alikuwa hajulikani alipo.

Stori:Mwandishi Wetu, RISASI MCHANGANYIKO

Comments are closed.