The House of Favourite Newspapers

EU Yatangaza 15 Watakaoshiriki European Youth Film 2017

0
Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini, Roeland van de Geer, akizungumzia shindano hilo.
Washiriki 15 wakiwa na waandaaji.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa Bodi ya Filamu nchini, Wilhadi Tairo, akizungumza kwa upande wa Serikali kuhusu shindano la European Youth Film 2017.

UMOJA Ulaya (EU) nchini umetangaza majina ya washiriki 15 walioshinda ambao wataendelea kuwemo kwenye shindano la European Youth Film 2017 lililoandaliwa na umoja huo kwa kushirikiana na balozi za Uholanzi, Uingereza, Ujerumani na Serikali ya Tanzania.

Washiriki ambao wamefuzu ni Christine Pande, Cornel Mwakyanjala, Daniel Manege, Dennis Chacha, Dosi Said Dosi, Florence Mkinga, Francis Nyerere, Franch Machiya, Freddy Feruzi, Karim Michuzi, Kherry Kafuku, Louis Shoo, Malik Hamis, Rashid Songoro, Taragwa Marwa na Wambura Nyingana.

Akizungumza kuhusu shindano hilo, Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) nchini, Roeland van de Geer, alisema washiriki hao wamechaguliwa kutokana na filamu walizotengeneza na kwamba lengo la kuanzisha shindano hilo ni kuiwezesha Tanzania kuwa na watengenezaji bora wa filamu.

“Kabla ya kuanza kutengeneza filamu washiriki walipewa mafunzo ya siku tatu kuhusu kutengeneza filamu, lengo ni Tanzania iwe na filamu bora si kuleta filamu kutoka Ulaya ila kuboresha filamu za Tanzania kupitia vijana ambao ndiyo sehemu kubwa ya Watanzania,” alisema Geer.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa Bodi ya Filamu nchini, Wilhadi Tairo, alisema shindano hilo limekuja kwa wakati muafaka kwani ili soko la filamu liwe imara linahitaji kuwa na watu wa aina zote wenye uwezo wa kushiriki nafasi zote za kwenye filamu.

“Filamu zinahusisha watu wa aina zote awe mtoto au mkubwa na kama hakuna watu wa aina zote hapo kutakuwa na upungufu, kwa hiyo nawashukuru Umoja wa Ulaya na washirika wao kwa kuleta shindano hili kwa muda mwafaka,” alisema Tairo.

Shindano hilo la European Youth Film 2017 linatarajiwa kumalizika mwezi Septemba na mshindi wa kwanza atapewa zawadi ya Sh. milioni saba, mshindi wa pili milioni tano na mshindi wa tatu milioni tatu.

Hata hivyo filamu hizo zilizotengenezwa zitapewa nafasi ya kuangaliwa na wananchi ili kuchagua filamu iliyopendwa zaidi ikiwa na lengo la kuwashirikisha lakini si lengo la kumchagua mshindi bali ni kujua filamu itakayopendwa zaidi.

“Filamu zinazotengenezwa zitapata nafasi ya kupelekwa mtaani kuangaliwa na wananchi ili tupate nafasi ya kujua filamu ipi imependwa zaidi na watazamaji,” alisema mmoja wa waratibu Mussa Sakar.

Na Hamida Hassan/GPL

Leave A Reply