The House of Favourite Newspapers

Epuka Vyakula Hivi Ndani ya Mwezi wa Ramadhani

KUNA aina sita za vyakula na ulaji ambao mfungaji anashauriwa kuepuka ili kulinda afya yake wakati huu wa mfungo wa Ramadhani, vyakula hivyo ni kama ifuatavyo:

Vyakula vya kukaanga na vyakula vya mafuta mengi kama chips, sambusa, biriyani, pilau na kadhalika vinafaa kuepukwa kwa sababu vina calories nyingi na virutubisho vichache hivyo kusababisha mlo uwe usio na uwiano. Hii husababisha shibe isiyo na faida na huongeza uchovu wakati wa Ramadhani kwa mfungaji.

Pia mfungaji aepuke kula vyakula vilivyo na chumvi nyingi kama achari pickles, sauces, chips na kadhalika kwa sababu chumvi hunyonya maji mwilini. Kutokana na unywaji mchache wa maji ndani ya Ramadhani, utumiaji wa chumvi nyingi unaweza kusababisha upungufu wa maji mwilini, kitaalamu huitwa dehydration na udhaifu wa mwili ndani ya Ramadhani

Mfungaji pia aepuke kula vyakula na vinywaji vilivyo na sukari nyingi kama soda, pipi, vinywaji vya kuongeza nguvu n.k. Ingawa vinaweza kukupa nguvu ya haraka lakini vyakula hivi vina virutubisho hafifu sana visivyo na manufaa mwilini. Pendelea juisi ya matunda.

Chai na kahawa kupita kiasi wakati wa daku ikitumika kwa wingi ni aina ya vinywaji ambavyo huchochea kiwango kikubwa cha maji na chumvi kuchujwa kupitia njia ya mkojo. Hii husababisha madini, maji na chumvi ambavyo vingehitajika mwilini wakati wa mchana kupotea kupitia njia ya mkojo.

Mara baada ya kula chakula wakati wa futari au daku mwili unahitaji muda kumeng’enya chakula. Subiri kwa saa mbili baada ya kula kabla hujalala.

Kula sana kunaweza kukuletea matatizo ya kimetabolitiki kama kushuka au kupanda sukari katika damu na kupungukiwa maji. Kula vyakula vilivyo na fibres (nyuzinyuzi) za kutosha wakati wa daku. Hivi ni vyakula vinavyopatikana katika

nafaka na mbegumbegu mfano mtama, matunda safi, mboga za majani na mkate wa nafaka zisizokobolewa. Unashauriwa kunywa maji mengi Ili kupunguza gesi inayoweza kuletwa na vyakula vilivyo na nyuzinyuzi (fibres). Kwa kawaida tende, maji na juisi hutumika wakati wa kufuturu.

Tumia tende tatu na juisi glasi moja ili ikusaidie  kurudisha sukari katika hali ya kawaida mwilini na kukupa nguvu ya haraka. Baada ya futari kunywa maji glasi nane kidogo kidogo kabla ya daku ili kurudisha maji mwilini.

Chagua nyama zilizo na mafuta kidogo, kama ni kuku, ondoa ngozi yake na mafuta yanayoonekana wazi kabla ya kupika nyama za aina nyingine. Ni vema kuoka au kuchoma vyakula badala ya kuvikaanga na kama utalazimika kukaanga punguza kiwango cha mafuta unayotumia.

Kula taratibu na hakikisha unatafuna chakula vizuri kabla ya kumeza, watu wengi wana tabia ya kula chakula kingi kwa haraka hivyo kusababisha matatizo ya tumbo. Kumbuka inachukua hadi dakika 20 kwa tumbo lako kuujulisha ubongo kuwa umeshiba.

Jenga tabia ya kutembea kwa angalau dakika 30 kila siku baada ya saa moja baada ya futari kwani husaidia mwili kubadilisha maji na chakula ulichokula kwa faida ya mwili. Ni vizuri chakula cha futari kikawa chepesi.

Comments are closed.