The House of Favourite Newspapers

EWURA Yaridhishwa Na Kazi Ya Utengenezaji Wa Matela Ya Kusafirisha Mabomba Ya Mradi Wa EACOP

0
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Profesa , Mark Mwandosya ( wa pili kulia) akisikiliza maelezo ya hatua iliyofikiwa ya matengenezo ya matela maalum kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Superdoll Seif Seif wakati alipotembelea karakana inayotengeza matela hayo yatakayotumika kusafirisha mabomba ya mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika la Afrika Mashariki (EACOP).

Bodi ya Wakurugenzi  wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini (Ewura), imesema kuwa imeridhishwa na utekelezaji wa mradi wa utengenezaji wa matela maalum 300 unaofanywa na kampuni ya Superdoll kwa ajili ya kusafirisha mabomba ya mradi wa bomba la Mafuta Ghafi la Afrika ya Mashariki (EACOP) pindi yatakapowasili nchini.

Ewura ndio walitoa kibali cha mradi wa bomba hilo la mafuta ghafi (EACOP) kwa upande wa Tanzania litakaloanzia Hoima nchini Uganda hadi Pwani ya Chongoleani mkoani Tanga, likiwa na urefu wa kilomota 1443 na kati ya hizo, kilomita 1147 zipo upande wa Tanzania.

Akizungumza kwa niaba ya bodi hiyo iliyoongozwa na Mwenyekiti wake Mark Mwandosya katika ziara ya kutembelea karakana ya Superdoll iliyopo barabara ya Nyerere Road mkoani Dar es Salaam, mmoja wa wajumbe wa bodi hiyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati Haruna Masebu amesema wameridhishwa na kazi ya utengenezaji wa matela hayo maalum yenye urefu wa mita 18.

Amesema kati ya matela 300 ,matela  217 tayari yameshatengenezwa na mengine yaliyobaki yapo katika hatua nzuri za umaliziaji,”

Sehemu ya matela 300 yatakayotumika kubeba mabomba ya mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika ya Mashariki ( EACOP) yakiwa yameegeshwa baada ya kuungwanishwa na vichwa vya Scania katika karakana ya Superdoll jijini Dar es Salaam.

”Haya matela yanatengenezwa kwa kibali maalum kwa ajili ya kazi ya usafirishaji wa mabomba kwenda kwenye maeneo husika yatakayopita Mkuza.“

“ Ewura, tukiwa kama mmoja wa wadau muhimu wa serikali katika kusimamia utekelezaji wa mradi huu, tumeridhishwa na kazi na viwango vya matela haya yenye vifaa maalum kwa ajili ya usalama wa barabarani.“

“Lakini pia tunafurahia kuona kampuni hii ya wazawa ikihusika katika kazi hii, kama sehemu ya sera ya nchi (Local Content) katika kuhakikisha wazawa wanashiriki kikamilifu katika ujenzi wa miradi hapa nchini,” amesema.

Naye Meneja wa Petroli kutoka Ewura, Gevald Maganga amesema waliamua kutembelea karakana hiyo ya Superdoll ili kuona maendeleo ya kazi hiyo, ambayo kwa kiasi kikubwa imefanyika kwa ufanisi na kuzingatia viwango vya kimataifa, kama mradi wa EACOP unavyotaka.

Naye Mkurugenzi wa Superdoll, Fulgence Bube amesema magari hayo yameombewa kibali maalum na wameshirikisha idara mbalimbali za serikali wakiwemo Wakala wa Barabara (Tanroads) ili kuhakikisha yanakidhi vigezo vya kupita katika barabarara bila kufanya uharibifu na kuzingatia usalama wa watuamiaji wengine wa barabara.

Pia amesema magari mapya aina ya Scania yatakayovuta matela hayo yatatembea katika spidi 50, yakiwa na vifaa maalum vyenye kuakisi mtetemeko ili kuyalinda yasiharibike.

Pia amesema magari hayo yana kamera ili kuyafuatilia yakiwa njiani na kuhakikisha madereva wanafuata taratibu zote za usalama barabarani.

Katika kuhakikisha msafara wa magari hayo hautasababisha foleni, Bube amesema wataruhusu magari 20 tu kwa siku ili kuondoa usumbufu huo kwa sababu ya urefu wake.

”Haya matela yana urefu wa mita 18, ukijumlisha na Cabin ( kichwa) yanaweza kufikia hadi mita hadi 20, hivyo ni marefu sana ukilinganisha na malori yenye urefu wa kawaida wa mita 12,” amesema.

Naye Busegi Kulwa, Meneja wa Rasilimali watu wa ndani ( Local Content) wa kampuni ya East African Logistics Services (EALS) Limited, inayoshirikiana na Superdoll katika kazi hiyo kupitia kampuni yake ya Superstar, amesema matarajio ni kumaliza matela yaliyobaki ndani ya kipindi kifupi ili kazi hiyo ianze mara moja.

Kwa mujibu wa Meneja wa Vibali na Taratibu wa EACOP, Ezra Kavana, wanategemea mabomba hayo kuanza kuwasili nchini kabla ya mwisho wa mwaka huu kwa ajili ya kuanza kazi ya kuchimba mkuza ambapo mabomba hayo yakishafukiwa, shughuli nyingine zitaendelea kama kawaida.

Mabomba hayo yatapita katika mikoa nane ya Tanzania Bara ambayo ni Shinyanga, Geita, Kagera, Tabora, Manyara, Dodoma na Tanga, ikijumlisha jumla ya wilaya 24, Kata 134 na vijiji zaidi ya 180.

Lengo la mradi ambao tayari umelipa fidia kwa walioguswa (PAPs) ni kuwezesha usafirishaji wa mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanzania ambapo yatahifadhiwa katika maghala maalumu katika Pwani ya Chongoleani mkoani Tanga kwa ajili ya kusafishwa na kuuzwa katika soko la kimataifa.

Leave A Reply