The House of Favourite Newspapers

DSTV Chupuchupu Wale Kichapo Kwa Global FC

0
Kikosi cha timu ya Global FC kilichoanza dhidi ya DStv leo Jumapili Januari 31, 2021 kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

UNAWEZA ukasema watasimulia waendako, mara baada ya kikosi bora na ghali cha Kampuni ya Global Group, Global FC  kuupiga mwingi dhidi ya timu ya Kampuni ya Multichoice, DStv ambao waliponea chupuchupu kula kichapo kwenye mchezo wa kirafiki uliochezwa leo Jumapili Januari 31, 2021 kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

 

Mchezo huo uliokuwa mkali ulimalizika kwa sare ya bao 3-3 huku DStv wakifanya kazi ya kusawazisha mabao hayo. Global FC walikuwa wa kwanza kuandika bao la uongozi kwa mpira wa kutengwa uliopigwa na nyota wa timu hiyo Saleh Ally ‘Jembe’ na kuzamishwa kimiani na mshambuliaji Abdulghafary Ally.

Kikosi cha DStv kilichoanza dhidi ya Global FC

Hadi mapumziko Global FC walitoka na mtaji wa mabao 2-1. DStv wao walipata mabao mengine mawili ya harakaharaka na kupata uongozi wa 3-2 kisha Abdulghafary akasawazisha kwa upande wa Global na kuwa 3-3 hadi dakika 90.

 

Baada ya matokeo hayo ya sare kituko ni kwamba refa aliamua zipigwe penalti ili mshindi apatikane lakini DStv wakakataa kabisa.

Mhariri mtendaji wa Global Publishers, Saleh Ally (kushoto) akimtoka mchezaji wa Dstv (katikati).

Baada ya mchezo zilitolewa zawadi kwa wachezaji waliofanya vizuri, wakiwemo wafungaji bora na mchezaji bora wa mechi hiyo kisha viongozi wakatoa neno la shukran na kufuatia zoezi la chakula na vinywaji kwa pande zote mbili.

 

Zawadi ya Mchezaji Bora wa Mechi (MOTM) ilienda kwa nyota wa Global FC, Thomas Mselemu ambapo DStv walimpa beki lenye vifaa mbalimbali likiwemo begi sawa na ile ya mfungaji bora, Abdulghafary aliyefunga mawili huku Saleh akipewa tuzo ya heshima ya mchezaji mzee.

Kwa upande wa kiongozi wa Global, Saleh Jembe alisema: “Imekuwa jambo nzuri kwa hiki ambacho kimefanyika hapa, lengo ilikuwa ni kudumisha ushirikiano, mchezo ulikuwa mzuri sana na tumewalaza na viatu na mmefanya jambo la maana kugoma kupiga penalti maana msingepata hata moja.

 

“Matumaini yangu tutacheza tena mchezo mwingine kabla ya mwaka huu kuisha ili tujue nani mbabe wa kweli, ingawa mnaondoka na kumbukumbu kuwa tumewalaza na viatu kwa sababu kila kitu tumewazidi kwenye mchezo huu,” alisema Jembe.

Kwa upande wa Multichoice, Mkuu wa Mahusiano wa kampuni hiyo, Johnson Mshana alisema: “Kwanza nitumie nafasi hii kuwapongeza Global Publishers kwani kuja kwenu hapa kumeonyesha kuwa ushirikiano wetu ni wa maana ndiyo hadi Saleh amekuja na kushiriki hadi mwisho, Hata mimi kuja kwangu kuna maana ile ile.

“Hivyo naomba ushirikiano wetu uendelee kudumu daima na tuwe tunakutana kwenye michezo kama hii kwa ajili ya kudumisha ushirikiano na umoja wetu,” alisema Mshana.

Stori na Issa Liponda | GPL

KUMEKUCHA! ZUCHU ALIVYOTINGA Kwa MKAPA Kupiga SHOO ya KIBABE, FAINALI SIMBA vs TP MAZEMBE

Leave A Reply