The House of Favourite Newspapers

Dr. Mayrose Akemea Mbowe Kushambuliwa

0

DAR ES SALAAM: KADA wa Chadema ambaye ametangaza nia ya kugombea urais, Mayrose Majinge ameonesha masikitiko yake kufuatia taarifa za mwenyekiti wa chama chake, Freeman Mbowe kushambuliwa na watu wasiojulikana.

 

Dr. Mayrose amefunguka hayo mapema leo alipokuwa akizungumza kwenye kipindi cha Front Page kinachorushwa na +255GlobalRadio kuhusu mambo mbalimbali kuelekea Uchaguzi Mkuu, Oktoba 2020.

 

Alisema, ameshtushwa na tukio hilo ambalo limetokea jana jioni wakati kiongozi huyo alipokuwa akirejea nyumbani kwake mjini Dodoma.

 

“Kuna habari za kushtusha kuhusu mwenyekiti wetu wa chama, nimesikia amejeruhiwa vibaya sana. Kwa watu wenye mapenzi mema tuungane kukataa vitendo hivi. Mimi binafsi nimesikitishwa, nimehuzunishwa na ninakemea sana,” alisema Dr. Mayrose.

 

Taarifa za Mbowe kuvamiwa jana zimethibitishwa leo na Kamanda wa Polisi Dodoma, Gilles Muroto ambaye amesema jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo.

 

“Ni kweli Mhe. Freeman Mbowe amevamiwa na watu watatu wakamkanyaga kanyaga na kumvunja mguu wa kulia kwa sasa yuko Ntyuka wodi no 4 na anaendelea vizuri, bado tunaendelea kuchunguza tutawajulisha baadaye,” alisema Muroto.

 

Kwenye mahojiano yake na Front Page, Dr. Mayrose alisema suala la yeye kutangaza mapema nia yake mapema na kuonekana amekiuka taratibu za chama halina mashiko.

 

“Hakukuwa na suala la kukikuka chama mimi kutangaza mapema na mimi kama mtoa nia nilitoa tangazo langu kama mtu mwenye nia. Suala la chama watafute watu wa chama. Mimi sio msemaji wa chama, niulize kuhusu nia yangu mimi nitakujibu. Mimi nimetangaza nia yangu,” alisema Dr. Mayrose.

 

Dr. Mayrose aliwazungumzia pia wale wanaomsema ameibuka ghafla tu na kutangaza azma yake hiyo ya kuutaka urais.

 

“Nimeanza maandalizi tangu miaka mingi tangu mwaka 2006, kwa hiyo sio kwamba nimekuja ghafla watu hawajui tu,” alisema Dr. Mayrose na kuongeza.

 

“Mimi nikipata ridhaa ya kuwa Rais, watu watarajie kuona maisha yenye furaha na yenye udugu, uhuru na umoja. Mimi naamini kuishi ni kufurahi, naamini katika kusikilizana. Katika kusikilizana ndio tunatambuana mimi ni nani na wewe ni nani, kila mtu ni muhimu sana.”

 

Stori: Erick Evarist, Risasi Mchanganyiko

Leave A Reply